Kituo cha Polisi Tazara ‘chawaruka’ washtakiwa kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

  • Shahidi wa nne katika kesi ndogo ndani kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ameieleza mahakama kuwa washtakiwa Mohamed Ling’wenya na Adam Kasekwa hawakuwahi kufikishwa katika Kituo cha Polisi Tazara kama walivyodai.


Dar es Salaam. Shahidi wa nne katika kesi ndogo ndani kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ameieleza mahakama kuwa washtakiwa Mohamed Ling’wenya na Adam Kasekwa hawakuwahi kufikishwa katika Kituo cha Polisi Tazara kama walivyodai.

Inspekta Issa Maulid, ambaye ni kaimu mkuu wa Kituo cha Polisi Tazara alieleza hayo katika Mahakama Kuu (Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi) mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi iliibuka baada ya mshtakiwa wa tatu, Mohamed Abdillahi Ling’wenya kupinga maelezo ya onyo yaliyotolewa na shahidi wa Jamhuri, SP Jumanne akidai hakuwahi kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam na kwamba alilazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyatoa.

Washtakiwa hao wamekuwa wakidai walihifadhiwa katika Kituo cha Polisi Tazara tangu walipofikishwa Dar es Salaam wakitokea Moshi, Kilimanjaro walikokamatwa kwa tuhuma za kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi.

Akiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando shahidi huyo alieleza kuwa yeye ni askari polisi katika Kikosi cha Reli Tazara, Barabara ya Pugu.

Shahidi huyo alidai Agosti 2, 2020 alipokea barua ya kukaimu nafasi ya Mkuu wa Kituo cha Polisi, Tazara baada ya aliyekuwepo, Richard Obutu kwenda likizo ya siku 20.

“Katika utekelezaji wa majukumu kuna aina tofauti ya vitabu vinavyotumika kuhifadhi taarifa mbalimbali.

“Kuna kitabu cha kufungulia taarifa, kitabu cha kuandika kumbukumbu za mahabusu (DR) na kitabu cha kunakili mali anazokutwa nazo mtuhumiwa baada ya upekuzi.

Shahidi huyo aliendelea kudai, Agosti 7, 2020 alifanya ukaguzi katika mahabusu ya kituo hicho na kwamba siku hiyo hapakuwa na mtuhumiwa hata mmoja.

Alidai alifanya tena ukaguzi Agosti 8, 2020 ambapo palikuwa na mtuhumiwa mmoja mwanamume aliyejifanya mtumishi wa Serikali na Agosti 9, 2020 palikuwa na watuhumiwa wawili wanafunzi waliotuhumiwa kufungua nati za reli.

“Kama zilivyo taratibu, asubuhi lazima kupitia vitabu vya kumbukumbu na katika ukaguzi nilijiridhisha mahabusu hao wapo na uthibitisho wangu mkubwa katika ukaguzi ni kitabu cha kumbukumbu za mahabusu (DR),” alidai.

Alipoulizwa iwapo washtakiwa walioko mahakamani--Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya--walikuwepo kituoni hapo Agosti 7, 8 na 9 2020, shahidi huyo alidai siku hiyo hapakuwa na mshtakiwa kituoni hapo.

Shahidi huyo aliendelea kudai, Novemba 14, 2021 akiwa ofisini kwake Tazara alifika mtu kutoka ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) aliyejitambulisha kwa jina la Inspekta Swilla aliyekuja kumweleza kuwa kitabu cha kumbukumbu za mahabusu (DR) iliyotumika Agosti 7, 2020 kilikuwa kinahitajika mahakamani kwa ajili ya ushahidi.

“DR hiyo kwa kuwa ilikuwa imetumika na kuisha tangu Machi 2021, haikuwepo kwenye chumba cha mashtaka (CRO). Baada ya Swilla kuondoka nilirudi na kukitafuta na nilipoikagua nikakuta Agosti 7, 2020 hapakuwa na mahabusu, Agosti 8, 2020 palikuwa na mmoja na Agosti 9 palikuwa na wawili,” alidai.

Baada ya utambuzi wa kitabu hicho, mawakili wa washtakiwa hawakuwa na pingamizi lolote na hivyo kuruhusu mahakama kukipokea kama kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya mawakili wa utetezi na shahidi huyo wa upande wa mashtaka:-

Wakili Jeremiah Mtobesya: Mliandikishiana popote mlipokabidhiana DR (kitabu cha kumbukumbu za mahahusu)?

Shahidi: Ndiyo.

Mtobesya: Mara ya mwisho kufanya ukaguzi ni tarehe ngapi?

Shahidi: Tarehe 10 mwisho.

Mtobesya: (Kitabu) Ulikiacha wapi?

Shahidi: Charge Room Office (chumba cha mashtaka).

Mtobesya: Kuanzia Septemba 6, 2020 ulikitumia lini tena kitabu hicho?

Shahidi: Sijakitumia tena hadi leo nilivyokuja mahakamani.

Mtobesya: Wakati unatambua kitabu hiki kuna sehemu ulitaja WEF, uliieleza maana yake?

Shahidi: Sikueleza.

Wakili: Wakati unaongozwa na wakili Kidando kuna namba imeandikwa mwanzo na kurudiwa, ulimweleza jaji?

Shahidi: Sikumweleza.

Ilifuata zamu ya Wakili wa Utetezi John Mallya: Unatambua kuwa makosa ya ugaidi ni serious (makubwa)?

Shahidi: Ndiyo, ni serious.

Mallya: Kunapotokea makosa ya ugaidi polisi wanaweza kuchukua hatua ya dharura kudhibiti?

Shahdi: Ndiyo.

Mallya: DCI akikwambia nina dharura na nina watu wangu ambao ni magaidi unaweza kukataa (kuwapokea)?

Shahidi: Kwa mamlaka ya DCI vituo vyote viko chini ya DCI, nitamkubalia with conditions (na masharti).

Wakili wa utetezi Fredrick Kihwelo: Ukipewa maelekezo ya kuhifadhi watuhumiwa utatekeleza au hutatekeleza?

Shahidi: Nitatekeleza.

Kihwelo: Ni sahihi Agosti 7, 2020 ulipewa maelekezo ya kuwahifadhi Adam Kasekwa na Ling’wenya?

Shahidi: Si sahihi.

Kihwelo: Kuna nyaraka uliyoiwasilisha mahakamani kuthibitisha ulikaimishwa ukuu wa kituo?

Shahidi: Hapana.

Kihwelo: Ni sahihi Inspekta Swilla alikutembelea ofisini kwako tarehe 14?

Shahidi: Ni sahihi.

Kihwelo: Unakumbuka siku uliyotembelewa na Inspekta Swilla?

Shahidi: Sikumbuki.

Kihwelo: Mimi nasema ilikuwa Jumapili.

Shahidi: Ndiyo, sikumbuki vizuri.

Wakili wa utetezi Peter Kibatala: Unafahamu kwa utaratibu mshtakiwa akipokelewa pale CR anatakiwa apelekwe kwa daktari kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake kwa mujibu wa PGO namba 353?

Shahidi: Sijui.

Kibatala: Ni sahihi anaweza mtuhumiwa kusindikizwa na incharge (msimamizi mkuu)?

Shahidi: Ni sahihi lakini sio lazima apelekwe na incharge.

Kibatala: Shahidi unafahamu kuwa kawa hakuna mtuhumiwa kwa siku katika Kituo cha Polisi unatakiwa kutuma ripoti katika Fomu ya Polisi namba 172?

Shahidi: Ni sahihi.

Kibatala: Hili sharti la kupeleka taarifa katika Fomu ya Polisi namba 172 ni la hiari au lazima?

Shahidi: Ni lazima.

Kibatala: Umeizungumzia mahakamani hiyo Fomu ya Polisi namba 172?

Shahidi: Sikuizungumzia.

Kibatala: Alipokuja Inspekta Swilla alikueleza kuwa alitumwa na nani?

Shahidi: Alitumwa na DCI Camilius Wambura.

Kibatala: Swila alikueleza nini?

Shahidi: Alinieleza kuwa natakiwa kuja kutoa ushahidi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake na aliomba nimpatie DR ya Tazara.

Kibatala: Kwa hiyo kama isingekuwa maelekezo ya Camilius Wambura aliyompa Inspekta Swilla wewe hungeitoa DR hapa mahakamani?

Shahidi: Kwa mamlaka niliyonayo DR ninaweza kuichukua na kuileta bila kuomba CRO. Na DR hii ilikuwa imeshaisha na ilikuwa imehifadhiwa katika ofisi yangu. Ikiwa ni nyaraka ya Serikali na nikaambiwa inahitajika mahakamani na leo ndio nimekuja.

Kibatala: Shahidi kuna tofauti gani kati ya DR ya Central Police, Dar es Salaam na DR ya Kituo cha Polisi, Tazara?

Shahidi: Hakuna tofauti.

Kibatala: Vipi kuhusu kituo kidogo cha Polisi Kurasini, Yombo na Pugu vinatofautiana DR?

Shahidi: Vinatofautiana, vituo vya Yombo, Kurasini ni outpost (vituo vidogo) na inatumika na askari kubadilishana shift (zamu) na havina DR....DR ipo Kituo Kikuu cha Tazara ambacho ni Pugu Road.

Kibatala: Kuna malalamiko kuwa Agosti 7, 8, 9, aliletwa mshtakiwa Ling’wenya na hakukufuatwa utaratibu wa kumuingiza katika Kitabu cha Kumbukumbu (DR). Angalia kitabu chako wewe ulisaini Agosti 10, maana yake ilikuwa ni nini?

Shahidi: Nilisaini Agosti 10, 2020 kwa sababu ni siku ambayo nilifanya ukaguzi.

Kibatala: Na hiyo ilikuwa ni kabla au baada ya Agosti 8, 2020?

Shahidi: Na hiyo ilikuwa ni baada ya Agosti 7, 8, 9 siku ambazo zinadaiwa watuhumiwa waliletwa kituo cha Tazara, Pugu Road.