Kiwanda cha simu kujengwa Mwanza

Kiwanda cha simu kujengwa Mwanza

Muktasari:

  • Ili kurahisisha upatikanaji na kupunguza bei, Serikali mesema inakamilisha mchakato wa kujenga kiwanda cha simu za kisasa jijini Mwanza.

Dodoma. Ili kurahisisha upatikanaji na kupunguza bei, Serikali mesema inakamilisha mchakato wa kujenga kiwanda cha simu za kisasa jijini Mwanza.

Mpango huo umebainishwa na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Dk Faustine Ndungulile kwamba ni jitihada za Serikali kupunguza bei ya bidhaa hiyo nchini.

Dk Ndungulile alitoa kauli hiyo alipozungumza na watendaji wakuu pamoja na menejimenti ya wizara yake na wajumbe wa bodi za taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2020 hadi 2025 inayolenga kuongeza wigo wa mawasiliano na matumizi ya mtandao wa intaneti jambo ambalo haliwezi kufanikiwa bila kuwa na simu nafuu za kisasa.

“Wizara tumeshaanza mchakato wa kuweka mazingira wezeshi kwa viwanda vyetu vya ndani. Tunatarajia kujenga kiwanda kimoja kule Mwanza ambacho kitakuwa kinazalisha simu janja,” alisema.

Alitoa wito kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika Tehama kujitokeza kwani Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili kuondoa kero zitakazojitokeza kuweza kutimiza lengo la kuwa na kufanikisha uwekezaji.

Alisema uwekezaji wa kiwanda hicho unalenga kuwawezesha Watanzania kupata simu za kisasa na vifaa vingine vya mawasiliano kwa bei nafuu.

Aidha, Dk Ndungulile ametoa siku 90 kwa TCRA kupeleka mapendekezo yatakayoondoa malalamiko ya wananchi kwenye wizi wa unaofanywa na kampuni za mawasiliano kwenye vifurushi, fedha na bando.

“Kama ilivyo katika umeme ambako hatupati malalamiko, na kwenye mitandao ya simu nako tunataka yasiwepo. Tukimaliza tutakwenda katika vifurushi vya televisheni na vingine,” alisema.

Kuhusu kitengo cha huduma za wateja cha TTCL kutopokea simu za wateja kwa wakati, Dk Ndungulile alisema tatizo hilo ameliona na amelitolea maelekezo kwa mkurugenzi wa shirika kuhakikisha analisimamia kwa karibu.

“Biashara ya kwanza mwananchi anatafuta customer care (huduma kwa wateja) kwa siku mbili hatutaki kuliona,” alisema.

Naye mkurugenzi wa TTCL, Waziri Kindamba alisema kucheleweshwa kwa huduma kwa wateja katika kampuni hiyo kulikojitokeza kwa siku tatu kulisababishwa na shughuli wa uboreshaji wa mifumo.

“Tulitoa notice (taarifa) kwa wateja wetu kuwa wakati tuna upgrade (tunaboresha) inawezekana ikatokea changamoto ya huduma. Lakini, naomba niwahakikishie kwa sasa kama utapiga simu huduma kwa wateja utaona unahudumiwa kwa haraka,” alisema Kindamba.

Alisema maboresho hayo yataenda sambamba na kasi ya mtandao kuliko ilivyokuwa mwanzo hivyo wateja wa mtandao huo wajiandae kupata huduma bora.

Ili kuongeza wigo wa utoaji huduma, alisema wamefungua tovuti na mitandao ya kijamii ambayo watu wengi wanaweza kuitumia kueleza mahitaji yao bila kulazimika kwenda ofisini.

Imeandikwa na Edda Laju, Mwananchi
[email protected]