Kiwango unywaji maziwa kila Mtanzania chafikia lita 67 kwa mwaka
Muktasari:
- Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) inatarajia kugawa zaidi ya lita 200 za maziwa kwa wakazi wa Mwanza ili kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa wananchi.
Mwanza. Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) inatarajia kugawa zaidi ya lita 200 za maziwa kwa wakazi wa jijini Mwanza kuwahamasisha unywaji wa maziwa, huku ikielezwa hali ya unywaji maziwa kwa mwaka jana ikipanda kutoka wastani wa lita 66 kwa Mtanzania mpaka lita 67.2.
Uzinduzi wa wiki ya maziwa kitaifa utazinduliwa Mei 29, 2024 na mkuu huyo wa mkoa katika viwanja vya Furahisha ukiambatana na kongamano la wadau litakalofanyika Mei 30 huku, kilele chake kikitarajiwa kuwa Juni Mosi mwaka huu kitakachohitimishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Mei 27, 2024 Meneja wa Fedha na Utawala TDB, Aggrey Msemwa amesema hiyo ni moja ya mbinu ya kuwahamasisha wananchi kunywa maziwa kuelekea wiki ya unywaji wa maziwa inayofanyika kitaifa Uwanja wa Furahisha mkoani Mwanza kuanzia Mei 28 hadi Juni Mosi 2024.
Amesema licha ya Mkoa wa Mwanza kuwa na wastani wa zaidi ya ng’ombe milioni tatu kati ya milioni 38 waliopo nchi nzima, hali ya unywaji maziwa hairidhishi.
“Tanzania tuna wastani wa ng’ombe milioni 38 na Mwanza pekee ina wastani wa ng’ombe milioni 3 kuendelea, kwa hiyo hali ya unywaji wa maziwa siyo nzuri sana ndiyo maana tukachaguwa kuwa na hili tamasha pamoja na mambo mengine kuja kuhamasisha wananchi kutumia maziwa.
“Kuna maziwa ambayo sisi wenyewe tunanunua kama bodi lakini pia kuna maziwa ambayo huwa tunashirikiana na wadau wengine. Sasa kwa sisi wenyewe huwa mara nyingi tunakuwa tumejiandaa kutoa wastani kuanzia lita 200 kwenda juu,” amesema.
Amesema hali ya uzalishaji maziwa kwa sasa nchini ni wastani wa lita bilioni 3.97 mwaka, katika hayo asilimia tatu ya maziwa ndiyo yanaongezewa thamani huku, hali ya unywaji maziwa kwa mwaka jana ikipanda kutoka wastani wa lita 66 kwa Mtanzania mpaka lita 67.2.
“Takwimu za kimataifa zinasema ili nchi iweze kutambulika kwamba ina utumiaji mzuri wa maziwa atleast (angalau) mtu awe anakunywa wastani wa lita 200 kwa mwaka. Kwa hiyo ukiangalia kwa takwimu hizo Tanzania tupo vizuri sana katika unywaji wa maziwa kwa ujumla,” amesema
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema pamoja na wiki ya maziwa kulenga kuelimisha wananchi na umma juu ya matumizi sahihi ya maziwa, teknolojia mbalimbali, namna bora ya ufugaji wa ng’ombe lakini pia makundi mbalimbali yatagawiwa maziwa wakiwemo watoto wanaoishi kwenye vituo vya kulelewa.
“Siku hiyo tutagawa maziwa kwa makundi mbalimbali hapa Mwanza kwenye hospitali, vituo vya watoto yatima tutakwenda kugawa maziwa bure kabisa watu wanywe maziwa wahamasike,” amesema Mtanda.
Amesema katika wiki hiyo yenye kauli mbiu ya ‘Kunywa maziwa salama kwa afya bora na uchumi endelevu’ fursa zilizopo kwenye tasnia ya maziwa zitatangazwa na wadau kukutanishwa.
“Hata watunga sera wetu na wenyewe watakuwepo ili kuweza kutunga sera bora, nzuri ni lazima wakutane na wadau kuelewa vizuri tasnia ya mzaiwa na wanapotunga sera za nchi basi ziweze kuwa na tija kwa wadau wa tasnia ya maziwa,” amesema.