Kizimbani wakidaiwa kukutwa na kilo 13 za heroin

Wednesday April 14 2021
KIZIMBANI pc
By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Mfanyabiashara mkazi wa Morogoro, Hamis Awadhi (44) na mwenzake Maria Mtumbuka (29) wamefikisha katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha heroin kilo 13.4.

Wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Aprili 14, 2021 na kusomewa mashtaka yao kwa mahakimu wawili tofauti.

Katika kesi ya kwanza, Awadhi amesomewa shtaka lake na wakili wa Serikali,  Ester Martin mbele ya hakimu mkazi mwandamizi,  Kassian Matembele kwamba mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 31/2021.

Hata hivyo, kabla ya kusomewa kwa mashtaka yao, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Martin amedai Aprili 2, 2021 katika Uwanja wa Ndege  wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Awadhi anadaiwa kusafirisha kilo 6.75 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka linalomkabili, hakutakiwa kujibu chochote na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Advertisement

Hakimu Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 27, 2021 itakapotajwa tena.

Katika kesi ya pili, Mtumbuka ambaye ni mkazi wa Ilala,  amesomewa shtaka lake na wakili wa Serikali,  Faraji Ngukah mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Yusto Ruboroga.

Ngukah amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 32/2021

Akimsomea hati ya mashtaka, Ngukah amedai April 2, 2021 JNIA, Mtumbuka anadaiwa kusafirisha kilo 6.65 za heroin kinyume cha sheria.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kesi hiyo kuahirishwa hadi Aprili 28, 2021 itakapotajwa tena.

Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya za Sh10 milioni kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Aprili  2, 2021 saa 1:50 usiku katika uwanja huo eneo la ukaguzi wa mizigo ya abiria  Jeshi la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege liliwakamata washtakiwa hao wakiwa na kiasi hicho cha dawa wakisafirisha kutoka Harare, Zimbabwe kwenda Bombay, India.

Advertisement