Kodi ya kanisa yamzuia kumzika mkewe kidini

Kodi ya kanisa yamzuia kumzika mkewe kidini

Muktasari:

  • Mtumishi wa umma nchini Nigeria, Uche Muodili amesema ameshindwa kumzika mkewe kwa mazishi ya Kikristo kutokana na gharama kubwa alizotozwa na kanisa.


Enugu. Mtumishi wa umma nchini Nigeria, Uche Muodili amesema ameshindwa kumzika mkewe kwa mazishi ya Kikristo kutokana na gharama kubwa alizotozwa na kanisa.

Akizungumza kwenye mahojiano na BBC, Muodili alisema kanisa lilikataa kumzika mkewe ambaye naye alikuwa mtumishi wa umma, kwa kushindwa kumudu gharama.

Muodili ambaye anatoka jamii ya Igbo, mashariki mwa Nigeria alisema kwenye mahojiano hayo kuwa kanisa lilimtaka alipe kiasi cha fedha za Nigeria, naira 100,000 (sawa na dola za Marekani 250, kiasi ambacho hakuwa nacho.

Alisema baada ya kushindwa kumudu kiasi hicho cha fedha, aliamua kumzika mkewe kwa mila na desturi za kwao.

Hata hivyo, Askofu wa Dayosisi ya Enugu wa Kanisa la Anglikana, Chukwuma Emmanuel, alizungumzia umuhimu wa kanisa wa kuwazika waumini wake bila kuhoji wafiwa kama marehemu alikuwa akichangia kanisa alipokuwa hai.

Alisisitiza kuwa fedha haziwezi kumpeleka mtu yeyote mbinguni na kwamba ni jukumu la kanisa kumzika muumini wake aliyebatizwa hapo hata kama anadaiwa au hadaiwi.

Chukwuma alisema uongozi wa Kanisa la Anglikana katika kanda yake utaendelea kuhubiri dhidi ya wanaotoza kodi familia zilizofiwa.

Pia, aliwataka wale wanaojiandalia mazishi ya kifahari, ikiwamo bendi za muziki, kutumia fedha hizo kwa maendeleo ya jamii na kuwasaidia maskini.

“Hatuwezi kuacha kuwazika waumini wetu kwa sababu familia wamekosa fedha za kodi. Tutahakikisha tunaliondoa hili,” alisema.

Kiongozi wa kimila, Martha Dunkwu alisema amekutana na viongozi wengine wa kimila kuangalia namna ya kupunguza kodi na gharama nyingine za mazishi.

Aliwatuhumu wanawake kwa kuwa tatizo kuu katika suala la mazishi kwa njia zote mbili za kimila na kanisani.

Dunkwu alisema wanawake ambao ni matajiri ndio wanaowalazimisha maskini kulipa kodi ya mazishi.

Aliwataka Wakristo kuelekeza imani zao kwa Mungu na siyo kuwa chini ya makundi ya kanisani.

Mchungaji John Chinenye alisema makanisa hayafanani na kwamba yeye kanisa lake haliwalazimishi wafiwa kulipa kodi kabla ya mazishi kama yanavyofanya makanisa mengine.

Alisema kodi hiyo siyo kitu kizuri na inatakiwa kusimamishwa. “Sisi haipo na tutaendelea kuhubiri isiwepo. Lazima tuwafunze waumini kuwekeza kwenye imani wanapokuwa hai na siyo kulipa kodi wanapokufa,” alisema.

“Kodi kubwa wakati wa mazishi inatozwa na waumini na siyo padri. Waumini wa kanisa wanasisitiza kukusanya kodi hata pale padri anapokataza. Tatizo linaanzia kwa waumini na linaweza kuisha kama watakubali,” alisema.

Mfanyabiashara, Kosiso Christiana aliwaomba viongozi wa makanisa na mila kupambana na kodi ya mazishi, hali inayowafanya wafiwa kukopa ili kununua vitu mbalimbali, wakiwemo wanyama kwa ajili ya kuwazika wapendwa wao.

“Kanisa halifanyi sahihi kukusanya kodi ya waliokufa kutoka kwa familia kabla ya kuzika. Kanisa liache kukusanya kodi ya waliokufa ili kuwarahisishia wale maskini wazike wapendwa wao,” alisema Christiana.

Ulitolewa mfano wa Gregory Nnaka, aliyekuwa akiishi jimbo la Anambra na alikuwa muumini wa Kanisa Katoliki, lakini aliondoka huko na kwenda kuishi Lagos kwa miaka mingi.

Alipofariki dunia viongozi wa kanisa hilo kwenye jimbo lake walikataa kumzika kwa kuwa alikuwa na madeni ya maelfu ya naira, fedha ambazo familia yake ilishindwa kulipa.

Hata hivyo, kaka wa marehemu, Chifu Innocent Nnaka alisema walilazimika kukodi Mchungaji wa Pentekoste kumzika ndugu yao kwenye mazishi ambayo familia yote ni Wakatoliki na kwamba hali hiyo iliharibu uhusiano wao na viongozi wa kanisa kwa kuwa marehemu alibatizwa hapo na alikuwa akihudhuria kanisani.