KONA YA WASTAAFU: Baada ya utumishi uliotukuka usiokuwa na utukutu...!

KONA YA WASTAAFU: Baada ya utumishi uliotukuka usiokuwa na utukutu...!

Muktasari:

  • Naam, sasa mhenga wetu ni mstaafu. Baada ya miaka 40 ya ratiba ya kutoka nyumbani saa 12:30 alfajiri na kurejea Saa 1:00 usiku, siku tano za wiki na miezi 11 ya mwaka, mwezi wa 12 ukiwa ni ule wa likizo, ghafla mzee wetu anajikuta huru bin free asiyekuwa na ulazima wa kujua muda, siku wala mwezi aliomo, zaidi ya kujua tu asubuhi, mchana, jioni na usiku, basi.

Naam, sasa mhenga wetu ni mstaafu. Baada ya miaka 40 ya ratiba ya kutoka nyumbani saa 12:30 alfajiri na kurejea Saa 1:00 usiku, siku tano za wiki na miezi 11 ya mwaka, mwezi wa 12 ukiwa ni ule wa likizo, ghafla mzee wetu anajikuta huru bin free asiyekuwa na ulazima wa kujua muda, siku wala mwezi aliomo, zaidi ya kujua tu asubuhi, mchana, jioni na usiku, basi.

Katika umri wake mpevu wa kasoro miaka minane kufikia ule umri tuliopewa na Mungu wetu mwema kwa mujibu wa vitabu vitakatifu, mzee wetu mstaafu anajikuta akianza maisha mapya ambayo anaamini alipaswa kuyaishi, lakini akayaweka pending kwanza ili kuishi haya ya miaka 40 ya kumtumikia kafiri ili apate mradi wake kwenye maeneo mbalimbali.

Katika ustaafu wake huu, anajikuta akifanya mambo ambayo huko nyuma alilazimika kuyafanya kama hobby siku za mwishoni mwa wiki na siku za sikukuu asizokwenda kibaruani, ambayo sasa ndio yamekuwa ajira yake kamili isiyokuwa na mshahara wala kuhitaji kusimamiwa na mtu.

Ustaafu wa mzee wetu unamuwezesha hata kufuatilia afya za kuku wawili watatu wa kienyeji wanaomilikiwa na familia waliopo kwenya kakibanda huko uani ambao wakisalimika Sikukuu za Pasaka, Iddi ama Krisimasi basi hawafi tena!!

Mstaafu wetu sasa anahudhuria misiba ya sio tu ndugu wa karibu na wa mbali, bali pia hata wa majirani walio mtaa wa saba na wa 17, ili mradi yeye na huyo jirani wamejenga kile dot.com wetu wanachosema ni ‘kupeana tano’. Enzi zake za miaka 40 ya kuwa kibarua, ajira ya mstaafu wetu ilikuwa sababu tosha ya kutohudhuria misiba ya namna hiyo kwa kisingizio cha kukosa nafasi kutokana na kazi!

Mzee wetu anajikuta sio ana nafasi ya kumwaga ya kuhudhuria misiba, bali hata pale msiba huo unapotokea jijini unaopaswa marehemu akazikwe kijijini, sasa anakuwa mstari wa mbele kuwahi kiti kwenye lile gari la wale watakaomsafirisha marehemu!

Anaharakisha kukiri hapa kwamba hili mara nyingi hutegemea hali na wakati kapensheni kake kalivyokaa. Naam, Kapensheni kake haka ambako hawa dotcom wetu wa nyakati hizi wamekata hadhi au kukaita ‘Laki si Pesa’ ingawaje kakikaa mfukoni kanampa amani ya moyo japo kwa siku mbili tatu.

Ni nyakati hizi hizi kwa mshtuko mkubwa mzee wetu anagundua kuwa ‘Team Mstaafu’ wake wanne wanaokamilisha mchango wake katika jukumu jema la kuijaza dunia, wameshamzidi urefu na upana wa kifua na hata anaporudi nyumbani jioni baada ya matembezi ya kunyoosha miguu na mwili akiwasikia wanaongea na mama yao inabidi asimame mbali kidogo ili kuhakikisha kwamba bezi anazosikia ni za wanawe na sio za ‘Mgeni njoo Mwenyeji Aumie’.

Sawa, mstaafu wetu anakiri si mrefu kiasi hicho ingawaje pia si Andunje, lakini mara kadhaa kwenye mikusanyiko ya ndugu amekuwa akisikia midomo ikitereza na kutamka kuwa ‘Team Mstaafu’ watatu wa kiume ‘Wamepanda juu hadi kumpita baba yao’ na ni watu wa ‘miraba minne’ tofauti na baba yao aliyekuwa wa miraba miwili enzi zake za miaka 40 ya ajira!

Alichogundua mapema mzee wetu mstaafu ni kuwa ameondokana na ratiba ngumu ya kukurupuka asubuhi kuwahi kibaruani, lakini akagundua mapema pia alikuwa anavuruga ratiba za raia wengine.

Chukulia huyu ‘Makamu wa Raisi’ wa moyo wa mstaafu wetu ambaye ameshirikiana naye katika jukumu la kuijaza dunia kwa mara nne. Watoto wakaanza shule na kumfanya kiumbe huyu mara nyingi kuwa yuko pekee nyumbani hadi pale watoto waliporudi shule. Upweke huu ukamfanya kuzoea kuwa huru bin free kufanya kila alichotaka kwa nafasi na wakati aliotaka mwenyewe.

Kufumba na kufumbua kiumbe huru akajikuta hata akiamka asubuhi kuwasha jiko la mkaa ili apike chai, mstaafu wake alijipa cheo cha kufuatilia na kuhoji kila anachofanya Mamaa kwa staili ya alichokuwa anafanyiwa yeye na mkuu wake wa Idara huko ofisini! Ndio, akawa kama amestaafu na kuyabeba ya ofisini na kuja nayo nyumbani!

Mstaafu akajipachika ratiba ya hata kumfuata mwenza eneo lake la kujidai la jikoni na hata kabla moto wa mkaa aliowasha haujakolea anatoa ushauri feki, ‘huo mkaa mbona hauwaki haraka? Inawezekana ni mbichi labda ubadilishe mwingine’. Ni baadaye ndipo mstaafu wetu akaanza kuhisi labda kuna wakati wa moyo wa kiumbe ulikuwa hauishii kwenye kuguna tu, bali kimoyomoyo alikuwa akichomekea kujibu ‘Ntolee hapa wee Mzee! Uliishaona mkaa unawaka baada ya dakika mbili tu?’

Kufumba na kufumbua, kiumbe huru huyu aliyekuwa amejizoelea kunywa chai hata saa tano ama sita mchana baada ya kuwa ameishafanya usafi wa nyumba yake, ama kuangalia marudio ya tamthilia aipendayo, sasa akajikuta akihimizwa na mstaafu wake aamke mapema kupika chai wanywe kwanza ndipo shughuli za usafi wa nyumba na kuangalia tamthilia ziendelee!

Mzee wetu akafikia kuhisi kuwa nyimbo za taarabu zilizokuwa zikishamiri kila pale alipotoa ushauri fulani wa kuijenga nchi njema hii ya ‘Jamhuri ya Watu wa Mstaafu’, ulikuwepo uwezekano mkubwa kwamba katika muda mfupi ujao haitakuwa ajabu kuambiwa: ‘Baba Mwanagutu, unaonaje wewe ukinisaidia kukwangua hilo sufuria hapo wakati mimi ninapiga deki hapa!’

Hakika ungekuwa ushahidi kamili kwamba mzee kweli alikuwa amestaafu na sasa hana ajira na anai miss kweli! Neno la Kiingereza kuweka msisitizo!

Mstaafu wetu anasema anajiuliza kwa nini isiwe hivyo wakati ajira yake mpya aliyojiajiri alidhani inamruhusu kumpa ushauri wa alichoamini kwamba ni bonge la ushauri kumbe kwa ‘Makamu wa Rais’ wake huyu wa moyo wake ulikuwa si zaidi ya utumbo wa bata usiokuwa na faida yoyote kwa yeyote labda kwa mlevi wa mataputapu wa Uwanja wa Fisi tu!

Tukutane Ijumaa ijayo.

0754 340606 / 0784 340606