Kongamano la wanawake na teknolojia kufanyika nchini

Muktasari:

  • Kongamano la kwanza la wanawake na teknolojia kufanyika nchini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe ya Siku ya Wanawake ambayo huadhimishwa Machi 8 duniani kote.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kwanza la wanawake na teknolojia litakalofanyika nchini Machi 7 jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo linalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika teknolojia kutokana na ukweli kwamba maendeleo hayawezi kutenganishwa na teknolojia.
Akizungumza leo Februari 2, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Lunchpad ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo, Caro Ndossi amesema wanalenga kuwaleta pamoja wataalamu wa sekta mbalimbali ili kujadili maendeleo ya teknolojia na athari zake kwa wanawake.
“Kwa kasi ya maendeleo ya kiteknolojia, ni muhimu kwamba wanawake wapewe fursa sawa za kuchangia na kuunda mustakabali wa teknolojia. Hivyo basi mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo hatua muhimu kwa wanawake na teknolojia, ukuaji wa teknolojia kama fursa kwa wanawake, teknolojia na ubunifu wa kujumuisha na usawa wa kijinsia,”amesema.
Amesema imani ya shirika hilo ni kwamba ushirikishwaji wa wanawake katika teknolojia ni muhimu kwasababu wanawake huleta mtazamo wa kipekee kwenye meza kuu za majadiliano.

Pamoja na mijadala, Caro ameeleza kuwa kongamano hilo litatoa fursa kwa wanawake kuonyesha kazi zao, kubadilishana uzoefu wao na kuungana na wengine katika masuala ya teknolojia.
“Tutaandaa maonyesho ya bidhaa za kidijitali ziilizoundwa kwa ajili ya wanawake na zile zilizobuniwa na wanawake pamoja na programu tofauti, tafiti za kifani kuhusu athari za teknolojia kwa wanawake nchinii,”amesema Caro.
Kwa upande wake Faith Manangwa aliyewakilisha Buni Hub kitengo kilichopo chini ya Tume ya Sayansi Tanzani (Costech) amesema kongamano hilo litakwenda kuibua mjadala mpya wa ushiriki wa wanawake kwenye teknolojia.
“Tunaamini hii ni fursa ya aina yake kuwaleta pamoja wataalamu wa teknolojia kuzungumza kuhusu wanawake na wasichana katika eneo hilo. Imani yangu ni kwamba kupitia jukwaa hili tutaongeza hamasa kwa wanawake na wasichana kuona na kuchangamkia fursa zilizopo kwenye tasnia hii,” amesema Faith.