Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kova atoa 'drones' kuchunguza masalia ya moto mlima Kilimanjaro

Muktasari:

  • Wakati moto ukiendelea kudhibitiwa katika mlima Kilimanjaro, Kamishna mstaafu wa Jeshi la polisi nchini, Suleiman Kova ametoa "drons" mbili kwa serikali kwa ajili ya kusaidia kuchunguza masalia ya mienendo ya moto katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA).

Moshi. Wakati moto ukiendelea kudhibitiwa katika mlima Kilimanjaro, Kamishna mstaafu wa Jeshi la polisi nchini, Suleiman Kova ametoa "drones" mbili kwa serikali kwa ajili ya kusaidia kuchunguza masalia ya mienendo ya moto katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA).
Moto huo ulitokea Oktoba 21 saa 2:30 usiku  katika eneo la Karanga kueleka Baranco mita 3,963 kutoka usawa wa bahari ambapo vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama nchini vilipelekwa katika mlima Kilimanjaro kukabiliana na moto huo.
Jana Novemba 3, 2022 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa bungeni akijibu maswali ya papo kwa papo alisema moto huo haujasababisha madhara ya kibinadamu na kwamba madhara yaliyojitokeza  ni kusababisha hasara, hofu na kilomita za mraba  33 za uoto wa asili zimeteketea kwa moto.
Vifaa hivyo pamoja na misaada mingine ya chakula na blanketi kutoka nchini China kwa kushirikiana na  Shirika la Sukos Kova linalojihusisha na maafa, majanga na hifadhi vimekabidhiwa leo Novemba 4 kwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ili kuendelea kusaidia  kuchunguza majanga mbalimbali yakiwemo  ya moto.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Babu amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wamefanikiwa kupambana na kuuzima moto huo na kwamba yaliyobaki ni masalia ya magogo ambayo vijana wanapambana kuyazima.
"Tumefanya jitihada kubwa sana tangu siku ya kwanza vijana wetu wamefanya kazi kubwa kupambana na kuuzima moto katika mlima wetu wa Kilimanjaro lakini viongozi mbalimbali wa serikali nao wamepambana na kuhakikisha moto unazima katika mlima Kilimanjaro,"
Babu amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuja mkoani humo  kesho kutwa  na kuangalia ni kwa kiasi gani moto huo umedhibitiwa na kwamba mpaka sasa moto umezima katika mlima Kilimanjaro kutokana na jitihada kubwa zinazoendelea.

"Kwa sasa moto katika mlima wetu umekwisha na kesho kutwa Waziri mkuu atakuja kuangalia ni wapi tumefikia lakini kwa sasa katika mlima wetu moto umekwisha yamebaki magogo ambayo yanawaka na kutoa moshi lakini vijana bado wapo wanapambana kuyazima,"
"Tunamshukuru mzee wetu Kamishna mstaafu Suleiman Kova kwa kuja kutushika mkono  kwa kutupatia vifaa hivi,  najua wewe ni mzalendo ambaye umetumikia nchi hii kwa muda mrefu sana,"amesema RC Babu
Mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo kwa mkuu huyo wa mkoa, Kamishna Kova amesema yeye kwa kushirikiana na wadau kutoka nchini China wameona ni jambo la kizalendo kuisaidia serikali kwa kuipatia vifaa hivyo ili viweze kuchunguza mienendo ya moto katika mlima Kilimanjaro.
"Baada ya kutokea janga la moto mlima Kilimanjaro na sisi tukasema tufanye haraka kuja na vifaa ambavyo ni vya kisasa ambavyo vinaweza vikaenda juu ya mlima na sehemu yoyote ambayo kuna janga hiki chombo kinaweza kwenda mbali na kuchunguza ni nini kimetokea, sababu ni nini kukawa na uharaka wa kufanya operesheni ya kwenda kuzima moto au kama kuna tatizo jingine,"
"Tunatoa wito kwa wenzetu wengine kwamba kukitokea janga kama hili wasifikiri ni serikali peke yake serikali inahitaji kupata msaada  kutoka kwa wadau mbalimbali kwasababu mlima Kilimanjaro ni sura ya dunia,"anesema Kova

Andrew Huang, kutoka nchini China amesema kwa kuwa  serikali ya Tanzania ina uhusiano mzuri na nchi hiyo wako bega kwa bega kuhakikisha  wanashirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo kutoa msaada pale ambapo unahitajika kwa haraka.
"Tunataka kuona mlima huu wa Kilimanjaro ukiendelea kuwa mzuri na mazingira yake  mazuri kwa ajili ya kuliwakilisha Taifa la Tanzania ndio maana tumekuja hapa kwa kushirikiana na Shirika la Sukos Kova kutoa misaada mbalimbali,"