Kubwata bila data si ni kudata kabisa?

Muktasari:

  • Unajua Makengeza, hapo zamani za kijikale, katika kukumbuka miaka kumi ya Mkataba wa Haki za Watoto, waheshimiwa wetu wa sponji wa mji unaodidimia waliamua kuwa na kikao maalumu kuhusu hali ya watoto nchini kwetu.

Unajua Makengeza, hapo zamani za kijikale, katika kukumbuka miaka kumi ya Mkataba wa Haki za Watoto, waheshimiwa wetu wa sponji wa mji unaodidimia waliamua kuwa na kikao maalumu kuhusu hali ya watoto nchini kwetu.

Nilikuwepo kama mtazamaji na nilishangaa. Wataalamu walieleza masuala mengi sana inayohusu watoto na kutoa takwimu za kutisha likiwemo suala la utapiamlo na kudumaa kwa watoto (hadi leo katika mikoa mingine zaidi ya nusu ya watoto wetu wamedumaa kimwili ambayo huathiri pia kudumaa kwao kiakili), hali ya elimu na vilevile janga la Ukimwi kwa vijana.

Katika kuongelea janga la Ukimwi, wataalamu wale na mawaziri husika walisisitiza hali halisi ya mazingira inayowafanya vijana wawe hatarini kuambukizwa VVU na walitoa mapendekezo jinsi ya kupambana na hali halisi hiyo.

Makusudi, hawakuongelea kondomu bali umuhimu wa kuangalia mazingira hatarishi yanayowapelekea vijana kuwa hatarini. Ili kuwa na mabadiliko ya tabia, lazima pawepo na mabadiliko ya mazingira. Kwa hiyo, walitaka waheshimiwa watafakari upya badala ya hubiri zilezile za kila siku.

Baada ya kutolewa kwa maelezo yote haya, waheshimiwa wale wa sponji walipewa nafasi ya kutoa maoni yao. Muda ulikuwa mfupi maana enzi zile, waheshimiwa waliangalia urefu wa bahasha na ufupi wa kikao. Bila shaka siku hizi wamebadilika!!. Basi kutokana na ufupi huo, ni waheshimiwa sita tu waliopata nafasi ya kuongea. Katika wale sita, wanne hawakutaka kabisa kuzingatia walichoambiwa na wataalamu, bali walitumia kale kanafasi kaduchu kao kulaani kondomu tu.

Yaani, wakati wataalamu wametoa taswira pana ya maisha ya watoto na vijana, waheshimiwa wa sponji waliweza kuona kakitu kadogo tu nje ya somo lote walilopewa.

Nikabaki najiuliza, kuna faida gani kuwa na waheshimiwa ambao wako tayari kubwata bila data. Kubwata bila data si kudata kabisa? Ndiyo maana wahenga wamesema, bila kutafiti, au kuelewa utafiti wa watu wengine, chunga mdomo, badala ya kuchonga.

Ndipo hapo, nikaanza kutafakari kuna uhusiano gani kati ya utaalamu na siasa. Si kwamba wanasiasa hawana utaalamu. Wana utaalamu sana kuchonga maneno na hata kupinda maneno hadi kupinda hata mwelekeo wa suala hili au lile au hata mwelekeo wa nchi.

Wana utaalamu sana kutumia maneno kuwafunika macho watu kwa namna ambayo wanakuwa vipofu kwa mambo mengine. Na kwenye jamii ambamo siasa ya chama fulani ni mfalme, wageni rasmi ni wanasiasa, habari ni za siasa, kila kitu kinapimwa kisiasa na sote tunatakiwa kuinama mbele ya wanasiasa wa chama kile, maneno yao ni dhahabu na maneno ya wengine, iwapo si ya kusifia na kutukuza, hayana maana. Badala yake huhesabiwa kuwa ni uchochezi.

Sasa, katika hali hii, nilitegemea kwamba ili wahalalishe ufalme wao hawa waheshimiwa wenye utaalamu wa maneno watatafuta kuelewa kila suala kwa undani kabla ya kuanza kuliongelea maana ukibwata bila data, ni rahisi kupotosha hivyo kurudisha nyuma elimu, amani na maendeleo ya nchi.

Nikaanza kuiuliza hivi waheshimiwa hawa wa sponji wanasoma vitu gani kila mwaka. Si ingekuwa vizuri kuwatakia kutaja si mali yao tu, wala elimu yao tu (maana najua utaalam wa kuchonga hauendani na elimu tu) Wataje vitabu walivyovisoma, makala, pepa, makabrasha waliyosoma katika kujiandaa kujadili na kufanyia maamuzi masuala muhimu wa taifa letu.

Naam. Wako mtandaoni muda wote. Sasa, pamoja na wasapu, na kutwiti na kuinstagrami, wanatumia mtandao mara ngapi kwa siku kutafuta habari zaidi au uchambuzi muhimu juu ya suala hili au lile?

Kwa mfano, wapo kuna muswada unaohusu mitaala ya elimu, wangapi wanasoma juu ya mitaala sehemu nyingine na faida na hasara ya kila mitaala? Ni muhimu kuuliza maana maamuzi yao yanatuathiri sote.

Wamenunua na kusoma vitabu vingapi na mapochopocho yao ya vikao na kadhalika? Najua wako wanaosoma na inaonekana wazi katika hotuba zao kwamba wamesoma na kuchambua. Wametumia akili kabla ya kutumia mdomo. Na wapo wanaoheshimu wataalam na utaalam wao, wanatafuta ushauri wa wataalam kabla ya kusema, lakini wote wanafanya hivyo?

Ndipo hapo ninapata shida nyingine makengeza. Zamani, nchi yetu ilikuwa na itikadi. Si lazima watu walikubaliana juu ya itikadi hii na si kweli kwamba kila mara maoni ya waliotofautiana na itikadi ile walipata nafasi ya kujieleza.

Upinzani ulikuwepo hata ndani ya mfumo wa chama kilekile na wataalamu na wasomi walitoa changamoto nyingi hadi kuwaka moto. Angalau tulijadiliana na kutofautiana juu ya masuala.

Tofauti na siku hizi. Siku hizi tuna iti-kada badala ya itikadi. La muhimu kuwa kada wa chama, na waweza kubadilisha ukada kama vila mtindo wa nywele tu maana ukada hauna itikadi.

Najua wewe Makengeza umesema siku nyingi aheri makengeza kuliko chongo maana uko huru hata kama macho ni mabovu. Angalau una uhuru wa kutafakari mwenyewe bila kulazimishwa tafakari za mtu mwingine.

Huna chongo kwa sababu hulazimishwi kufuata sera zote za chama fulani na kupigia makofi matamko na vitendo vyote vya viongozi wake hata kama hukubaliani nacho. Chongo huchonga akili hadi mtu huchonga hovyohovyo.

Lakini siku hizi kuna wataalam pia ambao wameamua kuwa wanasiasa, Nilitegemea kwamba utaalamu utaheshimiwa zaidi kuliko zamani. Kumbe iti-kada ni suala lingine kabisa hadi unawaona wengi wanaoingia siasa wanatelekeza utaalamu katika kutekeleza siasa.

Najiuliza hawa watu wanapikwa katika tanuru ya namna gani hadi wanabadilika hadharani bila hata kuona aibu. Oh, sikatai kwamba watu wanabadili mawazo, wanabadili msimamo, ni haki yao, na ni sehemu ya kuendelea kama binadamu kujikosoa, kutambua udhaifu na kuurekebisha. Lakini tanuru hii tunayoiona ni zaidi ya hapo. Mtu anakana kabisa mambo yote ya huko nyuma.

Si hivyo tu, wanakana pia hata weledi wao. Utakuta mwanasheria anapingana na sheria zilezile alizothamini jana, au kutoa hoja hafifu hadi wanasheria wenzake wanapigwa butwaa.

Aliyekuwa mwanaharakati ya haki atajikuta amekatika kabisa na harakati zake hadi kulaani hata dhana ya uanaharakati. Mtu wa afya … aaah bora nisiseme maana mkengeuko huo … Ni tanuru ya namna gani inayoleta giza badala ya nuru? Au tuite tanuru hii tagiza maana nuru haipo?

Nimeona Makengeza, nimeshuhudia. Nimewaona watu ambao nawafahamu vizuri sana, nimefurahia kuchambua masuala pamoja nao miaka mingi lakini wakishapita kwenye tanuru, huwezi kujadiliana nao tena. Au ni kwa sababu vyama ni kama ukumbi usio na madirisha ili watu wasiweze kuona nje.

Ndiyo maana ninaogopa siku hizi. Naona watu waliopikwa katika tanuru au tagiza za vyama vyao wanataka kila mtu apikwe vilevile, achonge na chongo la chama ili wachonge kinavyotakiwa. Na katika hali hii, taaluma, usomi, uelewa mpana wa masuala fulanifulani vinatupwa nje, na mtafiti huonekana kama msaliti.

Katika hali hii tufanyeje? Ama wenye iti-kada wakubali kutumia na kuendeleza utaalam wao katika kuchonga au hao iti-kada wakubali kusikiliza na kuthamini wataalam wenye mawazo mbadala. Kwa njia hiyo, ninao uhakika haya maendeleo tunayoyataka yatapatikana kwa kina na kasi zaidi.

Imeandikwa na Richard Mabala Makengeza