Kufeli uwakili kilio Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Kama ulidhani kilio cha kufeli vibaya wanafunzi wa wanaotaka kuwa mawakili katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) kipo Tanzania pekee, umekosea

Dar es Salaam. Kama ulidhani kilio cha kufeli vibaya wanafunzi wa wanaotaka kuwa mawakili katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) kipo Tanzania pekee, umekosea.

Ukweli ni kwamba kilio kama hicho kilichozua mjadala nchini hadi zikaundwa kamati mbili kuchunguza, pia kipo katika baadhi ya nchi za Afrika, zikiwemo za Afrika Mashariki, hali inayothibitisha ugumu wa kupata uwakili.

Ili kuwa wakili Tanzania, mbali na shahada utakayoipata katika chuo kikuu, inakupasa kwenda LST kusomea uwakili mwaka mmoja kwa vitendo.

Utaratibu kama huo upo pia kwenye nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Kenya, Uganda na Zambia ambako kote kumekuwa na njia nyembamba ya kufaulu mitihani hiyo na kuibua kilio kama kilichotokea hapa nchini.

Hali hiyo imebainika wakati hapa nchini, matokeo ya mtihani wa uwakili ya mwaka huu yaliyotangazwa na LST yameonyesha wanafunzi 26 pekee kati ya 633 ndio waliofaulu awamu ya kwanza.

Kati yao 265 wamefeli kabisa (discontinue) na 484 wametakiwa kurudia baadhi ya mitihani.

Kutokana na matokeo hayo, mzigo wa lawama vimebebeshwa vyuo vikuu vikidaiwa kutowaandaa vema wanafunzi katika masomo ya shahada kama alivyoeleza Naibu Mkuu wa LST, Profesa Zakayo Lukumay kuwa wanapelekewa “chakula kisichoiva”.

Hatua hiyo ambayo imekanushwa na baadhi ya vyuo hivyo vikirusha mpira kwa LST na kuomba ufanyike uchunguzi, imeiibua Serikali na kuamua kuunda kamati ya watu saba kuchunguza mzizi wa tatizo, ikiongozwa na Dk Harrison Mwakyembe.

Aidha, majaji wastaafu nao wameunda kamati itakayoongozwa na Dk Fauz Twaib kufuatilia malalamiko hayo ikiangazia undani wa hali ya mafunzo ya uanasheria katika vyuo vikuu, mitalaa, mifumo ya ufundishaji, namna gani Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) inasimamia ubora wa ufundishaji katika vyuo vikuu pamoja na njia za ufundishaji.


Si Tanzania pekee

Mjadala kuhusu mitihani hiyo na mfumo wake umeibua taarifa mpya kutoka nje ya nchi, zikibainisha kuwa kilio hicho hakipo tu hapa nchini.

Taarifa ambazo Mwananchi imezipata, zinaonyesha janga kama hilo limeikumba sekta ya sheria Zambia katika mtihani wa uwakili mwaka jana, ambapo mwanafunzi mmoja ndiye aliyefaulu kati ya 395.

Kulingana na maelezo ya Chama cha Wanasheria nchini Zambia (LAZ), anguko kubwa la wanafunzi katika mtihani huo limetokana na umakini wa taasisi inayosimamia kuandaa mawakili mahiri.

Kenya nako, mwaka 2020, Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, Kihara Kariuki alilazimika kutoa tamko baada ya asilimia 80 ya wanafunzi wa mtihani wa uwakili kufeli.

Katika tamko lake hilo, Kariuki alilinyooshea kidole Baraza la Elimu ya Sheria (CLE) akilituhumu kutunga maswali kinyume na kile walichofundishwa wanafunzi wa taasisi hiyo.

“Kuna haja ya kuoanisha kazi za KSL na CLE… Hii inatokana na kwamba wanafunzi wametahiniwa kwa mambo ambayo hawakufundishwa,” alisema.

Nchini Kenya, baada ya kusomea uwakili katika Shule ya sheria ya taifa hilo (KLS), mtihani kuhusu kilichofundishwa unatungwa na Baraza la Elimu ya Sheria (CLE).

Matokeo hayo yalisababisha Serikali ya nchi hiyo kuunda kamati ya uchunguzi wa kiini cha tatizo na kile kilichoelezwa na Kariuki.

Baada ya uchunguzi, ripoti iliyotolewa ilibainisha kuwa idadi kubwa ya vyuo havikidhi mahitaji ya kitaaluma, ikiwemo rasilimali watu, nyenzo za kusomea na miundombinu.

“Baadhi ya vyuo vya sheria havina hata maktaba au nafasi ya kufanyia kazi,” ilieleza ripoti hiyo.

Kulingana na ripoti hiyo, kilichojibiwa na wanafunzi katika mtihani wa uwakili ni mithili ya watu wasiowahi kwenda katika darasa la sheria.

“Ni wazi, mafunzo yanaakisi ubora wa huduma za kisheria zinazotolewa na wanafunzi hawa sokoni,” ilieleza ripoti hiyo.

Hata hivyo ilipendekeza kufutwa kwa mitihani ya kuhojiwa (oral examination) na kazi miradi na kuunganishwa katika mbinu za mafunzo ya kozi nzima.

Mapendekezo mengine ni kubadilishwa kwa muundo wa mtihani na kuwekwa muda mrefu zaidi wa mwanafunzi kurudia mitihani, tofauti na ilivyokuwa wakati huo ambapo walirudia kwa miaka mitano pekee.

Vilevile ilibainika wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu vya umma ndio walioongoza kufeli katika mtihani wa uwakili ikilinganishwa na wale wanaosoma katika vyuo binafsi.

Ripoti ilionyesha kwa mwaka 2016 Chuo Kikuu cha Kenyatta kilikuwa kinaongoza katika hilo ambapo asilimia 30 ya wanafunzi waliofeli walisoma shahada zao chuoni hapo.

Chuo Kikuu cha Moi kilishika nafasi ya pili, ambapo asilimia 22 ya waliofeli walisoma shahada katika chuo hicho na Chuo Kikuu cha Nairobi kikiwa cha tatu baada ya asilimia 20 ya wahitimu wake kufeli.

Kwa ujumla asilimia 79 ya wanafunzi waliofeli mtihani wa uwakili KLS nchini Kenya kwa miaka minane nyuma hadi 2016 walikuwa wametoka katika taasisi za elimu ya juu za umma.


Uganda nako shida

Kadhalika, taaluma ya uwakili ni mfupa mgumu nchini Uganda ambako kulingana na matokeo ya mwaka 2019/20, kati ya wanafunzi 1,474 waliofanya mtihani huo 145 sawa na asilimia tisa walifaulu.

Katika orodha hiyo wanafunzi 1,329 waliangukia pua, hali hiyo vilevile iliibua haja ya kufanyika uchunguzi.

Haja hiyo iliibuliwa na Wakili Richard Anguria alipohojiwa na vyombo vya habari, akisema hakuna kinachohalalisha matokeo hayo, hoja ambayo iliungwa mkono na Wakili wa Haki za Binadamu, Nicolas Opiyo.


Tatizo muda

Ukiacha kilio mitihani ya mawakili katika nchi hizo, hapa nchini, juzi usiku ulifanyika mjadala kupitia Space ya mtandao wa Twitter na kukusanya watu zaidi ya 2,000 waliokuwa wanasikiliza au kuzungumzia mitihani hiyo.

Akizungumza katika mjadala huo ulioandaliwa na Mwananchi, Wakili Jebra Kambole alisema mzizi wa tatizo la kufeli katika mtihani wa sheria, haswa kwa Tanzania ni muda mfupi wa masomo katika taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo.

“Kuna haja ya kuboresha utaratibu kwamba kigezo cha kuingia LST kisiwe kwa kila mwenye ada, kuwepo na mtihani wapewe wanafunzi atakayefaulu ndiyo aingie, lakini kuna haja ya kuongeza muda wa masomo kutoka mwaka mmoja wa sasa,” alisema.

Ndani ya hoja ya ugumu wa kuupata uwakili zimeibuka nyingine lukuki zinazochagiza mzizi wa kufeli kwa wanafunzi wa taaluma hiyo.