Kuna nini TPA, kila anayeteuliwa anaondolewa kwa tuhuma

Muktasari:

  • Hapakaliki, ndivyo inavyoweza kusema ukizungumzia kibarua cha kila anayeteuliwa kuongoza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).


Dar es Salaam. Hapakaliki, ndivyo inavyoweza kusema ukizungumzia kibarua cha kila anayeteuliwa kuongoza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Uchambuzi wa Mwananchi Digital umebaini kuwa katika kipindi cha miaka 10, TPA wameteuliwa na kuondolewa watu sita kuiongiza mamlaka hiyo na kila aliyeondolewa haikuwa kwa kustaafu, bali ni tuhuma mbalimbali ikiwemo  ubadhirifu wa fedha na rushwa.

Mwaka 2012 mamlaka hiyo ilikuwa inaongozwa na Ephraim Mgawe na aliondolewa Agosti 23, 2012 baada ya tuhuma zilizoibuliwa na tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili ni pamoja na kushuka kwa mapato ya bandari kutoka Sh36 bilioni ya mwaka 2011 hadi Sh23 bilioni.

Hali hiyo ilisababisha TPA kuwasilisha maombi Septemba, 2012 wakikusudia kupandisha gharama za matumizi ya bandari kutoka asilimia 17 hadi 134 ili kukabiliana na nakisi ya fedha inayoikabili.

Baada ya sekeseke hilo, Madeni Kipande akakaimu nafasi hiyo lakini Februari 16, 2015 alisimamishwa kazi na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wakati huo, marehemu Samwel Sitta.

Zama za Kipande zilikoma  Aprili 16, 2015 alipotumbuliwa kwa tuhuma za rushwa, kesi ambayo inamkabili hadi sasa na juzi alisomewa mashtaka akiwa hoi  kitandani katika Taasisi ya Mifupa (Moi).

Awadh Massawe, aliachiwa kijiti kukaimu nafasi hiyo na baadaye Oktoba 18, 2015 aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alimteua kuwa mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo.

Massawe alidumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu tu na baadaye Desemba 7, 2015 ilikumbana na tumbuatumbua iliyoondoka na yeye, aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TPA, Profesa Joseph Mchambisaka na aliyekuwa katibu mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka.

Walikumbana na tumbuatumbua hiyo wakati Hayati John Magufuli akiwa Rais wa Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine, kiongozi huyo alitaja sababu za kuwatumbua ni uwepo wa mianya ya upitishaji mizigo bila utaratibu katika Bandari ya Dar es Salaam.

Juni 25, 2016, Deusdedit Kakoko alikaimishwa ubosi wa TPA kuanzia Juni 25, 2016 akitokea Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na baadaye kuteuliwa kuwa bosi kamili mwaka 2018.

Hata hivyo, naye hakudumu kwa tuhuma mbalimbali ukiwemo ubadhilifu wa fedha za TPA ambao ulimsababishia kusimamishwa kupishas uchunguzi wa tuhuma mbalimbali Machi 28, 2021 ambapo hadi sasa haijafahamika umefikia wapi.

Wadhifa wake huo ulikoma Aprili 4, 2021 baada ya panda shuka za kusimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizomkabili, hatimaye mkurugenzi mpya wa mamlaka hiyo aliteuliwa ambaye ni Eric Hamissi.

Hata hivyo, Hamissi hakudumu katika wadhifa kwani Julai 4, 2022 alitumbuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan alimtumbua kutokana na kukosekana ufanisi wa mamlaka hiyo.

Baada ya Hamissi wadhifa huo umeshikwa na aliyekuwa naibu mkurugenzi wa TPA, Plasduce Mbossa.