Kunenge: Mpango wa Kariakoo kufanya biashara saa 24 upo palepale

Kunenge: Mpango wa Kariakoo kufanya biashara saa 24 upo palepale

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakari Kunenge amesema mpango huo utafanyika baada ya kukamilika kwa uwekaji  mazingira mazuri katika eneo la Kariakoo

Dar es Salaam. Serikali imesema mpango wa maeneo ya Kariakoo kufanya biashara  kwa saa 24 upo palepale.

Hayo yamesemwa jana Mei 1,2021 na Mkuu wa Mkoa huo, Aboubakari Kunenge, kwenye shughuli ya kufuturisha iliyoandaliwa na Kampuni ya Silent Ocean kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania(JWT).

Kunenge amesema hilo litafanyika baada ya kukamilika kwa uwekaji  mazingira mazuri katika eneo hilo,ikiwamo taa za kutosha, barabara,usalama pamoja na maeneo makubwa ya kugesha magari.

"Tunataka kuirudisha ile Karikoo ya wakati ule, nchi mbalimbali ziliweza kuja kuchukua bidhaa hapa tena ikiwezekana tutayafanya zaidi tutakapokamilisha miundombinu niliyoitaja,”amesema Kunenge.

Kuhusu kuwafuturisha wafanyabiashara hao, Kunenge amesema ni jambo jema kwa kuwa ni moja ya thawabu iliyoandikwa katika vitabu pale mtu anapofuturisha watu na pia inasaidia kuzidi kujenga uhusiano bora kati ya kampuni na wateja wake.


Waziri wa Uwekezaji Goffrey Mwambe amesema tayari wameanza kufanyia kazi baadhi ya changamoto ikiwamo masuala ya kodi na wapo mbioni kupeleka muswada wa kubadili sheria ya uwekezaji ya mwaka 2003 na ile ya sera ya ujasiriamali ya mwaka 2003 na kueleza kuhitaji maoni ya wafanyabiashara.

Pia, katika kurahisisha usafirishaji Mwambe amesema safari ya ndege ya kwenda Gwanzuu China, inaanza wiki ijayo na itandoka na Wachina na itakapirudi itarudi na Watanzania waliopo China pamoja na mizigo.

Mkurugenzi mwenza wa Silent Ocean, Said Soloka amesema wanashukuru katika kipindi cha miaka 17 cha utendaji kazi wao,wameweza kutatua tatizo kubwa la kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara jambo ambalo awali lilikuwa ni changamoto kubwa kutokana na gharama kubwa kwa waliokuwa wakiisafirisha.

Soloka amesema awali mfanyabiashara alipaswa awe amejaza kontena jambo ambalo kwa mitaji midogo waliokuwa nao wengi wa wafanyabiashara hao iliwawia vigumu.

Katibu Mkuu wa JWT, Abdul Mwinyi amesema ahadi yao kwa Serikali na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania ipo palepale.