Kura kuamua mgombea mwenza wa Raila

Tuesday April 26 2022
kura pic
By Luqman Maloto

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Kenya, imeweka ukomo kuwa Aprili 28, mwaka huu ndiyo tarehe ya mwisho kwa wenye nia ya urais kuwasilisha majina ya wagombea wenza wao.

Chama cha ushirikiano wa uchaguzi, Azimio la Umoja One Kenya, kupitia baraza lake, kimeteua chombo maalumu kwa ajili ya kupendekeza majina ya watu ambao wanafaa kuwa mgombea mwenza.

Chombo hicho kitasimamia kura za maoni ili kupima umaarufu wa majina yanayotajwa kushika nafasi ya mgombea ili kumpata mtu sahihi zaidi atakayesimama na mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga.

Alhamisi iliyopita, viongozi wa juu wa vyama vinavyounda Azimio la Umoja One Kenya, walikutana kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC), Nairobi kwa ajili ya uzinduzi wa Baraza la Azimio, linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Uamuzi huo wa kuendesha kura za maoni kumpata mgombea mwenza, umeafikiwa kwa lengo mahsusi la kumsaidia kumwondolea shinikizo Raila, ambaye tayari ana majina kadhaa mezani na kuna msukumo wa kutoka kila upande.


Advertisement

Kutokana na changamoto za kumpata mgombea mwenza, Azimio la Umoja wameiomba Tume ya Uchaguzi kusogeza mbele muda wao wa kuwasilisha jina la mgombea mwenza ili waendeshe mchakato wao kwa umakini.

Katika barua kwenda IEBC, Azimio wametaka jina la mgombea mwenza wa Raila waliwasilishe kati ya Mei 29 na Juni 6, mwaka huu, hivyo wanaiomba tume iwape ruhusa hiyo ya kutolazimika kupeleka jina Aprili 28.


Mchakato wa kumtafuta

Alhamisi iliyopita (Aprili 21), Katibu Mkuu wa Azimio, Junet Mohamed, akisoma taarifa ya Baraza, alisema kuwa chombo kilichoundwa kuchakata kukusanya kura za maoni, kinatakiwa kuwasilisha majina yanayopendekezwa kwenye Baraza ili yafanyiwe kazi kupata mmoja.

“Baraza limeamua kuteua jopo la washauri ili lenyewe lipendekeze majina yaliyotajwa zaidi kwa mgombea urais kwa ajili ya uteuzi wa naibu mgombea urais,” alisema Junet.

“Baraza pia limeipa Kamati Kuu ya Taifa ya Ushirika (NCEC), kupendekeza haraka majina ya watu ambao wanafaa kuteuliwa kuunda Bodi ya Uchaguzi ya Azimio, Bodi ya Rufaa za Uchaguzi, Kamati ya Taifa ya Nidhamu na Jopo la Utatuzi wa Migogoro,” alisema Junet.

Haijawa wazi ni kwa namna gani timu iliyoundwa na Baraza la Azimio itaweza kufikia majina machache yatakayopendekezwa kwa mgombea urais na Baraza. Hata hivyo, mambo mawili yametajwa kuwa yatazingatiwa; mosi ni umaarufu wa mtu, pili ni jinsi mhusika anavyoendana na mgombea urais.

“Katika hili la kuendana, kutokana na ufahamu wa kina kuhusu Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais, William Ruto, itakuwa sahihi zaidi kumwezesha Baba (Raila), mtu ambaye watakuwa wanaendana na kuepuka kuendesha serikali ikiwa na upinzani wa ndani kwa ndani kama tunavyoona sasa,” kilisema chanzo ndani ya Azimio, kikiuambia ntandao wa The Nation, Kenya.

Chanzo hicho kikaongeza: “Kuhusu suala la umaarufu, hii itafafanuliwa na wachukua maoni kuwa uwezo wa watu wanaopendekezwa kusimama kufanya kampeni za kitaifa, utazingatiwa sana.”

Jambo lingine ambalo chanzo hicho kilidokeza ni kwamba kwa vile Raila anatokea Nyanza, hiyo inaondoa uwezekano wa mgombea mwenza kutoka Nyanza, Mashariki na hata Rift Valley, katika kufikiria kumpata mgombea mwenza.

Muhimu pia imebainishwa kuwa timu iliyoundwa na Baraza la Azimio, itachambua nguvu, udhaifu, fursa na hatari za mgombea mwenza anayefaa kupendekezwa.


Vigogo matumbo moto

Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, Bosi wa Narc Kenya, Martha Karua, Mbunge wa zamani wa jimbo la Gatanga, Peter Kenneth, Waziri wa Kilimo, Peter Munya, Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui na Mwakilishi wa Wanawake jimbo la Murang’a, Sabina Chege wamekuwa wakitajwa kama majina ya mstari wa mbele kuelekea uteuzi wa mgombea mwenza wa Raila.

Hoja kubwa ni swali je, watu hao wanaotarajiwa mmoja wao kutangazwa kama mgombea mwenza wa Raila, watakubali uamuzi wa timu iliyoundwa? Hata hivyo, imebainishwa kuwa uamuzi ni wa Bodi ya Azimio na kila mtu ndani ya Azimio la Umoja One Kenya, anapaswa kuuheshimu.

Katika mkutano wa Baraza la Azimio, uliofanyika Alhamisi iliyopita, KICC, Nairobi, mmoja wa wajumbe alitaka msimamo wa Baraza kuhusu mmoja wa watu wanaotajwa kuwa wanaweza kuteuliwa kushika nafasi ya kusimama kama mgombea mwenza, kutokeza hadharani na kujitangaza kwamba yeye ndiye atateuliwa.

Mjumbe huyo alikwenda mbele zaidi na kumtaja Kalonzo kuwa ameshajitaja hadharani kwamba nafasi ya mgombea mwenza wa Raila imewekwa kwa ajili yake.

Advertisement