Kutoka China: Tujifunze mpangilio wa miji na matumizi ya madaraja

Muktasari:

  • Katika vitu ambavyo nafikiri vinaweza kuvutia watu wengi wanaotoka katika mataifa yanayoendelea ni pale wanapozulu mataifa yaliyoendelea ama yaliyopo hatua kadhaa mbele yao, miongoni mwa mambo hayo ni mpangilio wa miji.

Katika vitu ambavyo nafikiri vinaweza kuvutia watu wengi wanaotoka katika mataifa yanayoendelea ni pale wanapozulu mataifa yaliyoendelea ama yaliyopo hatua kadhaa mbele yao, miongoni mwa mambo hayo ni mpangilio wa miji.

Naweza kusema mpangilio wa miji katika mataifa yaliyopiga hatua kimaendeleo ni tofauti sana na miji yetu mingi.

Ukitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam katika jiji kubwa la nchi tofauti ya mpangilio sio kubwa sana, hata Dar es Salaam na majiji mengine makubwa ndani ya Afrika Mashariki kama Nairobi au Kampala mambo ni yale yale.

China nayo bado ipo kwenye kundi la nchi zinazoendelea, lakini yenyewe unaweza kusema imeendelea kulingana na mafanikio ya kiuchumi yaliyofikiwa, nchi nyingi zinazoendelea zinaitazama kama mfano wa kuigwa.

Ukiachilia mbali kinachoweza kuigwa katika kusukuma gurudumu la kiuchumi katika mataifa yanayoendelea, pia namna ya upangiliaji wa makazi na miji katika Taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu duniani ni jambo linaloweza kuigwa.

China ambayo ni ya tatu kwa ukubwa dunia, ina majiji 155 yenye idadi ya watu inayoanzia milioni moja, kubwa zaidi ya Shanghai lenye watu zaidi ya milioni 24. Ukipita katika majiji hayo utaona tofauti kubwa na majiji yetu.

Binafsi nimepata bahati ya kuzulu majiji kadhaa mpaka sasa, ambayo ni Beijing (jiji la pili kwa ukubwa na makao makuu ya nchi), Guangzhou (jiji la tatu kwa ukubwa) Qingdao (jiji la 17 kwa ukubwa), Yantai (jiji la 46 kwa ukubwa) na Weihai ambayo linatajwa kuwa namba 125.

Ukiachana na maendeleo unayoweza kuyashuhudia katika miji hiyo, mpangilio wake ni jambo ambalo linafaa kuigwa, katika mji wa jiji la Weihai rafiki yangu mmoja kutoka Afrika ambaye ni mgeni kama mimi alipigwa na mshangao kuona mawaridi (red roses) yakiwa yamepandwa pembezoni mwa barabara.

Maua nyasi na miti vimepandwa karibia kila sehemu ya majiji ya China, huenda ni sera ya kitaifa au majiji yanashindana kupendeza, ni hali inayovutia.

Hata viongozi wao wa kitaifa wamekuwa wakitoa msisitizo juu ya utunzaji wa mazingira ambayo mwisho wa juhudi hizo majiji kupendeza. Juni katika siku ya kitaifa ya mazingira Rais Xi Jinping alitilia mkazo suala la utunzaji mazingira akisema ndiyo msingi wa kuishi kwa watu na maendeleo ya dunia nzima.

Alisema ana matumiani jamii zote zikichukua hatua za makusudi katika ustaarabu wa kiikolojia kwa kuwa na makazi bora, ardhi ya kijani, anga la blue na maji safi kwa ajili ya kizazi kijacho.

Inaelezwa kuwa katika muongo uliopita, watu wa China wamepanda zaidi ya hekta milioni 73.33 za nyasi na miti.

Pengine ni hatua za makusudi kwa kuwa Taifa hilo kwa miaka kadhaa limetajwa kuwa linaongozo kwa uzalishaji wa hewa chafu ambayo ni matokeo ya kutotunzwa vizuri kwa mazingira ya asili.

Katika vitu ambavyo vinaweza kushangaza wageni wengi ni namna nyasi, maua na miti vinavyotunza kwa ari na maarifa katika majiji hayo, pale inapobidi miti hutibiwa kwa kuchomwa sindano au hata kutundikiwa maji (drip).

Vile vile miti mingi huwekewa kingo za kulindwa kuharibiwa na shughuli za binadamu na hufuatiwa mwenendo wa ukuaji wake , kuhakikisha unakuwa katika mwonekano ambao wao wanautaka.

Watu waliotembelea Taifa hili miaka ya nyuma wanasema kuwa ilikuwa ni kawaida kuona moshi mzito ukiwa katika majiji makubwa na hata hewa haikuwa nzuri, lakini sasa unaweza kuona anga kwa uangavu ukiwa katika majiji tofauti na hewa nayo ni safi.

Ukiachilia suala la miti, maua na nyasi katika majiji hayo, suala lingine ni namna wanavyotumia madaraja ya juu, huku ni mengi sio kama kwetu na chini ya madaraja hayo ni maegesho ya magari ya kulipia.

Yaani pale chini ya Daraja la Mfugale au la Kijazi zinawekwa ‘Parking Slot’ vizuri na watu hupaki magari yao kwa kulipia, uzuri ni kwamba unaweza ‘ku-book’ ukiwa nyumbani, hivyo unatoka na gari lako ukiwa unajua utaliegesha wapi.

Vilevile kama hujafanya ‘booking’ ukiwa barabarani kuna skrini za kukuonyesha maeneo ya karibu yenye maegesho na idadi ya nafasi zilizobaki, kama maegesho yote yamejaa utajua hivyo utaamua mapema kutafuta namna nyingine.

Suala la mpangilio wa makazi nalo linaifanya miji yao ipendeze, yaani kuna Magomeni kota nyingi, hivyo maeneo mengi ya majiji yana mwonekano unaofanana, lakini pia yanachukua watu wengi kwa wakati mmoja.

Pengine wao wanatumia aina hiyo ya uendelezaji wa makazi kwa kuwa wana idadi kubwa ya watu.

Lakini kwa kuwa nasi na nchi nyingi za Afrika, bado tuna changamoto ya makazi bora njia hiyo inaweza kusaidia kutatua changamoto pia kupendezesha mji.

Mbali na kupendezesha, mji unapopangwa ni rahisi kutoa huduma za kijamii kwa kuwa njia na ramani zinaeleweka, hivyo hata mipango ya muda mrefu inaweza kutekelezwa kwakuwa iliachiwa nafasi. kwa sababu kila kitu kilipangwa kwa mpangiio maalumu.