Kwa nini wanawake hubadili maumbile licha ya madhara yake

Kwa nini wanawake hubadili maumbile licha ya madhara yake

Muktasari:

Kutokana na kupenda mwonekano au haja ya kutimiza malengo tofauti, idadi ya wanaorekebisha maumbile inazidi kuongezeka siku za hivi karibuni.

  



Dar es Salaam. Kutokana na kupenda mwonekano au haja ya kutimiza malengo tofauti, idadi ya wanaorekebisha maumbile inazidi kuongezeka siku za hivi karibuni.

Idadi kubwa ya wanaofanya hivyo, wataalamu wanasema ni wanaotaka kupunguza unene, wanaotamani kukuza au kuongeza matiti, makalio au kuwekewa homoni.

Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile wa Hospitali ya Aga Khan, Idan Njau anasema wanapokea wenye mahitaji tofauti na idadi yao inaongezeka kadri siku zinavyokwenda.

“Tunaowapata hapa Aga Khan ni wenye unene wa kupindukia au wanaohitaji kubadili matiti. Tunapata waliokatwa matiti kutokana na saratani pia ambao hutaka kutengenezwa wawe na shepu inayoonyesha wana matiti,” alisema Dk Njau.

Kwa sasa, anasema uhitaji ni mkubwa kutokana na mtindo wa maisha unaochangiwa na kutofanya mazoezi hivyo kuwa na uzito mkubwa au sura kujaa hivyo wengi kuhitaji marekebisho.

Mtu anayeongezwa ukubwa wa matiti au makalio anasema anachomwa sindano au kuwekewa maji maalumu yanayoweza kudumu muda mrefu mwilini.

Kuhusu malipo, anasema ni ghali kwa kuwa huchukua muda mrefu na kuhitaji utaalamu wa hali ya juu kuukamilisha upasuaji huo.

Upandikizaji viungo

Licha ya kurembesha na kuongeza maungo ya miili, daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha viungo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Laurean Rwanyuma anasema ni ngumu kumwekea mtu kiungo cha mwingine kutokana na kutoingiliana kwa kingamwili (antibodies).

“Watu huwekewa viungo vya mtu mwingine lakini hudumu kwa wiki tatu pekee baada ya hapo mwili unakataa kwa kuwa kila mtu ana kingamwili zake ndiyo maana viungo vingine kama moyo, figo na ini huwekwa viwapo DNA zimeoana na mgonjwa anaishi kwa kunywa dawa,” anasema.

Hata hivyo, Dk Njau anasema upasuaji wa kurekebisha maumbile una faida nyingi yakiwamo matibabu ya kisaikolojia.

“Mtu atajikubali na atakuwa ameridhika, itamsaidia kujiamini na kujituma zaidi na kipato kikaongezeka,” anasema.

Kwa waliopata majeraha kutokana na kipigo au kuungua moto anasema upasuaji huo huwawezesha kurudi hali zao za zamani.

“Tunatibu viungo vilivyoharibika kwa kipigo kinachowakuta akina mama, ajali za barabarani, kuungua moto zinazoacha makovu kurudishiwa viungo vyao vifanye kazi kama zamani,” alisema Dk Njau.

Kwa wenye matiti makubwa, Dk Njau anasema hufanya upasuaji kuyapunguza kutokana na madhara yanayoweza kusababisha yakiwamo maumivu ya mgongo ya muda mrefu hasa hasa mwanamke anapoinama.


Madhara ya upasuaji

Kama ilivyo kwa upasuaji mwingine, wa kubadilisha maumbile ya mwili nao una athari zake ikiwamo kupata matokeo usiyoyatarajia.

Dk Njau anasema kwa wanaojiremba wanaweza kupasuliwa ili kukuza makalio, mapaja au matiti lakini yakakua kwa namna ambayo haikutakiwa au yakaleta usumbufu mwingine wowote baadaye hivyo mhusika kutamani arudie umbo lake la zamani.

Madhara hayo, Dk Njau anasema hujitokeza kwa wanaowekewa vitu mbadala hasa makalio ambao wakati mwingine wanaweza kupata maumivu au michubuko wakitembea.

“Atakapoanza kuzeeka anaanza kushindwa kuhimili kubeba makalio hayo kwani hayapungui kama mwili unavyopungua kwa mtu anayezeeka,” anasema.

Vilevile, Dk Rwanyuma wa Muhimbili anasema mhusika anaweza kupata maambukizo yatakayosababisha makovu na vidonda vitakavyochukua muda mrefu kupona.

Madhara mengine anasema ni kupoteza maisha, “mtu anaweza kuwa anafanyiwa upasuaji lakini dawa za usingizi zikamlaza moja kwa moja asiamke tena.”


Gharama

Upasuaji wa kurekebisha maumbile unagharimu fedha nyingi.Dk Rwenyuma kanasema gharama hizo zinazoanzia Sh5 milioni.

“Hii ni hospitali ya umma kwa maana hiyo hii huduma inatolewa kulingana na uhitaji wa mteja na iwe kupunguza au kuongeza haipungua Sh5 milioni,” anasema.

Katika Hospitali ya Aga Khan, upasuaji huo unaanzia Sh13 milioni. Meneja Masoko na Mawasiliano wa Hospitali ya Aga Khan, Olayce Lotha anasema “Aga Khan inatoa huduma za upasuaji wa kurekebisha maumbile lakini gharama zake ni za juu kwa sababu muda mwingi unatumika kufanya hiyo kazi, vifaa na michoro muhimu kabla ya huduma.”


Sababu wengi kupasuliwa

Wataalamu wanasema wanawake wengi wanaongeza maumbile yao yakiwamo matiti, mapaja na makalio kuzirembesha sura zao huku wachache wakipunguza matiti lakini kwa wanaume, hutaka kupunguza mafuta yaliyozidi au kuwekewa homoni za kike.

Kali Rahaj ni miongoni mwa watu waliofanikiwa kubadili maumbile yao kwa kufanyiwa upasuaji wa kupunguza unene.

“Nilikuwa na kilo 123. Ukubwa wa tumbo ulinisukuma kufanya upasuaji kwani sikuwa navaa nguo zikakaa vizuri,” anasema.

Kali aliyefanyiwa upasuaji Hospitali ya Aga Khan miaka miwili iliyopita, alitumia Sh9 milioni.

Mwigizaji Muna Love amefanya upasuaji mara nne lakini analo lengo la kurekebisha viungo vyake mara 11.

“Nilikua napenda dimpoz msema kweli mpenzi wa Mungu sitaki maswali, huu ulikuwa upasuaji wa pili katika nne nilizofanya. Sasa hivi tukikutana ninatabasamu hata mkiniudhi ili muone dimpoz ya uso sasa ndiyo mtafurahi. Mungu ni mwema kwangu,” aliandika katika ukurasa wake wa Instagram.