Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kyecu yaahidi neema kwa wakulima wa ufuta

Ufuta ukiwa shambani. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Msimu wa zao la ufuta umeanza wilayani Kyela, ambapo bei imeanza kwa Sh2,560 ikiwa ni zaidi ya msimu uliopita, huku wadau na wakulima wakipongeza juhudi za serikali katika kutafuta soko.

Mbeya. Wakati msimu wa zao la Ufuta ukianza kwa bei ya Sh2,560, wakulima wilayani Kyela mkoani Mbeya wameonesha furaha yao na kupongeza uwazi wa mfumo wa uuzaji, huku serikali ikitoa mwelekeo wa zao hilo kiuchumi.

Kwa msimu wa mwaka jana, bei ya zao hilo ilianza kwa Sh1,800 ambapo hadi mwisho wa msimu, iliishia Sh2,300 hali ambayo imeleta tumaini jipya kwa mwaka huu kwa wakulima kujiinua kiuchumi.

Kyela ina mazao manne ya kimkakati ambayo yapo katika mfumo wa stakabadhi ghalani yakichangia uchumi kwa wananchi ambayo ni Cocoa, Ufuta, Mbaazi na Korosho, huku uzalishaji ukitarajia kuongezeka mwaka huu.

Msimu uliopita zaidi ya tani 300 za zao la Ufuta zilizalishwa na kuuzwa, huku mwaka huu matarajio ikiwa ni kufikia tani 600 ambapo wakulima wametakiwa kuzingatia ubora ili kuvutia soko kwa wanunuzi.

Katika mnada wa jana Juni 8 uliofanyika katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Kyela (Kyecu) jumla ya kilo 72,900 ziliuzwa baada ya wakulima kuridhia bei ya Sh2,560 kwa wanunuzi.

Kwa upande wa Cocoa ambalo ni zao mama, msimu wake unaendelea ambapo bei ya zao hilo imeonekana kupanda na kushuka, ambapo mnada wa juzi ziliuzwa kilo 196,140 kwa Sh 8,910 kwa kilo moja.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 9, Meneja Mkuu wa Chama cha Ushirika Kyela (Kyecu), Aman Hankungwe amesema bei hiyo si mbaya ikilinganishwa na msimu wa mwaka jana walivyoanza.

Amesema mkakati wa serikali ni kuona bei inafikia Sh2,700 kwa kilo moja, akieleza kuwa wakulima wanapaswa kuzingatia ubora ili kushawishi na kuvutia wanunuzi wakati juhudi zikiendelea kutafuta wateja zaidi.

“Tunahitaji zaidi ya bei hiyo lakini kwa kuanzia tunataka ifike angalau Sh2,700 kwa ajili ya wakulima wetu waweze kupata faida, mwaka jana tulikuwa na uzalishaji mzuri kufikia tani 300, lakini kwa mwaka huu tunayo matarajio ya zaidi”

“Kwakuwa ni mnada wa kwanza bado takwimu hazijawa sawa lakini tunatarajia kuzalisha tani 600, wakulima wajitahidi kuzingatia ubora na sisi uongozi tunaendelea kutafuta wateja zaidi ili kufikia malengo,” amesema Hankungwe.

Mkulima Elizabeth Msokwa amesema bei hiyo inawapa matumaini katika kujiimarisha kiuchumi akipongeza juhudi za Kyecu katika kuongeza idadi ya wanunuzi wa zao hilo.

“Kilimo ni maisha yetu, tunasomesha na kuendesha shughuli zote kupitia Ufuta na Cocoa, tunahitaji soko lenye kuvutia ili tufikie malengo, Kyecu wanasaidia sana kutufikishia wateja hatutumii nguvu sisi wakulima,” amesema Elizabeth.

Mdau wa kilimo wilayani humo, Jafeth Msunga amesema licha ya kuanza kwa bei rafiki, lakini mkulima hutumia gharama na muda mwingi kuandaa kilimo hicho akiomba serikali kuongeza juhudi.

“Tunaipongeza serikali kwakuwa kipindi hiki wameonesha uharaka na uwajibikaji haswa viongozi wa Kyecu, wanatafuta kampuni za ununuzi wa mazao yote yanayosimamiwa na mfumo na kutoa uwazi kwa wakulima.

“Tuombe malipo yafanyike kwa wakati ili kusaidia wakulima kuweza kumudu maisha yao kwakuwa wanategemea zaidi kilimo hiki, sisi wadau tunaridhishwa na utekelezaji wao,” amesema Msunga.