Latra: Tumieni tiketi mtandaoni kuepuka kubambikiwa nauli
Mkuu wa wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga(aliyevaa kofia ya blue) akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), Simon Maigwa pamoja Ofisa Mfawidhi wa LATRA mkoa wa Kilimanjaro, Paul Nyello(wa kwanza kushoto) wakikagua moja ya basi la abiria katika stendi kuu ya Mabasi Moshi Mjini.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Mkoa wa Kilimanjaro imesema uwepo wa tiketi mtandao utasaidia kupunguza changamoto za abiria kupandishiwa nauli kiholela kuelekea kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka mpya.
Moshi. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Mkoa wa Kilimanjaro imesema matumizi ya tiketi mtandao yatasaidia kupunguza changamoto za abiria kupandishiwa nauli kiholela kuelekea kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka mpya.
Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa ambayo kila ikifika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka wageni hufurika kwa wingi na kupelekea adha mbali ikiwemo foleni pamoja na nauli kupanda.
Kauli hiyo imetolewa leo, Desemba 7, 2022 na Ofisa Mfawidhi wa Mamalaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini mkoani Kilimanjaro (Latra), Paul Nyello wakati wa operesheni ya ukaguzi wa tiketi mtandao kwa mabasi yaendayo mikoani sambamba na utoaji elimu juu ya usalama barabarani katika Stendi Kuu ya Mabasi Moshi.
"Kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka, miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto ya baadhi ya watu kuzidishiwa nauli, lakini leo hii serikali imetoa maelekezo ya namna ya kutumika kwa tiketi mtandao ambazo zitapunguza changamoto iliyokuwepo," amesema Nyello.
Aidha ametoa rai kwa watoa huduma wote wa vyombo vya usafiri katika mkoa huo kuhakikisha katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka wanazingatia taratibu zote na sheria za usalama barabarani katika kutoa huduma.
"Wakati tunaelekea mwisho wa mwaka wa sikukuu, nitoe rai kwa watoa huduma, wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha madereva wao wanazingatia taratibu zote za na sheria za usalama barabarani katika kutoa huduma," amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simon Maigwa amewataka wageni wanaoingia katika mkoa huo wakati wa msimu huu wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka wahakikishe wanafuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo sio za lazima.
"Kwa yeyote anayeingia Mkoa wa Kilimanjaro katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka ahakikishe anafuata sheria za usalama barabarani, tumejipanga na tuna nguvu ya kutosha ya kuhakikisha kwamba wale wanaoingia na kutoka katika msimu huu wanakuwa salama," amesema.
"Tutaendelea kufanya ukaguzi kwa magari yanayotoka hapa mkoani kuelekea mikoa mingine kuhakikisha abiria wanafika makwao salama, madereva kabla ya kuondoka lazima tuhakikishe tumewapima kilevi ili kuhakikisha hawatarishi maisha ya watu," amesema Kamanda Maigwa.
"Wananchi wanaoingia katika mkoa huu wataendelea kuwa salama na tumejipanga hata kwenye masuala mengine ya kiusalama. Tunao askari wa kutosha hivyo tunawakaribisha sana katika Mkoa wa Kilimanjaro. Usalama ni wa kutosha na atakayejihusisha na vitendo vya kiuhalifu hatutasita kumchukulia hatua za kisheria,"
Naye, Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani mkoani hapa, Mohamed Nkya amesema wamejipanga kuhakikisha vyombo vyote vya usafiri vinavyotoka katika mkoa huo kuelekea mikoa ya jirani vinakuwa salama.
"Kamati tumejipanga na tumeongea na madereva wa mabasi makubwa kwasababu mkoa huu unapokea wageni wengi sana katika msimu huu wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka. Hivyo tumetoa elimu kwa waendeshe magari haya kuwa uangalifu kwa kuzingatia sheria za barabarani," amesema