Latra yaeleza uwezekano wa kupanda kwa nauli Mwendokasi

Muktasari:

  • Kikao cha wadau kimeketi leo jijini Dar es Salaam kujadili viwango vipya vya nauli kwa mabasi yaendeyo haraka maarufu Mwendokasi, ambapo Latra wamezungumzia uwezekano wa nauli hiyo kupanda.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Gilliard Ngewe amesema licha ya Serikali kutoa Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta nchini lakini hawategemei kiwango kipya cha nauli kilichotangazwa kwenye vyombo vya usafiri kitashuka.

Majibu hayo ameyatoa leo Mei 26 /2022 kwenye kikao cha wadau cha kujadili mabadiliko ya viwango vipya vya nauli kwa mabasi yaendeyo haraka maarufu Mwendokasi vinavyotarajiwa kutangazwa rasmi baada ya siku saba.

Ngewe mesema kilichosababisha kupanda gharama za uendeshaji kwenye vyombo vya usafiri si mafuta peke yake bali kuna vitu vingi vimepanda zaidi ya bidhaa hiyo kwahiyo hawategemei kama kiwango kitashuka.

"Kuna vitu vingi vimepandisha gharama ya uendeshaji kwenye vyombo vya usafiri mafuta ni moja ya bidhaa iliyochangia na inawezekana kufikia hiyo Julai bidhaa nyingine zikapanda maradufu hivyo hatutarajii kama viwango vya nauli vitashuka," amesema.

Ngewe amesisitiza kwamba mamlaka hiyo inapanga viwango kwa kuzingatia utalaamu na kuzingatia kipato cha wananchi.