Latra yagomea maombi ya daladala Arusha

Muktasari:

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imegoma kupokea maombi ya wafanyabiashara wapya wa daladala kuongezwa kwenye idadi ya watoa huduma ya usafiri ndani ya jiji la Arusha.

Arusha. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imegoma kupokea maombi ya wafanyabiashara wapya wa daladala kuongezwa kwenye idadi ya watoa huduma ya usafiri ndani ya jiji la Arusha.

Latra imegomea ombi hilo leo Jumamosi Novemba 19 mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete aliyekuwa kwenye ziara jijini Arusha kusikiliza kero za wananchi.

Akitoa kero yake mbele ya viongozi mbalimbali wa uchukuzi, mmoja wa wafanyabiashara wa daladala Jijini Arusha, Alex Kimaro amesema kero katika sekta yao ni Latra kufunga baadhi ya ruti zenye wateja wengi wahitaji wa huduma za usafiri huku wao wakikwama kiuchumi kwa kuwakosa abiria hao.

"Mimi natoka saccos ya frence corner, naomba mheshimiwa Waziri utusaidie kutuombea kwa Latra watufungulie baadhi ya ruti na kuongeza zingine hasa kutoka Murombo kwenda Chekereni lakini pia barabara ya Muriet kwani tumechukua mkopo wa milioni 100 na tunashindwa kufanya marejesho kutokana na tulinunua magari lakini tumenyimwa lesseni ya Latra"

Akijibu swali hilo, Ofisa Mfawidhi wa Latra Mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela amesema wamefunga ruti hizo kutokana na idadi ya daladala kwenye maeneo hayo kujitosheleza huku akiwataka watoa huduma hizo kuhamia barabara za pembezoni mwa mji ikiwemo barabara ya Afrika Mashariki kuelekea Nadosoito au Mkonoo.

"Barabara hizo nimezitaja bado zina nafasi kwa sasa lakini zinaombwa hasa, na mkichelewa mtakuta zimejaa huku mnapoomba mko zaidi ya 200 sasa wewe uliyesimama tukikupa upendeleo utasababisha wale wengine waliotanguliza maombi nao waje na hatuna nafasi hiyo kutokana na zilizopo tu zenyewe zinasababisha msongamano mkubwa sana hasa asubuhi na jioni" alisema Mwakalebela

Zaidi ya hayo, Mwakalebela pia aliwataka wafanyabiashara kusitisha kununua daladala ndani ya jiji la Arusha kwani wanaelekea kuzipiga marufuku vyombo hivyo kutoa huduma za usafirishaji ndani ya jiji la Arusha badala yake wanazipa kipaumbele mabasi madogo (coaster).

Kwa Upande wake Waziri Mwakibete alikubaliana na hoja hiyo ya Latra, amewataka wafanyabiashara hao kufuata sheria na kanuni hizo Ili kuleta tija ya huduma hiyo nchini.