Latra yaomba ushirikiano kuimarisha safari za usiku
Muktasari:
- Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Salum Pazzy amesema Serikali inategemea ushirikiano wa abiria ili kudhibiti madereva watakaoendelea kukiuka taratibuza usafirishaji ikiwamo kuwachuja bila kusitisha safari za abiria kwa saa 24.
Dar es Salaam. Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Salum Pazzy amesema Serikali inategemea ushirikiano wa abiria ili kudhibiti madereva watakaoendelea kukiuka taratibu za usafirishaji ikiwamo kuwachuja bila kusitisha safari za abiria kwa saa 24.
Pazzy amesema tathmini iliyofanyika kabla ya kurejesha huduma za usafiri huo wa 24, ulizingatia hali ya miundombinu na udhibiti uliopo sasa ikilinganishwa na miaka ya 1990.
Pazzy ametoa kauli hiyo leo Julai 5, 2023 wakati wa mjadala kuhusu uamuzi wa Serikali kuruhusu mabasi kufanya safari saa 24 kupitia Jukwaa la Mwananchi Twitter space linalofanyika kila Jumatano chini ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited(MCL).
Safari za usiku za mabasi ya abiria zimerejeshwa kufuatia kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha vikao vya Bunge Juni 28, mwaka huu.
Akizungumzia suala hilo, Pazzy amesema mabasi 47 yaliyofungiwa ratiba za saa tisa ni baada ya kubaini ukiukwaji wa sheria na sio kuwafungia biashara.
“Wengi wana nidhamu na taratibu wenye changamoto za betting tunawaonya, tunawalea na wakiendelea na fujo tunatoa adhabu, wakiendelea na fujo watajiondoa wenyewe kwenye huduma.
“Ni kweli kuna changamoto zilizoelezwa hapa lakini tunasisitiza ushirikiano, tuna mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi, kilometa 80 kwa saa kuna alamu itapiga kelele, abiria watoe taarifa ikitoa taarifa hiyo ya mfumo wa VTS, hivyo ndio tunaweza kushirikiana.”
Kwa mujibu wa Latra, mfumo huo wa VTS unaunganisha mamlaka hiyo, mmiliki wa gari na wote wanakuwa na uwezo wa kuona mwenendo wa dereva mwanzo mpaka mwisho wa safari.Mfumo unarekodi muda wa safari, jina na taarifa za dereva wa basi husika linakoelekea.
Pia, amesema tasnia hiyo ya udereva inatakiwa kurasimishwa kama ilivyo kwa taaluma nyingine zinazotoa adhabu ya kufungia leseni wasifanye kazi mahali popote.