LHRC: Ukatili kwa wanawake bado tatizo nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC,Wakili Anna Henga akizungumza na wageni waalikwa katika maadhimisho ya 74  ya siku ya haki za binadamu Duniani, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya haki za binadamu, ambapo matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yametajwa kutikisa.

Dar es Salaam. Licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali kulinda wanawake, ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa madawati ya jinsia, bado kundi hilo linakabiliwa na ukatili.

Hayo yamebainishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambapo kwa mwaka 2022 kimekusanya jumla ya matukio 346 ya ukatili dhidi ya wanawake kuanzia Januari hadi Juni.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga wakati wa maadhimisho ya siku ya Haki za Binadamu yaliyobebwa na kauli mbiu ‘Utu, Uhuru na Sheria kwa wote’.


Akizungumza katika maadhimisho hayo Anna amesema aina nyingi za ukatili dhidi ya wanawake zinazoripotiwa zaidi ni zile za ni ukatili wa kimwili na udhalilishaji, kupigwa na kutukanwa.

Aina nyingine ni ukatili wa kingono unaohusisha ubakaji na kulawiti, ukatili wa kisaikolojia na ukatili wa kiuchumi.

Mkurugenzi huyo amesema matukio mengi ya ukatili dhidi ya wanawake yaliripotiwa kutoka Mara, Mwanza, Arusha, Mtwara na Morogoro.

Kufuatia hilo ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria pamoja na wizara ya maendeleo ya jamii, ihakikishe inatungwa sheria mahususi na ya kina kuhusu ukatili wa kijinsia au Ukatili wa majumbani kwani sheria zilizopo haziangazii ipasavyo masuala ya ukatili wa kijinsia.

“Serikali pia kupitia Wizara ya Katiba na Mambo ya Sheria na Tume ya Kurekebisha Sheria, ifanye mapitio, kurekebisha na kufuta sheria zote za kibaguzi zinazoendelea kuwanyima wanawake haki zao na ambazo ni kinyume na misingi ya haki za binadamu kama ilivyoainishwa katika mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania ikiwemo sheria ya ndoa, sheria ya mirathi ya kimila na sheria ya uhamiaji.

“Serikali kupitia wizara husika iendelee kutimiza masharti yaliyoainishwa katika Mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania ni nchi mwanachama, ikiwemo kutuma ripoti kwa muda ulioainishwa,” amesema.