Lissu: Serikali imenilipa mafao yangu ya ubunge

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amesema Serikali imemlipa kiinua mgongo chake aliochukuwa anadai baada ya kutumikia nafasi ya ubunge kwa zaidi ya miaka mitatu.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amesema Serikali imemlipa kiinua mgongo chake aliochukuwa anadai baada ya kutumikia nafasi ya ubunge kwa zaidi ya miaka mitatu.

Lissu alivuliwa ubunge Juni 28 mwaka 2019 kutokana sababu mbalimbali ikiwemo ya kutojaza taarifa za mali na madeni na kutokutoa taarifa kwa Spika mahali alipo.

Wakati anavuliwa ubunge, mwanasiasa huyo alikuwa Ubelgiji akiendelea na matibabu baada ya kupigwa risasi 16 na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake Dodoma Septemba 2017.

Kwa muda mrefu, juhudi mbalimbali za kufuatilia kiinua mgongo chake na malipo ya matibabu hazikufanikiwa.

Februari mwaka huu, alipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ubelgiji anakoishi, Lissu alifikisha kilio hicho baadaye alieleza kuwa ameahidiwa kusaidiwa.

Pia alimuomba Rais Samia kumsaidia kupata hati ya kusafiria, jambo ambalo alisema lilitekelezwa ndani ya muda mfupi.

Jana, akizungumza katika mtandao wa Club House, Lissu alisema miezi miwili iliyopita alipigiwa simu na mtu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango akamweleza kuwa mafao aliyokuwa akidai yameshalipwa kwa kumaliza madeni aliyokuwa anadaiwa na benki.

“Nilikuwa na madeni ambayo nilikopa katika benki mbili na nilishtakiwa na mojawapo ya benki hizo kwa kushindwa kulipa mkopo uliokuwa unalipwa kupitia mshahara wa ubunge.

“Alivyonipigia simu akaniambia nimelipiwa madeni yangu yote kutokana na kiinua mgongo cha ubunge.

“Kwa hiyo naweza nikasema hadharani kwamba (hilo) limefanyiwa kazi na ni jambo jema kwa kweli. Sina madeni ya benki na usumbufu niliokuwa nikiupata,” alisema.

Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba alipoulizwa, alisema ni utendaji wa kawaida serikalini kulipa madeni ya wafanyakazi na viongozi hata mafao ya wastaafu.

Tunapolipa huwa tunapeleka kwa ofisa masuuli wa taasisi husika. Kwa mbunge, kuna mfuko wa Bunge. Pesa zinapelekwa huko. Hata hizo za matibabu zinaingizwa huko pia. Ukiwasiliana na Bunge watakuwa na taarifa zaidi kwa sababu wao ndio wanaowajua wanaostahili,” alisema katibu mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Uongozi wa Bunge haukupatikana jana kuzungumzia suala hilo.

Kuhusu fedha matibabu Lissu alisema, “nililetewa ujumbe niandike barua kuomba nilipwe stahiki zangu za matibabu na nimeshaiandaa kukamilika kwa kiasi kikubwa, ingawa bado natafuta nyaraka kwa sababu nimetibiwa Kenya na Ubelgiji.”