LIVE: Machumu aeleza undani wa ‘Tunawezesha Taifa’

Muktasari:

  • Machumu amesema kauli hiyo inalenga kuibua changamoto katika jamii na kuishirikisha sekta binafasi na sekta ya umma ili kuchukua hatua.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji Mwananchi Communication Limited, Bakari Machumu ameelezea sababu kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kuja na kauli mbiu mpya ‘Tunawezesha Taifa’ kuwa ni kuchochea maendeleo na utawala bora.

Machumu ameyasema hayo leo Juni 27 katika kipindi cha ‘Morning Mwananchi’ kinachorushwa na televisheni ya Mwananchi Digital inayopatikana Youtube, akisema pia kauli hiyo inalenga kuibua changamoto katika jamii na kuishirikisha sekta binafasi na sekta ya umma ili kuchukua hatua.

🔴 #LIVE: MORNING MWANANCHI: Chadema wamvaa Tulia kisa kina Mdee, kibano kipya

“Hivyo sisi kama kampuni tunavyo sema Tunawezesha Taifa, ni lazima uandishi wetu wa habari uondoke katika kukosoa tu, bali uwe uandishi wa habari wa kukosoa na kuonesha njia za kutokea, kwa kutafuta wataalamu mbalimbali waelezee tunawezaje kuepukana na tatizo fulani” amesema Machumu.

Hata hivyo, ameeleza na kusema katika miaka 23 tangu Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, ilivyo anza wamefanya mapinduzi makubwa ambayo yamewawezesha kwenda mbele zaidi kama kampuni.

“Tumeweza kuanzisha Jukwa la Fikra, ili kuweka uwanda wa watu kujadili mambo, ilikuweza kufikia watu wengi zaidi,” amesema Machumu.

Mbali na kusafirisha magazeti katika mikoa mbalimbali, Machumu amesema pia kampuni hiyo pia imeanzisha bishara ya vifurushi katika mikoa husika.

“Pia sisi kama kampuni tumeweza kutoa mikataba ya makubaliano na kampuni mbalimbali za magazeti ili kuweza kuchapisha magazeti yao kwa ubora,” amesema Machumu.


Amesema kwa mwezi mzima kampuni inawafikia zaidi ya wasomaji milioni 23 na kwamba bado wanaangalia namna ya kwenda mbele zaidi ili kutoa huduma za taarifa ambazo zinaenda kwa makundi tofauti tofauti.

“Tumeanzisha madawati kwa ajili ya kutoa taarifa kwa undani na kupata fursa mbalimbali, tunalo dawati la elimu, dawati la kilimo, siasa, afya, burudani,” amesema Machumu.