Ludewa kitimoto ruksa, masharti kuzigatiwa

Muktasari:

  • Uongozi wa Wilaya ya Ludewa waruhusu uuzaji na matumizi ya mazao yatokanayo na Nguruwe baada ya katazo hilo kudumu kwa miezi miwili.

Ludewa. Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa umeruhusu kwa masharti, matumizi ya nyama na mazao ya nguruwe, baada ya kupungua kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe iliyokuwa imeikumba wilaya hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 2, 2023 Afisa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Festo Mkomba amesema mnyama huyo ameruhusiwa kuchinjwa pamoja na kutumika kwa mazao yake kwa sharti la kutotoa mazao hayo nje ya kijiji ambacho mnyama huyo amechinjwa.

Amesema nguruwe yoyote atapaswa kufanyiwa ukaguzi masaa yasiyo pungua 48 kabla ya kuchinjwa.

“Ukaguzi wa awali ufanyike saa 48 kabla ya kuchinjwa na ufanywe na mtaalamu aliyeidhinishwa katika eneo husika, na nguruwe atakayeonesha dalili za aina yoyote ya ugonjwa, taarifa zitolewe kwa wataalamu wa eneo husika," amesema Mkomba.

Ameongeza kuwa mpaka sasa zaidi ya nguruwe 417 wamekufa kwa ugonjwa huo na wamefanya jitihada za kutosha kuhakikisha ugonjwa huo hauenei.

"Tumekuwa tukitoa elimu na kupita kukagua nguruwe katika maeneo mabalimbali ya wilaya hii na tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa huu japo haikuwa rahisi kwa kuwa kuna baadhi ya watu wasio waaminifu walikuwa wakichinja kwa siri na kuuza nyama hiyo huku wakiwa wameipa jina la Mbolea ya Ruzuku ili wasigundulike kwa urahisi," amesema Mkomba.