Lugumi giza nene, nyumba zake zapangishwa kinyemela

Thursday April 15 2021
lugumi pc
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Said Lugumi ameibuka upya akidai kuwa nyumba zake zilizokosa wanunuzi katika mnada wa Mamlaka ya Mapato tanzania (TRA) mwaka 2017 zimepangishwa kinyemela kinyume na utaratibu.

Mbali ya madai hayo, Lugumi pia amepinga kudaiwa na TRA Sh14 bilioni, ikiwa ndiyo sababu za mamlaka hiyo kushikilia nyumba zake, moja ikiwa Upanga na mbili Mbweni JKT jijini Dar es Salaam, akisema madai halisi ni Sh3.6 bilioni.

Nyumba hizo ndizo zilimuibua Dk Luis Shika, sasa marehemu, na kauli yake ya “Mia tisa itapendeza”, alipotangaza dau kwa nyumba zote tatu katika mnada mmojawapo, lakini baadaye ikabainika kuwa licha ya kushinda hakuwa na fedha hizo za kununua nyumba husika.

TRA ilipoulizwa kuhusu kupangishwa kwa nyumba hizo imesema haina taarifa na kuwa masuala ya kodi ni siri ya mamlaka hiyo na walipa kodi husika.

Kamishna Msaidizi wa TRA, Msafiri Mbibo alipoulizwa kwa simu juzi kuhusu nyumba hizo, alisema; “sina hizo taarifa, lakini masuala ya kodi ni ya mtu binafsi, sheria hairuhusu, ni confidential (siri).”

Madai ya Lugumi yamekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kudai kuwa TRA ilimbambika madai ya kodi ya Sh2 bilioni alipokuwa rumande katika Gereza la Segerea mwaka 2018, kisha ikakamata akaunti zake zote.

Advertisement

Akizungumza na Mwananchi jana, Lugumi alisema mbali na kugundua kuwa nyumba zake zinapangishwa, alipoteza vifaa vyake vilivyokuwa ndani ya nyumba hizo wakati zinachukuliwa.

“Mambo yalikuwa yanafanyika kwa nguvu tu, ndiyo maana kuna vitu vyangu vingi vilichukuliwa kwenye nyumba hizo, hasa nyumba ya Upanga ambayo ndiyo ilikuwa ofisi yangu,” alidai Lugumi, ambaye hata hivyo hakusema vitu hivyo vina thamani gani.

Kuhusu madai ya kodi, Lugumi alisema, “mimi sidaiwi hela hizo, ninachodaiwa ni Sh3.6 bilioni. Walileta bili mwaka 2012 na wao ndiyo walinipa msamaha wa riba. Mwaka 2017 wakaleta deni hilo wakiwa wanatumia taskforce (kikosi kazi), mara polisi,” alisema.

Alipoulizwa kwa nini asiende TRA kuzungumza nao ili wayamalize, alisema; “siwezi kuchukua hizo nyumba mpaka wanirudishie vifaa nyangu walivyovikuta,” alisema.

Licha ya mnada wa nyumba hizo kurudiwa mara mbili na kampuni ya udalali ya Yono, hazikupatikana fedha zinazolingana na thamani za nyumba husika au na fedha zilizokuwa zinatakiwa.

Mwananchi lilifika kwenye nyumba hizo zilizopo Upanga na kukuta kuna watu wanaishi.

Mmoja wa watu aliyekuwamo alipoulizwa kama kuna nafasi ya kupanga alisema tayari kuna watu.

Kwa upande wa nyumba zilizopo Mbweni, mmoja wa walinzi aliyeomba kutotajwa jina lake gazetini alisema nyumba zinapangishwa.

“Nyumba mbili zimeshapangishwa ila imebaki moja. Wapo watu wa kawaida na wanafunzi wanaoishi hapa,” alisema mlinzi huyo.

Katika mazingira kama hayo, Wakili Onesmo Mpinzile alisema inapotokea mnada umeshindwa kumpata mnunuzi anayeweza kulipa thamani inayotakiwa, sheria inamruhusu mdai kutumia njia nyingine kupata fedha zake.

“Anaweza kuiendesha mali iliyowekwa dhamana mpaka deni lake litakapoisha au akamtafuta mtu wa kuendesha kwa niaba yake na wanaweza kuingia ubia wa biashara na mdaiwa kuendesha biashara mpaka mdai atakapopata fedha anazodai,” alisema wakili huyo.


Dk Shika avuruga mnada

Katika mnada wa pili wa nyumba hizo ndipo aliibuka Dk Shika, maarufu kama ‘Mia tisa itapendeza’, aliyejitokeza na kutangaza kununua nyumba tatu, moja Sh900 milioni na nyingine Sh1.1 bilioni na nyingine ya Upanga Sh1.2 bilioni, lakini alipotakiwa kutoa asilimia 25 kama yalivyo masharti ya mnada alishindwa kutoa.

Baada ya polisi kumhoji Dk Shika walikosa maelezo ya kutosha wakamkamata kwa madai ya kuharibu mnada.

Baadaye Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema jeshi hilo linahisi Dk Shika alitumwa na Lugumi kutokana na mazingira ya tukio husika.

“Aliwekwa na Lugumi ili kukwamisha mnada. Ingawa sina facts (vielelezo) kuthibitisha hilo, lakini alichokuwa anafanya kinatufanya tuamini hivyo.” Kwa sababu alikuwa anapandisha bei kila nyumba ili washiriki wengine wasinunue,” aliongeza.

Advertisement