Lusinde ang’aka akiwashukia wanaomsema vibaya Magufuli

Lusinde ang’aka akiwashukia wanaomsema vibaya Magufuli

Muktasari:

  • Mbunge wa Mvumi (CCM),  Livingstone Lusinde amewashukia wabunge na viongozi wanaopinga mambo mazuri yaliyofanywa na rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli.

Dodoma. Mbunge wa Mvumi (CCM),  Livingstone Lusinde amewashukia wabunge na viongozi wanaopinga mambo mazuri yaliyofanywa na rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli.

Lusinde ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 13, 2021 alipokuwa akichangia mapato na matumizi ya fedha ya ofisi ya waziri mkuu na taasisi zake mwaka 2021/22.

Amesema haiwezekani kuwa na amani na utulivu wakati kuna watu wanamsema vibaya Magufuli akibainisha kuwa  haiwezekani kuwa na viongozi wanaojaribu kupinga mambo mazuri yaliyofanywa na Magufuli.

“Haiwezekani, hatuwezi kuwavumilia hawa wanaomsema vibaya Magufuli maana watamsema vibaya Samia (Suluhu Hassan) hii ni tabia..., jamani Magufuli ameifanya kazi nzuri sana nchi hii. Lazima tukubaliane unajua kuna wengine wanafikiri Rais Samia alikuwa nje ya benchi akaingia kucheza mpira hapana, Samia alikuwa  akicheza pamoja na Magufuli,” amesema.

Amebainisha kuwa aliyemtaja Samia alikuwa Magufuli na kwamba siku zote kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021 alikuwa akijitabiria kifo chake kwa kuwataka watu wamheshimu kwa kuwa ameacha alama katika Bara la Afrika.

“Hivi leo ni mbunge gani hakutetewa na Magufuli,  tupo humu ndani kwa sababu ya Magufuli na Samia. Walipita kila sehemu  kuwaombea kura. Kuna watu hapa walikuwa hawachaguliki lakini  Magufuli na Samia wakapita wakasema tupeni huyu tutafanya naye kazi tutamrekebisha,  kwa sababu yao wakachaguliwa.”

“Leo Magufuli asemwe vibaya na sisi tupo hata 40 haijafika, hili jambo halikubaliki, hawa watu washike adabu na adabu ziwashike. Hatutaki warudie tena mambo ya kipuuzi kama hayo,” amesema mbunge huyo.

Lusinde amesema ni vyema wakatengeneza vitabu vidogo kwa ajili ya kukumbusha ahadi zilitolewa na viongozi wakuu wa kitaifa.

“Alikopita Rais Samia aliahidi, alikopita Dk Magufuli aliahidi sasa badala kila mbunge anakumbusha ahadi za Rais ni vyema zikawekwa katika kitabu kimoja tukajua ahadi za viongozi ni hizi,” amesema.