Maabara ya upasuaji bila kufungua fuvu kielelezo cha mapinduzi ya sekta ya afya

Tuesday August 31 2021
MOI pc

Madaktari bingwa wa MOI wakimfanyia upasuaji mkubwa mgonjwa katika maabara maalum ya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu (Angio Suite).

By Maliki Muunguja

Sina hakika kama kuna namna ya kipekee ambayo tunaweza kuwashukuru wanasayansi na wavumbuzi mbalimbali ikakidhi na kukonga nyoyo zao ipasavyo.

Kwa hakika wamefanya kila kitu kufanyika kwa wepesi ambao kwa nguvu na akili za binadamu wa kawaida isingewezekana au pengine ingechukua miongo kuja kukifanya katika uwezo huo.

Teknolojia imetenda maajabu karibu katika kila sekta. Kada ya afya haiko nyuma katika hili, kwani kwa sasa imekuwa ikipokea vumbuzi mbalimbali zinazoendelea kuokoa maisha ya watu ulimwenguni.

MOI pcc

Darubini ya kisasa ya upasuaji wa ubongo.

Achilia mbali, matibabu ya masafa, vifaa vya kisasa kama vile MRI, maabara za matibabu ya moyo, matibabu ya saratani, chunguzi za kisasa, vitendanishi n.k, ambavyo ni sehemu ya jitihada za uboreshaji wa huduma za afya lakini leo dunia inazungumzia mapin-duzi makubwa katika eneo la uchunguzi na tiba. Bila shaka utakuwa umeshasikia kuhusiana na upasuaji bila ya kufungua fuvu (Angio Suite) na kama haujasikia, basi hii ndiyo fursa adhimu ya kufahamu kuhusiana na matibabu hayo ya kisasa kuwahi kufanyika nchini.

Historia imeandikwa, kwani matibabu haya kwa sasa yamefika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambapo kwa sasa Watanzania wanaweza kupatiwa huduma za uchunguzi na tiba kwa kutumia utaalamu huo.

Advertisement

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Respicius Boniface katika mahojiano yake na gazeti hili, anasema kuwa “Angio Suite” ni msamiati wa kitaalamu ambao unamaanisha “maabara ya upasuaji wa ubongo.”Anasema kabla ya ujio wa maabara hii, Serikali tayari ilishawekeza kiasi cha Sh7.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara hiyo ambayo haikuwahi kuwapo nchini huku akikiri kabla ya hapo kuwapo kwa maabara ndogo za matibabu ya moyo pekee kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF). “Hapo nyuma hakukuwa na maabara iliyokuwa na uwezo wa kufika hadi kati-ka ubongo sababu nyingi zilizokuwapo ni kwa ajili ya moyo tu,” anaeleza Dk Boniface.

MOI pccc

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Respicius Boniface.

Anasema zaidi ya kufanya uchunguzi na upasuaji wa moyo pekee, maabara hiyo ina uwezo mkubwa wa kuchunguza na kutibu sehemu zingine za mwili kwa ufanisi ule ule.

Anaeleza kuwa si MOI pekee, bali hata Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wanaitumia maabara hiyo kwa matibabu kadha wa kadha.

Dk Boniface anabainisha kuwa maabara hiyo imenunuliwa kutoka katika kampuni ya Siemen iliyopo Ujerumani.

Kwa sasa Tanzania ni nchi pekee yenye maabara hiyo ya kisasa ya uchunguzi na tiba ya upasuaji bila kufungua fuvu kwa Afrika, baada ya Afrika Kusini.

“Kwa kuwa ni teknolojia mpya kabisa kwa Tanzania na Afrika, madaktari kutoka Marekani wamekuwa wakija kujenga uwezo kwa wataalamu wetu wa afya namna ya kuitumia kwa ufanisi,” anafafanua Dk Boniface.

Inavyofanya kazi

Anaeleza kuwa maabara hii hufanyia kazi eneo lengwa kwa kupitia mishipa mikubwa ya damu iliyopo mapajani kwa kuingiza katheta (mrija) ambao unaweza kuusogeza taratibu mpaka katika eneo husika kwa msaada wa screen maalumu inayoonyesha uelekeo wa katheta ndani ya mwili.

Anasema baada ya kufikia eneo lililoathiriwa, unaweza kulitibu mara moja na kutoka kwa haraka. “Kupitia mishipa ya damu, ndiyo unaweza kufanya upasuaji wa bila ya kufungua fuvu na ikumbukwe magonjwa mengi yanaanzia katika mishipa ya damu kama vile uvimbe,”anaongeza.

Faida zake

Moja ya faida zinazopatikana anaeleza ni mkombozi kwa wagonjwa wenye matatizo ya muingiliano wa mishipa (arteriovenous malformation) ambapo hapo awali njia pekee ilikuwa ni kuwapandisha wagonjwa hao ndege waende nje ya nchi ikigharimu si chini ya Sh60 milioni wakati ukitibiwa hapa nchini ni nafuu zaidi kwa gharama ya kuanzia Sh8 mpaka 15 milioni pekee. “Vifaa vyake vile ili uweze kununua ilikuwa lazima ikutoke si chini ya Sh5 mpaka 8 milioni,” anaeleza.Kutokana na ujio wa maabara hii sasa wanaweza kutibiwa, kwa kuanza kufanyiwa uchunguzi na kugundua tatizo halafu matibabu.Kizuri zaidi, upasuaji huu hauhatarishi maisha ya mgonjwa kwa kupoteza damu nyingi kwa kuwa ni wa kisasa na usiohusisha uchanaji eneo kubwa la mwili.

Akiongezea, Dk Boniface anasema mgonjwa anayefanyiwa matibabu hayo anaweza kuchukua muda mfupi tu baada ya tiba na kuruhusiwa kuondoka tofauti na ule utaratibu mwingine.Maabara hiyo pia inatibu matatizo mengine ndani ya mwili kama vile uvimbe kwa wanawake (fibroids) ambayo yamekuwa yakiwasumbua wanawake wengi na hata matatizo ya ini.

Kuanza kufanya kazi rasmi

Dk Boniface anasema kuwa maabara hiyo imeanza kufanya kazi rasmi Januari 27, 2021 ambapo mgonjwa wa kwanza alifanyiwa upasuaji huo wa bila kufun-gua fuvu. Anaweka wazi kuwa MOI ilitumia mtaalamu kutoka Afrika Kusini, akishirikiana na wataalamu wa taasisi hiyo kufanya upasuaji huo ambao ulifanikiwa kwa asilimia 100.Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo MOI, Dk Nicephorus Rutabasibwa anasema kuanza kwa maabara hii kumeleta mageuzi makubwa katika huduma za uchunguzi na upasuaji wa ubongo hapa nchini kwani hakuna mgonjwa atakayelazimika kwenda nje ya nchi kufuata huduma hii ambayo ilikuwa haipatikani hapa nchini.Anasema kuwa hadi kufikia mwezi Mei wagonjwa 23 walikuwa tayari wameshapatiwa huduma katika maabara hii, zamani ilikuwa lazima waende nje ya nchi kwa kuwa huduma hii haikuwepo.“Kwa haraka gharama ambazo tumezitumia hapa kutibu wagonjwa 23 ni Sh200 milioni na ikiwa wagonjwa wangeenda nje wangetumia si chini ya Sh600 milioni, unaona ni kiasi gani fedha kinaokolewa kwa uwekezaji wa Serikali katika afya,” anasema Dk Rutabasibwa.

Pia, anasema wamefanikiwa kuanzisha huduma za upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu na wagonjwa 800.Anataja mafanikio mengine kuwa ni kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo kwa wagonjwa watano, kunyoosha vibiongo kwa watoto 12 na upasuaji wa uti wa mgongo kwa kupitia tundu dogo kwa wagonjwa 120.

Anasema katika kipindi hicho wameanzisha wodi maalum ya kulazwa na kufanyiwa upasuaji siku hiyo hiyo na wagonjwa 335 wamehudumiwa na huduma ya dawa za usingizi pasipo kulala na wagonjwa 250 wal-inufaika na hivyo kuwezesha huduma muhimu za matibabu kutolewa nchini kwa asilimia 95.

Uwezo wa ufanyaji kazi

Dk Boniface anasema endapo katheta zitakuwa za kutosha, wagonjwa na wataalamu wenye uzoefu wa kuridhisha, maabara hiyo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wanaohitaji kutibiwa ubongo mpaka wa nne (4) lakini kwa wale wanaofanyiwa matibabu ya kawaida wanaweza kufika mpaka saba kwa siku kwa kuwa ni teknolojia ya kisasa na fanisi zaidi.

Changamoto

Dk Boniface anasema moja ya changamoto kubwa kwa sasa katika macho ya watu wengi ni vile matibabu haya kutokuwapo katika mipango ya bima kwa kuwa gharama zake zinaonekana kuwa juu kwa mtu mmoja mmoja.

Mikakati

Ugonjwa wa Uviko-19, umekuwa ndiyo kikwazo cha mkakati wa MOI kupeleka timu ya wataalamu wa afya nje ya nchi kwa ajili ya kujengewa uwezo wa utaalamu huo ambapo Dk Boniface kwa maoni yake anaona bado kama taasisi haijafikia uwezo wake wa juu.

Hitimisho

Uwepo wa maabara hii Taasisi ya MOI imeandika historia kubwa hapa nchini na ni sehemu ya uungaji mkono jitihada za aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli katika kuboresha sekta ya afya nchini. Watanzania wanashauriwa kuendelea kuamini uwezo wa maabara hiyo na kutokusita kufika MOI na MNH kwa matibabu yanayohusu matatizo ya mishipa ya damu na men-gineyo.

Kuhusu MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) ni taasisi inayojitegemea iliyoanzishwa chini ya Sheria Na 7 ya 1996 ikiwa na lengo kuu la kutoa huduma za ngazi za msingi, kati na juu za kinga na tiba katika kada ya mifupa, tromatolojia na upasuaji wa mfumo wa fahamu, na pia kuwa mfano wa kuigwa kwa usimamizi mzuri wa hospitali nchini Tanzania.

Taasisi hii pia inahusika katika ukuzaji wa rasilimali watu kwa taifa na pia ina-fanya utafiti katika fani hizi kwa nia ya kutengeneza njia rahisi za matibabu ya wagonjwa na kupunguza hali duni kwa wanajamii.

Hivi sasa Taasisi ina uwezo wa vitanda vipatavyo 150, (binafsi 30 na jumla 120).Kukamilika kwa jengo jipya la MOI (MOI Awamu ya Tatu) Taasisi hii itakuwa na uwezo wa zaidi ya vitanda 380, itajumuisha pia ufungaji wa mashine za MRI, CT-SCAN na kuanzisha huduma za tiba za masafa ambapo huduma zote zitatolewa kulingana na mfumo usiohusisha matumizi ya nyaraka nyingi.

Usimamizi wa taasisi hiyo umeegemea katika dhana mpya ya mchanganyiko wa ushirikiano wa umma / binafsi inayolenga kuboresha utendaji na kujiendeleza.

Advertisement