Maajabu Mti wa Nyerere yawashangaza waandishi wa habari

Muktasari:

  • Ufahamu mti wa maajabu maarufu huitwa mti wa Nyerere unaopatikana katikati ya Hifadhi ya Msitu wa Rondo inayomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi. 

Mtwara. Mti huo umekuwa ukitumika kama sehemu ya matambiko na maombi mbalimbali ambapo watu hufika katika eneo hilo na kutoa sadaka kisha kuondoka na gome la mti huo ulioanza kutumika miaka ya 70 baada ya Mwalimu Julius Nyerere kufika na kuchukua gome la mti huo na kuondoka nalo.

Akizungumza na waandishi wa habari wa mikoa ya Lindi na Mtwara walipotembelea Hifadhi ya Msitu huo Afisa Muongoza Utalii hifadhi asilia ya Rondo, Denis Joas amesema kuwa mti huo umekuwa wa kihistoria kubwa.

Alisema kuwa mwaka 1976 Mwalimu Julius Nyerere  alipita Rondo kuzindua mradi wa maji na kuuliza juu ya mti ujulikanao kama minanga (Kizanaki) na kupelekwa katika mti huo  ambapo alibandua gamba la mti huo  na kuondoka nalo hivyo kuwavutia watu na walianza kuamini kuwa huo mti ni dawa.

“Baada ya hapo watu mbalimbali wamefika na  kutumia kama sehemu ya kuwatatulia matatizo yao ama wakiwa na shida za kifamilia na wengine wakitaka kupanda vyeo, kupata pesa  wanaomba na kuondoka na gamba la mti huo ambapo wenye imani wamekuwa wakifanikiwa,” amesema.

“Mti huu kwa Kiswahili unajulikana kama Mkufi watu ni wengi wanakuja kutembelea mti huu ambao wamepata shuhudia  za watu waliochukua gamba na kuombea shida zao na zikatatuliwa ambapo wengi wao ni viongozi wa serikali, taasisi binafsi,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Lindi, Fatuma Maumba alisema kuwa ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na kuwafanya wanahabari kufahamu kuhusu mti wa Nyerere.

“Yapo mambo mengi tulikuwa tunasikia lakini leo tumekuja kujifunza na kuona kumbe msitu huu una wanyama kama wengi kama simba, tembo, nyoka, twiga na ndege wa aina mbalimbali wanaopatikana katika Rondo kreta,” amesema.

“Tunaambiwa kuwa mwalimu Nyerere alifika hapa katika mti huu na kuchukua gome la mti  na kuondoka nalo leo umekuwa ni mti ambao ni kivitio ambapo watu wengi wamekuwa wakija na kuweka pesa kisha kuchukua gome la mti na kwenda kuomba kile unachotaka wakiamini itawasaidia,” alisema Maumba.