Maajabu ya sekondari ya Ilboru

Dar es Salaam. Kazi kubwa imefanyika kwa shule ya sekondari Ilboru ya mkoani Arusha ambayo mwaka ilishika nafasi ya 36 kitaifa, lakini katika matokeo yaliyotangazwa juzi, imevuka nafasi nyingi hadi kuwa ya pili.

Ilboru inaingia katika orodha hiyo huku ikiwa na historia ya kushika nafasi ya kuanzia 36 hadi 53 katika miaka mitano iliyopita. Mwaka 2015 shule hiyo ilishika nafasi ya 53 kitaifa, 2016 nafasi ya 42, 2017 nafasi ya 39 huku mwaka 2018 na 2019 ikishika nafasi ya 36.

Ilboru ndiyo shule pekee ya Serikali iliyoingia katika orodha hiyo ambayo shule binafsi zilionekana kuendelea kuchuana vikali kwa nyingine kupanda na nyingine kushushwa katika orodha hiyo.

Mbali na kushika nafasi ya pili katika orodha hiyo, Ilboru pia imefanikiwa kutoa wanafunzi wawili bora ambao, ni Ashraf Ally na Derick Mushi walioshika nafasi za tano na saba kitaifa.

“Tumepokea matokeo haya kwa furaha kubwa, yamechangiwa na ushirikiano uliopo baina ya walimu, utawala na wanafunzi ambao wamekua wakiwaandaa tangu kidato cha kwanza,” alisema Denis Otieno ambaye ni Mkuu wa shule hiyo

Alisema mbali na kufurahia matokeo hayo mikakati yao imekuwa ni kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri zaidi.

“Jambo hili limekuwa likiwapa kazi kubwa walimu kufanya marejeo mengi bila kuchoka kwa wanafunzi wetu. Serikali pia imetoa mchango mkubwa katika haya matokeo,” alisema Otieno.


Ilboru na daraja sifuri

Licha ya Ilboru kutoingia katika orodha ya shule kumi bora katika miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, lakini ilikuwa ikifanya vizuri huku ndani ya kipindi hicho ni mwanafunzi mmoja pekee ndiye alipata daraja sifuri kati ya wanafunzi 599 waliofanya mtihani ndani ya miaka mitano hiyo.

Pia katika kipindi hicho ni wanafunzi 15 pekee ndiyo waliopata daraja la nne, wanafunzi 12 wakipata daraja la tatu, 161 wakipata daraja la pili na wanafunzi 333 wakipata daraja la kwanza.


Yavunja rekodi

Rekodi hiyo imekuja kuvunjwa katika mtihani wa taifa wa mwaka 2020 ambapo hakukuwa na daraja la tatu, nne wala sifuri, huku mwanafunzi mmoja pekee ndiye alipata daraja la pili na wengine 118 wakipata daraja la kwanza.

Katika matokeo hayo Shule ya Wasichana ya St Francis ya Mbeya ilishika nafasi ya kwanza kitaifa ikiwa imepanda kutoka nafasi ya pili mwaka 2019 huku ikiishusha sekondari Kemobos ya Kagera hadi nafasi ya nne. Shule nyingine zilizofanya vizuri ni Cannosa (Dar), Kemobos (Kagera) na Feza ya Dar es Salaam. Pia kuna Ahmes ya St Aloysius Girls, Marian Boys (Pwani), St Augustine Tagaste ya Dar es Salaam.