Maandalizi ya kesi dhidi ya George Stinney

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Katika matoleo yaliyopita ya mfululizo wa makala hizi, tuliona kuwa Ijumaa ya Juni 16, 1944, Jimbo la South Carolina lilimnyonga George Stinney (14), aliyepatikana na hatia ya kumuua Betty June Binnicker aliyekuwa na miaka 11 katika mji wa Clarendon County wa Alcolu.

Katika matoleo yaliyopita ya mfululizo wa makala hizi, tuliona kuwa Ijumaa ya Juni 16, 1944, Jimbo la South Carolina lilimnyonga George Stinney (14), aliyepatikana na hatia ya kumuua Betty June Binnicker aliyekuwa na miaka 11 katika mji wa Clarendon County wa Alcolu.

Betty June Binnicker na Mary Emma Thames mwenye umri wa miaka 7, walitoweka Alhamisi ya Machi 23, 1944. Wachunguzi waligundua miili yao mapema asubuhi iliyofuata. Baiskeli ya Binnicker na gurudumu lake la mbele lililojitenga, lilikuwa limewekwa juu ya miili yao.

Mamlaka ya mji huo ilimtuhumu George Stinney kwa kuwaua wasichana wote wawili. Lakini, kwa sababu zisizojulikana, Stinney alishtakiwa kwa mauaji ya Binnicker pekee. Siku 83 baada ya vifo vya wasichana hao, bila kukata rufaa, George Stinney alinyongwa kwa kutumia kiti cha umeme jimboni South Carolina.

Wakazi wa Alcolu waliotikiswa sana na tukio la mauaji ya wasichana wawili, walihudhuria kwa wingi maziko yao yaliyofanyika Jumatatu ya Machi 27, 1944.

Vijana wa eneo hilo walikuwa wamejaza Kanisa la Kibaptisti la Clarendon. Mchungaji Paul Batson aliyeongoza ibada akisaidiana na makasisi wawili alisoma neno la Biblia kutoka Warumi 12:19 lisemalo: “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.”

Watu walikuwa na ghadhabu dhidi ya George Stinney wakiamini kuwa aliwabaka na kuwaua wasichana hao.

Serikali iliendelea kumhamisha George kutoka jela moja hadi nyingine kwa sababu watu wengi katika eneo la Manning walikuwa na nia ya kumkamata na kumuua. Kulikuwa na chuki sana kwa kila mtu wakati huo.

George Stinney hakuwa mlengwa pekee wa chuki hiyo kutoka kwa weupe. Uadui dhidi ya watu weusi wa Alcolu uliendelea kuongezeka mara tu baada ya mauaji.

Siku mbili baada ya mazishi, baraza la majaji lilikutana katika kaunti ya Manning kusikiliza ushuhuda kuhusu uhusika wa George Stinney katika mauaji hayo.

Baraza la wazee wa Mahakama lilijumuisha wanaume wawili ambao waliongoza wito wa kuuawa kwa George siku tano tu mapema.

Hakukuwa na ushahidi dhidi ya George, lakini naibu wa polisi wa eneo hilo, Henry Newman alisoma kile alichosema ni ‘ungamo’ alilodai kuwa lilisainiwa na George, kwamba aliwapiga wasichana hao wawili hadi kufa.

Uamuzi wa baraza la wazee wa Mahakama ukawa mmoja tu: George kuhukumiwa kifo.

Ingawa katika upelelezi wake walidai kuwa George alibaka kabla ya kuua, madai hayo hayakuletwa mahakamani. Labda ni kwa sababu ripoti ya madaktari ilisema “...Sehemu za siri za wasichana hao na kizinda zilikuwa shwari.” Chini ya wiki nne baadaye, Newman pamoja na mpelelezi Sidney Pratt, walisimulia hadithi tofauti sana walipotoa ushahidi dhidi ya George, wakati kesi ikiendelea.

Wakili McLeod alipeleka mashahidi wawili tu dhidi ya George na mmoja wa mashahidi hao ni Newman aliyedai kuwa George alikiri kuwaua wasichana hao.

Hakuna ushahidi mwingine alioutoa zaidi ya huo. Na ingawa kwenye upelelezi wake alisema George alikiri kuwabaka wasichana hao kabla ya kuwaua, akitoa ushahidi mahakamani hakutoa madai hayo.

Mahakama iliahirishwa kuanzia Aprili 24, 1944, ikiwa ni mwezi mmoja barabara tangu kufanyika kwa mauaji. Aliyeongoza jopo la majaji wa kuisikiliza kesi hiyo ni Jaji Philip Henry Stoll.

Kabla ya kesi kuanza, John Stinney, ambaye ni kaka yake George waliokamatwa siku moja na kuwekwa mahabusu, aliachiwa na polisi, lakini George aliendelea kubaki kizuizini.

Hakuruhusiwa kuwaona wazazi wake hadi baada ya kesi yake na kuhukumiwa.

Kulingana na taarifa iliyoandikwa kwa mkono na Newman, ambaye ndiye ofisa aliyemkamata na alikuwa ni naibu mkuu wa polisi wa Kaunti ya Clarendon, George alikiri kuwa alitumia kipande cha chuma kuwapiga wasichana hao.

Kufuatia kukamatwa kwa Stinney, baba yake alifukuzwa kazi katika kiwanda cha mbao cha eneo hilo na kama ilivyoelezwa katika toleo lililopita, familia ya Stinney ililazimika kuondoka mara moja kwenye makazi yao ikihofia usalama wao, hivyo hawakumuona tena kijana wao kabla ya kesi kuanza.

George hakuwa na msaada wowote wakati wote wa siku 81 akiwa mahabusu pamoja na siku za kesi. Alihojiwa peke yake, bila wazazi wake au wakili.

Mchunguzi wa afya ya akili, Emily Moorer wa Greenwood, South Carolina, aliona kuwa katika hukumu ya kifo ya George kulikuwa na ushahidi wa wazi wa ubaguzi wa rangi.

“Ikiwa mvulana huyo angekuwa mzungu hukumu ingekuwa kifungo cha maisha gerezani, kifungo cha muda mrefu katika kituo cha kurekebisha tabia au taasisi ya wahalifu wenye upungufu wa akili,” aliandika Greenwood.

Labda jambo la kushangaza zaidi ni kwamba mawakili wa George Stinney, yaonekana hawakufikiria kamwe kuhoji kuhusu kutokuwapo kwa damu kwenye mwili wa George.

Majeraha mabaya na makubwa ya Mary Emma Thames na Betty June Binnecker yangesababisha damu kumrukia muuaji na kumchafua.

Kama George Stinney ndiye alikuwa muuaji, wapelelezi wengine walisema ni lazima angekutwa na angalau doa la tone ya damu. Lakini hakukutwa na doa lolote mwilini na kwenye nguo zake.

Hata hivyo, nguo na viatu vya Stinney vyenye damu vilikuwa wapi? Je, kulikuwa na mashahidi waliomwona akirudi nyumbani baada ya mauaji hayo akiwa na damu mwilini au nguoni?

Haya ni maswali ambayo mawakili wa utetezi walipaswa kuuliza, lakini hawakuuliza.

Hisia za umma tayari zimemwona George ana hatia. Ilionekana kila mtu alijua kwamba muuaji ni George.

Lakini vipi ikiwa Mahakama ingemwona hana hatia? Au, namna gani ikiwa wangemwona kuwa na hatia, lakini wakapendekeza kubadili hukumu yake iwe kifungo cha maisha? Uvumi ulienea sana katika muda wa wiki mbili kabla ya kesi kuanza kwamba George akifika mahakamani angekamatwa na kuuawa.

Tetesi nyingine zilidai kuwa iwapo angeenda mahakamani na kukutwa hana hatia, au kukutwa na hatia lakini ikapendekeza hukumu ndogo kuliko kunyongwa, angeuawa kwa kupigwa risasi hapo hapo kwenye chumba cha Mahakama.

Uvumi ulienea sana kwamba bunduki zingeletwa mahakamani na wananchi. Kutokana na uvumi huo, ulinzi mkubwa zaidi uliongezwa mahakamani kiasi kwamba kulikuwa kunafanyika upekuzi usio wa kawaida mahakamani hapo siku ya kesi.

Kwa kuwa jamii ya eneo hilo ilikuwa imeshamhukumu George Stinney kifo kutokana na kile kilichoaminika kuwa yeye ndiye alikuwa muuaji wa wasichana wawili wazungu, jambo hilo liliishinikiza Mahakama kupitisha adhabu ya kifo kwa kijana huyo.

Na iwapo Mahakama ingetamka kuwa George hakuwa na hatia kama ilivyodhaniwa awali, wao walikuwa tayari kumhukumu kifo kwa kumuua.

Chuki dhidi yake ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba maofisa wa Serikali walilazimika kumhamisha kwa siri kutoka gereza moja kwenda jingine, lakini huko kulikuwa ni kuahirisha tu mambo. Hatimaye aliuawa.

Je, kesi iliendeshwaje?

Tukutane toleo lijalo.