Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maaskofu washusha nondo 12

Muktasari:

  • Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini wametoa salamu za Krismasi na mwaka mpya kwa Watanzania, zikiwa zimebeba ujumbe unaozungumzia masuala takriban 12 yanayoligusa Taifa.

Moshi/Mwanza. Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini wametoa salamu za Krismasi na mwaka mpya kwa Watanzania, zikiwa zimebeba ujumbe unaozungumzia masuala takriban 12 yanayoligusa Taifa.

Masuala hayo ambayo viongozi hao waliyataja walipozungumza na waandishi wa Mwananchi, ni pamoja na umuhimu wa maridhiano ya kisiasa na haja ya Katiba mpya.

Mambo mengine waliyoyagusia katika salamu hizo ni kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia, mabadiliko ya tabianchi, umoja, haki na amani, janga la Uviko-19, ajira kwa vijana, rushwa, upendeleo na kuibuka kwa utamaduni wa kusifiana.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, aligusia suala la maridhiano ya kisiasa yanayoendelea, akisema jambo hilo ni muhimu kwa ajili ya maelewano, amani na maendeleo ya nchi.

Itakumbukwa tangu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aachiwe huru baada ya kukaa mahabusu kwa miezi takribani minane, chama chake kimeingia katika mazungumzo na CCM ya kutafuta maridhiano.

Askofu Shoo alisema mwaka 2022 kuna mambo yaliyoshuhudiwa na Taifa, ikiwamo kuongezeka kwa vitendo vya ukatili.

“Tumeshuhudia kuongezeka kwa vitendo hivyo. Jambo hili si jema kwa jamii yetu. Mungu atuwezeshe tukatae na kupinga ukatili wa namna yoyote. Mwaka 2023 tuweke mkazo katika malezi na makuzi ya maadili kuanzia ngazi ya familia na taasisi zote.”

Alisema viongozi wa dini, wazazi, walimu waone wajibu wao na kuutimiza katika kumjenga na kumkuza katika maadili yenye hofu ya Mungu.

“Tumeshuhudia ukame usio wa kawaida na upungufu wa maji maeneo kadhaa ya nchi yetu. Hapa tunahitaji kuongeza jitihada za utunzaji wa mazingira, kutunza vyanzo vya maji, kuotesha miti na kuhifadhi maji nyakati za mvua,” alisisitiza.

Askofu Shoo aligusia pia suala la maridhiano linaloendelea nchini akisema; “Maridhiano na uelewano kati ya makundi mbalimbali ndani ya jamii yetu ni jambo la muhimu kwa amani na maendeleo ya nchi yetu.

“Hivyo tunaposherehekea sikukuu hizi Mungu atujalie kujenga demokrasia ya kweli ambayo itahakikisha umoja, maelewano, haki na amani vinatunzika kwa maendeleo ya nchi yetu.”

Askofu Shoo alisema jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali za kuleta maendeleo, zinastahili kupongezwa na kwa sababu Watanzania wanahitaji maendeleo endelevu sambamba na kumtanguliza Mungu na kumheshimu kabla ya mambo yote.

Hata hivyo, alisema mwaka 2022 Tanzania imeona baraka nyingi zikishuka, huku akisema hiyo ni kutokana na amani iliyotamalaki kwa Taifa na hivyo kila Mtanzania anapaswa kushukuru kwa hilo.

“Tumshukuru Mungu kwa huruma zake, ametuwezesha kulikabili na kustahimili madhila ya janga la Uviko-19 lililotutesa, kuchukua uhai wa ndugu zetu na kudhoofisha uchumi na mambo mengine kadha wa kadha.

“Ingawa ugonjwa huu haujaisha kabisa, kwa neema ya Mungu, madhara yake yamepungua kwa kiwango kikubwa. Tuzidi kumwomba Mungu na kuchukua tahadhari, ikiwemo kupata chanjo na kufuata maelekezo ya wataalamu,” alisema.


Shoo ataka shukrani


Askofu Shoo katika ujumbe wake mahsusi kwa ajili ya Sikukuu ya Krismasi alisema wakati Wakristo duniani kote na Watanzania wakisherehekea sikukuu hiyo, wanapaswa kumshukuru Mungu kwa upendo wake kwa wanadamu.

“Kristo aliye mfalme wa amani azaliwe kweli mioyoni mwetu. Furaha, upendo na amani itawale na kuonekana katika familia zetu na jamii yetu. Katika kusherehekea tutunze amani na utulivu, sio wakati wa kulewa na kugombana.

“Bali ni wakati wa kuonyesha upendo, furaha na amani, na kuwakirimu wengine, hasa wale wasiokuwa na chakula. Atukuzwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia,” alisema Askofu Shoo.


Askofu Niwemugizi

Katika salamu zake alizotoa kwa gazeti hili, Askofu Severine Niwemugizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, alishauri wote waliokasimiwa dhamana ya uongozi kuiga busara ya Mfalme Suleiman kwa kuomba hekima ya kuongoza watu kwa haki, usawa, upendo na utu.

Alisisitiza haki kwa wote kuwa ndiyo msingi mkuu wa amani, upendo na mshikamano katika jamii.

“Tutumie sikukuu hizi siyo kwa kula, kunywa na kufurahi, bali pia tuzitumie kutafakari upendo na neema ya Mungu kwetu, huku tukiishi kwa haki, usawa, upendo na utu kwa kila mmoja,” alisema Askofu Niwemugizi.


Askofu Mwamakula agusia Katiba, ajira


Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula alitaka mwaka 2023 uwe wa kudai Katiba mpya, huku akigusia pia suala la ukosefu wa ajira

“Tunasherekea Krismasi na kuingia mwaka mpya 2023 wakati Taifa letu likiwa linakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa ajira kwa vijana pengine kuliko kipindi chochote cha historia ya Taifa letu,” alisema kiongozi huyo ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian Duniani.

Aliongeza: “Idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu pamoja na taasisi nyingi za elimu ya juu, hawana ajira, jambo ambalo ni hatari sana kwa usalama wa raia, kwani jamii ambayo kundi kubwa la watu wake hawana ajira, haiwezi kuwa salama.

“Kwa muono wetu, tatizo la upungufu wa ajira Tanzania linasababishwa na Katiba ambayo haitoi fursa ya kutatua tatizo hilo. Viongozi (baadhi) wanapata au kupewa nafasi za uongozi kwa kigezo cha rushwa, upendeleo na kulipa fadhila.

“Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulitikisa mfumo wa utawala ambao haukuwa rafiki kwa maendeleo ya kiroho na kiuchumi. Mtu ambaye uchumi wake hauko sawa na mtu ambaye haki yake inafinywa hawezi kuzalisha vizuri.

“Kwa sababu hiyo, tunauasa umma kushiriki katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kuwa sehemu ya kudai katiba mpya. Krismasi hii itusaidie kuona umuhimu wa kuufanya mwaka 2023 kuwa ni mwaka wa Katiba mpya”.

Wakati askofu huyo akizungumzia suala la rushwa kwenye uongozi, Novemba 22, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Simiyu na kusimamisha uchaguzi wa wajumbe wa halmashauri kuu mikoa ya Arusha na Mbeya kwa tuhuma za rushwa.

Chongolo alisema uamuzi wa kufuta matokeo unaweza kuendelea katika maeneo yatakayobainika kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi. Alisema CCM haiko tayari kuona viongozi wanaingia madarakani kwa rushwa wala vitendo viovu.

Moja ya matukio ambayo yaliibua mijadala katika mitandao ya kijamii ni kipande cha video kilichorushwa kikiwaonyesha makada wa UVCCM wakilizunguka gari dogo wilayani Itilima, Mkoa wa Simiyu, ambako inadaiwa walikuwa wanachukua mlungula.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni alilieleza gazeti hili kwamba wanaendelea na uchunguzi na watakaobainika hatua zitachukuliwa.

Ripoti ya kikosi kazi iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 21, ilibainisha kwamba viongozi na taasisi mbalimbali walizungumzia suala la rushwa na kusema limekuwa tatizo kubwa linalovuruga demokrasia na iwapo itapunguzwa nchi itapiga hatua kidemokrasia.

Kutokana na maoni ya wadau kuhusu rushwa, mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala akisoma taarifa ya mapendekezo ya kikosi hicho, alisema sheria za uchaguzi zirekebishwe kuweka masharti, mgombea atakayethibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa aondolewe sifa ya kugombea katika uchaguzi wowote kwa miaka 10 mfululizo.


Askofu Bagonza alia na tabianchi

Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la KKKT, Dk Benson Bagonza alisema hali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira nchini, bado inaleta hofu miongoni mwa Watanzania akisema:

“Tukubali ukweli, hali si nzuri.Tupokee na kutumia dawa ili tupone. Yesu Kristo alikuja kwa ajili ya haya tunayoyaona. Tuache tabia ya kujiliwaza, kujisifu na kusifiana. Mabadiliko ya tabianchi yanatishia kutuangamiza sote bila ubaguzi,” alisema askofu Bagonza na kuongeza:

“Tubadili tabia zetu ili tabianchi nayo ibadilike. Tunaalikwa katika wajibu wetu wa kutunza mazingira. Badala ya kuombea mvua, tuombee mabadiliko ya tabia zetu ziache ubinafsi, ubabe na dhuluma zinazozalisha umasikini.”

Akizungumzia kuzaliwa kwa Yesu, Askofu Bagonza aliwataka viongozi na Watanzania kuacha kutumikia maono mafupi, bali waungane katika kuwajibishana ili kurejesha matumaini yaliyopotea.

Alisema tukio la kuzaliwa kwa Kristo miaka zaidi ya 2000 iliyopita, bado linafurahisha kila linapokumbukwa, akisema:

“Walioona na sisi tuliohadithiwa tunakuwa na furaha tunapokumbuka tukio hili. Jamii ya wakati huo ilijaa kukata tamaa, wafalme na makuhani walishindwa kurejesha matumaini. Manabii walitabiri lakini hawakuaminika, kila kulipokuwa utawala wa Warumi kulizidisha mateso kwa kuwatoza watu kodi nyingi.

“Yusuf na Mariam wakamleta duniani Yesu Kristo. Mimba ya aibu ikageuka mimba ya ukombozi. Aibu ikageuka utukufu na unyonge wa Yusuf na Mariam vikageuka kuwa msingi wa matumaini. Ukombozi wa kiroho na kimwili ukaingia duniani.’’


Walichosema Maaskofu Anglikana, KKMM

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Oscar Ulotu alisema kipindi hiki cha kuelekelea Krismasi, ni wakati mzuri kwa kuiombea nchi na viongozi wake ili iendelee kuwa na amani.

Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza, Zephania Ntunza aliwasihi viongozi waliokasimiwa madaraka kuyatumia kwa utu, haki na usawa wakitambua dhamana hiyo imetoka kwa Mungu.

“Viongozi wote watambue kundi walilopewa kuliongoza ni kundi la Mungu na waliongoze kwa mapenzi ya Mungu, maana wakitenda kinyume watakuwa wanamchukiza Mungu mwenyewe aliyewapa dhamana ya uongozi,” alisema.

Aliwataka Watanzania kutendeana mema ili kudumisha amani, upendo na mshikamano, huku akitaka njia ya majadiliano na maridhiano itumike kupata mwafaka penye mvutano au tofauti yoyote.

Askofu Mkuu wa KKAM, Ulotu alisema Krismasi ni tendo linalosherehekewa na watu wengi duniani na ni kipindi kitakatifu kwa Wakristo kinachowapa nafasi ya kumshangilia Yesu anayezaliwa kwa wokovu wao.

“Ni nafasi yetu Wakristo kujitathmini katika hili ambalo Yesu analifanya ndani yetu. Tujitathmini maisha yetu ya kila siku na uhusiano wetu na Mungu,” alisema.

“Yesu aliye mfariji wetu na mfalme wa amani atupe kusherehekea vyema sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya 2023.”


Akemea kujikweza

Askofu mstaafu wa Kanisa la Assemblies of God (TAG), Glorious Shoo alikemea watu kujikweza kuliko kujishusha.

“Krismasi ni wakati wa kukumbuka kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu. Kuna mambo mengi ya kujifunza katika sikukuu hii. Pamoja na kwamba alikuwa mbinguni alizaliwa katika banda la kulia ng’ombe,” alisema.

“Siku za leo tumejikuza kuliko kujishusha. Endapo Mungu amekubali na kukupa nafasi basi jishushe. Nenda chini endapo unataka kubakia juu,” alisisitiza askofu huyo.


Nyongeza na Sada Amir (Mwanza)