Machinga aeleza mabaunsa wa Sabaya walivyompora simu, Sh35,000 Sabaya (3)

What you need to know:

  • Tulisoma pia shahidi wa pili ambaye alikuwa msaidizi wa Saad, Numan Jasin (17) akiieleza mahakama jinsi ‘mabaunsa’ wa Sabaya walivyomshambulia Diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi, baada ya kufika dukani kwao kujua nini kilikuwa kikiendelea. Endelea…

Julai 23, 2021 shahidi wa tatu, Ramadhan Rashid, aliieleza mahakama kuwa Sabaya aliamuru apigwe, apekuliwe na kunyang’anywa simu na fedha alizokuwa nazo, Sh35,000.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa kati ya watu wote aliowakuta dukani (Shaahid Store), aliweza kumkariri Sabaya kwa kuwa ndiye aliyekuwa akitoa amri ya yeye kupigwa.

Rashid, aliyejitambulisha kama mfanyabiashara mdogo, maarufu kama machinga, alidai mahakamani hapo kuwa alinyang’anywa vitu hivyo katika duka hilo alilokuwa ameenda kununua bidhaa.

Siku hiyo Jamhuri iliwakilishwa na mawakili Tumaini Kweka, Abdallah Chavula na Baraka Mgaya.

Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na mawakili Dancan Oola, Mosses Mahuna, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka, Fridolin Bwemelo na Jeston Jastin.

Akiongozwa na Mgaya, shahidi huyo aliieleza mahakama siku ya tukio Februari 9, 2021 alipata mteja aliyekuwa akitaka kununua chandarua, hivyo akaenda dukani hapo kwa ajili ya kununua lakini alipofika alikuta mageti ya duka hilo yamefungwa.

Alieleza kuwa kutokana na wahusika dukani hapo kusali mara tano kwa siku na wakati wa kusali hurudishia mageti, alinyanyua geti na kuingia ndani ambapo alipochukua chandarua. Alishangaa anafuatwa na watu wawili na kusikia amri ikisema ’mtoe lock.’

“Nikaanza kupigwa vibao vya masikio, nikasema Mungu mkubwa, niliendelea kupigwa na kwa muda huo nilipekuliwa, nilichukuliwa pesa Sh35,000 na simu yangu na karatasi iliyokuwa nimeandika vitu vya kuchukua,” alidai shahidi huyo.

Shahidi huyo alidai baada ya kuchukuliwa simu yake ya Tecno Pop 1, aliamriwa kulala chini kifudifudi huku mabishano yakiendelea juu ya duka hilo kuuza bidhaa bila kutoa risiti na kuwa wanabadili Dola za Marekani.

Aliendelea kueleza mahakama kuwa baada ya muda aliingia mtu mmoja dukani hapo (Bakari Msangi-Diwani wa CCM, Sombetini) ambaye alidai kuwa Sabaya alitoa amri Msangi atolewe lock (apigwe), kisha kijana huyo akaambiwa aondoke dukani humo.

“Nilikuwa natoka, nilipofika mlangoni nikakumbuka nyuma nimeacha hela na simu. Nikamwambia naomba simu na hela yangu kwa sababu umeshaniruhusu niondoke. Yule jamaa akajibu ‘huyu bado ana wenge mtoe lock.’ Nikachuchumaa, nikapigwa moja kubwa, nikaulizwa bado unadai? Nikakimbia zangu, hela na simu nikaacha hapo hapo.” (wasikilizaji wanaangua kicheko)

Akihojiwa na wakili Mahuna, shahidi huyo alidai hakumbuki laini za mitandao ya simu za Airtel na Vodacom alinunua lini na kuwa hakuwahi kwenda kuripoti polisi kwani alikuwa na woga na wala hafahamu IMEI (namba ya utambulisho) ya simu yake.

Akihojiwa na Wakili Oola, shahidi huyo alisema licha ya kukuta kundi la watu dukani hapo anayemkumbuka ni Sabaya peke yake ambaye alimtambua mahakamani kwa kumshika bega.

Baada ya Rashid kutoa ushahidi wake, mahakama ilianza kumsikiliza shahidi wa nne, Saad Hajirin (32).

Akiongozwa na wakili Chavula kutoa ushahidi, Hajirin ambaye ni ndugu wa shahidi wa kwanza, Mohamed Saad, alidai kuwa siku ya tukio alifika dukani kwa kaka yake (Mohamed) aliyemwomba aende kujua kuna tatizo gani baada ya kupigiwa simu kuwa kuna maofisa wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wanamhitaji.

Alidai kuwa awali alipigiwa simu kuwa kuna wateja wanataka kununua mapazia ya jumla dukani hapo, hivyo, kaka yake alimwomba akamsaidie lakini kabla hajaenda alipigiwa tena na kaka yake aliyemweleza kuwa si wateja ni maofisa wa TRA na alipofika alishangaa kumkuta Sabaya na wenzake.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa alipoingia dukani hapo alikuta watu ambao hawakumbiki idadi yao wakiwa wamelazwa chini huku wakiwa wamefungwa pingu na wengine bila pingu, akiwemo mmoja wa wauzaji dukani hapo.

Shahidi huyo aliendelea kueleza kuwa wakati Sabaya anaendelea kuwahoji aliingia Msangi ambaye alimsalimia Sabaya mara kadhaa bila kuitikiwa na badala yake alihoji amefuata nini dukani hapo.


Meya Moshi atajwa

Akiendelea kutoa ushahidi Julai 26, 2021, shahidi huyo alieleza mahakama kuwa wakati Msangi anapigwa alimwomba Sabaya amsamehe kwani yeye ni ndugu wa rafiki yake Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu Juma.

Shahidi huyo alidai diwani huyo alipigwa sana na ‘mabaunsa’ wa Sabaya na kuwa kutokana na kipigo kikali alimwomba Sabaya amsamehe na kumshika miguu huku akidai mke wake ni mgonjwa.

Shahidi huyo aliieleza kuwa mbali na kupigwa kwa amri ya Sabaya, DC huyo na kundi lake walikuwa na bastola ambapo kuna wakati alikuwa ameishika Sabaya na wakati mwingine walikuwa wameishika mabaunsa wake.

Alieleza kuwa awali Msangi alimsalimia Sabaya mara mbili lakini hakuitika na baada ya muda Sabaya alimjibu kwa kumuuliza, ‘hujui cheo changu, niite General.’

Alidai baada ya maelezo hayo Sabaya alimwambia: “Huyu dada ameiba Dola 70,000 Moshi na hawa Waarabu ndiyo anashirikiana nao.”

Shahidi alidai Sabaya alikwenda kufungua pochi ya yule dada na kusema amekuwa akija kubadili fedha dukani hapo. “Mnashirikishana na majambazi, wahujumu uchumi,” alisema Sabaya baada ya kukuta dola 100 katika pochi ya yele dada.

Alieleza kuwa Sabaya aliamuru mabaunsa wamtoe lock Msangi (wampige) na kuanza kumpiga makofi usoni na masikioni. “Walisimama kwa nyuma wakampigisha magoti na kabla ya hapo walimpekua kwa amri ya Sabaya na kuchukua simu zake na pochi,” alidai.

“Baada ya muda niliingizwa katika stoo ambapo yanahifadhiwa mapazia, Sabaya akaamrisha nitolewe lock kama watu wengine, akaniuliza ‘inatosha? Nikamjibu ‘inatosha mheshimiwa.’ Akasema ‘niite general. ’Nikamwita hivyo kisha akatoka na baunsa mmoja nikabaki na mmoja,”

Shahidi huyo aliendelea kueleza kuwa baunsa aliyebaki naye alimweleza kuwa kama ana Sh70 milioni nimweleze ili aongee na Sabaya yaishe.

“Nikamwambia tuombe Mungu yaishe ila kuhusu hiyo Sh 70 milioni mimi binafsi nina madeni tu labda niendelee kuwasiliana na wanayemtafuta (Mohamed).

Shahidi huyo pia alimtambua na kumgusa bega aliyekuwa msaidizi wa Sabaya, Sylvester Nyegu aliyedaiwa kuondoka na mfuko wenye nyaraka mbalimbali za duka hilo ikiwemo mashine mbili za EFD.

Alidai zilipita zaidi ya saa nne tangu afike katika duka hilo hadi muda walioruhusiwa kuondoka na kwamba baada ya kumaliza kufunga duka hilo alimfuata Sabaya aliyekuwa amesimama kwenye mkokotoni wa dagaa na kumuomba amnunulie ndizi kwani alikuwa amefunga.

Alimalizia ushahidi wake kwa kufafanua kuwa baada ya kufunga duka hilo walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi na walipofika Sabaya aliwaeleza Polisi kuwa wao walikuwa watuhumiwa wake wa uhujumu uchumi na kuamuru wachukuliwe wachukuliwe maelezo na Inspekta Gwakisa.

Alisema baada ya kuchukuliwa maelezo hayo walipewa dhamana na askari mmoja aliambiwa na Gwakisa awape lifti hadi eneo la Bondeni.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Moses Mahuna, shahidi huyo alidai licha ya kukaa na simu yake katika kachumba kadogo dukani hapo kwa muda wa nusu saa hakuweza kupiga simu polisi .Alidai kuwa kutokana na hofu aliyokuwa nayo hakuweza kupiga simu kuomba msaada polisi.

Itaendelea kesho

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.