Machinga Iringa wagomea maeneo mapya ya Mlandege
Baadhi ya vibanda katika eneo la Mlandege mkoani Iringa vikiendelea kufanyiwa matengenezo.
Muktasari:
- Wakati ikiwa Machi 1, 2023 ikiwa imepangwa kwa wamachinga kuanza kutumia eneo jipya la Soko la Mlandege Manispaa ya Iringa, wafanyabishara hao wamegoma kupokea maeneo hayo wakilalamikia uchache wa vibanda na kutokamilika kwa miundombinu.
Iringa. Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa umeahirisha kugawa vibanda vya wafanyabiashara ndogo maarufu kwa jina la wamachinga katika eneo la Mlandege.
Awali, wafanyabishara hao walitakiwa kuwa wamehamia kwenye eneo hilo Machi 1, 2023 jambo ambalo limeshindikana baada ya kugoma kuhamia kutokana na uchache wa vibanda na kutokamilika kwa miundombinu.
Leo, Machi 3, 2023 Mwananchi imeshuhudia uongozi wa wafanyabiashara hao ukilazimika kuketi meza moja na uongozi wa halmashauri hiyo kujadili suala hilo baada ya wafanyabishara hao kugoma kukabidhiwa maeneo hayo.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Iringa, Yahaya wanachofanya kuwasikiliza wamachinga hao na kutimiza matakwa yao.
“Tukikaa kama hivi mtu akileta mawazo tunasikilizana, tunabeba mawazo ya wamachinga na kuyafanyia kazi, kilichotakiwa kufanyika leo tunasitisha ili uwekwe utaratibu mzuri wa kugawiwa maeneo haya ili hii keki tuipate wote,” alisema Mwenyekiti.
Kwa upande wake, Katibu wa Machinga Mkoani Iringa, Joseph Kilyenyi maarufu kama Mwanakijiji amewaomba wafanyabishara hao kuwa wasikivu.
“Tutakuwa na hatua kubwa kwa ajili ya kugawa eneo hili, kuna wakati nyie mnapokuwepo na tukiwa na nidhamu ni rahisi kusaidiwa na kupewa haki yetu,” alisema Kilywenyi.
Nao baadhi ya wafanyabishara wamesema hatua ya kuahirishwa kupewa maeneo hayo imewafurahisha ili kuwepo kwa usawa wa hadhi za vibanda.
Mmoja wa Machinga hao alisema waligoma kupokea maeneo hayo kwa sababu hakukuwa na miundombinu kama maji sambamba ya uchache wa vibanda.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kuzungumza na uongozi wa manispaa baada ya kikao hicho ili kujua nini kinaendelea baada ya kuzuiwa kuingia ndani.