Machinga waanza kuhamishwa

Machinga waanza kuhamishwa

Muktasari:

  • Hatua za Serikali kuanza kuwaondoa wamachinga pembezoni mwa barabara zimeanza kuchukuliwa jijini Dar es Salaam, baada ya vibanda vya baadhi yao kuvunjwa katika eneo la Vingunguti Wilaya ya Ilala.


Dar es Salaam. Hatua za Serikali kuanza kuwaondoa wamachinga pembezoni mwa barabara zimeanza kuchukuliwa jijini Dar es Salaam, baada ya vibanda vya baadhi yao kuvunjwa katika eneo la Vingunguti Wilaya ya Ilala.

Wamachinga wa eneo hilo jana walijikuta katika sintofahamu baada ya kukuta asubuhi vibanda wanavyofanyia shughuli zao vimebomolewa.

Kubomolewa kwa vibanda hivyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan la kuwataka wakuu wa mikoa kuwapanga wamachinga na kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri alisema wafanyabiashara hao walitakiwa waondoke kwa sababu walipewa mwezi mmoja.

“Matangazo ya mkuu wa mkoa hamkuyasikia... waliambiwa wote waliokuwapo katika maeneo matano yaliyotajwa wanatakiwa kuondoka,” alisema Shauri.

Alisema wafanyabiashara hao wanatakiwa kwenda maeneo ya Machinga Complex, huku akibainisha kuwa tayari wapo baadhi ya wenzao ambao wameondoka.

“Wanatakiwa waondoke wenyewe. Kama kuna bidhaa ndani, wanatakiwa kuondoa wenyewe, ambavyo havina ndio hivyo vinaondolewa,” alisema Shauri.

Wakati Mkurugenzi akiyasema hayo, wafanyabishara walilalamika kupoteza bidhaa zao wakati wa ubomoaji huo uliofanyika usiku.

Hamna Karne alisema anahisi kuchanganyikiwa kwa sababu amekuwa akihudumia familia na kusomesha kupitia kazi hiyo.

“Jana kama saa sita usiku yalikuja magari kama matano na mgambo, wamechukua mali zetu na kuondoka nazo, walikuwa wanachukua na kuondoka,” alisema Karne.

Alisema wao walipewa taarifa kuwa mwisho wa kuwa eneo hilo ni Oktoba mosi, lakini sasa hawaamini kilichotokea.

Naye Rajab Shomari pia mfanyabiashara wa Vingunguti alisema kwa mujibu wa tangazo, waliambiwa watapangwa Oktoba mosi na hivyo hawajui kilichotokea kama ndiyo njia ya kupangwa au kufukuzwa. “Hatukukataa kuwa tupangwe au tupelekwe sehemu nyingine, lakini kitendo cha kuja kutuvunjia saa sita usiku si haki,” alisema Shomari.

Zena Shaibu alisema katika shughuli hiyo baadhi ya vitu vimeibwa huku wengine wakiwa na mikopo.

“Bora tungeambiwa tutoe vitu vyetu vibanda vibomolewe, si kubomolewa na vitu vikiwa ndani,” alisema Zena.

Hawa Khamis ambaye ni muuza mihogo aliiomba Serikali iwasaidie ili wajue wataishi vipi, kwani yeye ndo mama na ndiyo baba wa familia.

Kwa upande wake, Ally Tembo alisema kitendo hicho si cha kiungwana kwa wananchi wa hali ya chini huku akibainisha kuwa ni tofauti na walivyoambiwa.

Tuliambiwa tumepewa mwezi mmoja mzima tujiandae kuhama, sasa mchana wanatoa taarifa usiku wamekuja kuvunja, bora wangesema mchana toeni vitu vyenu usiku tunakuja kuvunja,” alisema Tembo. Alisema baadhi yao wana mikopo, wanasomesha, wanalipa kodi, wanaenda wapi.

“Wengine tuna vitambulisho vya Sh20,000 maana yake tunaruhusiwa kuwa na vitambulisho lakini mnatuvunjia, tunaenda wapi,” alisema Tembo.

Miongoni mwa waliolalamika ni Tanga Shilali, aliyesema amepoteza vitu vingi katika bomoabomoa hiyo na sasa hajui cha kufanya.

Mfanyabiashara mwingine alisema agizo la Rais lilitaka sehemu zitafutwe ili wafanyabiashara wapelekwe lakini kilichotokea si uungwana.

Wakati wao wakilia, maeneo mengine ya jiji bado ni vicheko kwani wafanyabiashara wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Licha ya kuwa halmashauri imeweka mabango kuzuia biashara kufanyika maeneo hayo, lakini watu hawavijali.

Maeneo kama Manzese, Halmashauri ya manispaa Kinondoni imeweka vibao kuzuia biashara kufanyika karibu na hifadhi ya barabara, lakini watu wamepanga bidhaa zao hadi barabarani bila kujali. Huenda Vingunguti na barabara ya kuelekea Uwanja wa ndege ikawa mfano kwao, kama msamiati unaosema mwenzako akinyolewa na wewe tia maji.

Imeandikwa na Aurea Simtowe, Mariam Mbwana na Bakari Kiango.