Madai ya katiba mpya yatawala vinywa vya wapinzani mwanzo wa 2021

Madai ya katiba mpya yatawala vinywa vya wapinzani mwanzo wa 2021

Muktasari:

  • Mwaka mpya umeanza kwa vyama vya upinzani nchini kudai katiba mpya ya wananchi huku vikieleza kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kutibu majeraha yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka jana.

Mwaka mpya umeanza kwa vyama vya upinzani nchini kudai katiba mpya ya wananchi huku vikieleza kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kutibu majeraha yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka jana.

Mbio hizo za kudai katiba mpya zinakwenda sambamba na uhitaji wao wa Tume huru ya uchaguzi wanayosema itatoa nafasi sawa kwa vyama vyote kushindana kwa haki katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Licha ya changamoto nyingi wanazoziona mbele yao, bado wana matumaini ya kufanikisha azma yao wakiona ndiyo njia pekee ya kuleta usawa katika siasa za Tanzania ambazo zinawaacha nyuma.

Tangu mwaka umeanza, vyama hivyo kwa nyakati tofauti, vimetoa matamko ya kudai katiba mpya kama hitaji la lazima litakalosaidia kuondoa sintofahamu iliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi.

Siyo mara ya kwanza kwa vyama hivyo, kudai Katiba mpya, vuguvugu hilo lilianza mwaka 2011 ambapo Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alisikiliza kilio hicho na kuanzisha rasmi mchakato wa katiba mpya kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya mwenyekiti, Jaji mstaafu, Joseph Warioba.

Tume hiyo ilizunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wadau mbalimbali na kuandika rasimu ya kwanza ya Katiba na baadaye rasimu ya pili ambayo ilikwenda kujadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba (BMK), mpaka kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa mwaka 2015.

Katiba Inayopendekezwa ilitakiwa kupigiwa kura ya maoni na wananchi, hata hivyo, haikuwezekana kwa sababu wakati huo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ilikuwa ikifanya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Tangu wakati huo, mchakato wa kupata katiba mpya umekwama licha ya kilio cha wadau mbalimbali wa masuala ya siasa kushinikiza kurudiwa kwa mchakato huo kuanzia kwenye rasimu ya pili ya Katiba.

Mwaka huu umeanza kwa vyama vya upinzani kuibeba ajenda hiyo kama hitaji la lazima kutokana na kile wanachoeleza kuwa ni majeraha yaliyotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Juzi, mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema hali ya siasa nchini siyo shwari kutokana na uchaguzi huo kuacha majeraha na kuondoa baadhi ya Watanzania. Hivyo, ili amani na furaha iwepo lazima katiba mpya ipatikane.

“Ili tutoke huku tunahitaji katiba mpya na hiyo ni lazima kwa Watanzania ili tuwe na furaha. Katiba mpya itatupa Tume huru ya uchaguzi, kwa kuwa yote yaliyotokea kwenye uchaguzi ni giza nene na kunapoibuka giza nene tujue karibu una pambazuka,” alisema Mbatia.

Katika salamu zake za mwaka mpya, Januari 4, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema mwaka 2021 utakuwa wa kudai Katiba mpya kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kutibu majeraha ambayo Watanzania wanapitia katika nyanja tofauti za maisha.

Chama cha Wananchi (CUF), nacho kimetangaza kutoshiriki uchaguzi wowote mpaka pale katiba mpya itakapopatikana. Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba alitangaza msimamo huo Novemba 2, 2020 baada ya matokeo kutangazwa.

Akizungumza na Mwananchi wiki hii kuhusu msimamo wa chama chake, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema kwa jinsi uchaguzi wa mwaka jana ulivyofanyika, hauna hadhi ya kuitwa uchaguzi huru, hivyo, mabadiliko makubwa yanahitajika.

Alisema pengine wapinzani hawajashughulikia kiini cha tatizo ambacho ni kukoekana kwa Tume huru ya uchaguzi pamoja na katiba mpya aliyosema itakwenda kuongoza mwelekeo wa maisha ya Watanzania hasa wakati wa uchaguzi.

“Changamoto ni namna gani Tume huru na katiba mpya vitapatikana katika mazingira tuliyonayo. Tuko kwenye tafakari kutafuta namna bora ya kuhakikisha mambo hayo yanapatikana, tukikamilisha tutatoa taarifa,” alisema Shaibu.

Katibu mkuu huyo alisema anaviona vikwazo viwili katika kuhakikisha katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi vinapatikana.

Mosi, anasema mfumo wa sasa unatoa nafasi kwa chama tawala cha Mapinduzi, hivyo si rahisi kukubali mabadiliko.

Pili, utawala wa sasa umeweka wazi kwamba katiba mpya siyo kipaumbele.

“Tuna wajibu wa kuisukuma CCM na serikali ya awamu ya tano ili waone hilo ni takwa la wananchi wenyewe, siyo suala la mtu au chama kimoja,” anasema Shaibu alipohojiwa na Mwananchi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alipoulizwa juu ya kilio hicho cha wapinzani, alisema uhitaji wa katiba mpya upo tangu miaka 1990 baada ya Tume ya Jaji Nyalali kupendekeza katiba mpya ambayo itaendana na mfumo wa vyama vingi.

Anasema kipengele hicho hakijawahi kutekelezwa licha ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi mpaka ilipofika mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete aliporidhia mchakato wa kuandika katiba mpya.

“Haya madai ya katiba mpya ni ya muhimu kwa sababu iliyopo ni ya chama kimoja, iliandikwa mwaka 1977. Mapendekezo yangu ni turudi kwenye rasimu ya Warioba, iboreshwe tu lakini iwe ndiyo msingi,” anasema Profesa Mpangala.