Madaktari waonya matumizi holela ya dawa za panadol

Madaktari waonya matumizi holela ya dawa za panadol

Muktasari:

  • Madaktari nchini wameonya kukithiri kwa matumizi holela ya dawa za panadol wakieleza kuwa yanaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa mtumiaji.

Dar es Salaam. Madaktari nchini wameonya kukithiri kwa matumizi holela ya dawa za panadol wakieleza kuwa yanaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa mtumiaji.

Wataalamu hao wameleeza kuwa utumiaji uliokithiri wa dawa hizo na kuzidisha kiwango ambacho mtu anatakiwa kutumiwa kwa siku pale anapokuwa na maumivu inaweza kumsababishia athari tano mwilini ikiwemo maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kizunguzungu, rangi ya manjano kwenye macho na kuharibu ini.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, watu wengi wamekuwa na tabia ya kutumia dawa hizo bila kufuata maelekezo ya daktari wakiamini hazina madhara zaidi ya kuondoa maumivu.

Dawa hizi zimekuwa kimbilio kutokana na kupatikana kwa urahisi kwenye maduka ya dawa hadi maduka ya kawaida ya mitaani na zinauzwa kwa gharama nafuu ikilinganishwa na dawa zingine.


Kwanini wanakimbilia panadol?

Gloria Ernest, mfanyabiashara wa Kariakoo alisema dawa hizo zimekuwa mkombozi wake pindi anapopata maumivu, kwani ana mwaka wa tatu hajakwenda hospitali kwa kuwa kila anapohisi hali tofauti anameza dawa hizo.

Alichokisema Gloria ni tabia ya wengi ya kutopenda kwenda hospitali na badala yake kukimbilia dawa za kupunguza maumivu na sio kutibu tatizo husika.

Benson Mkinga, ambaye ni mmiliki wa duka la dawa lililpo Tabata Segerea, alisema panado ni dawa zinazoongoza kununuliwa kwa kile alichodai kuwa huenda shughuli za kila siku zinawafanya watu kupata maumivu.

“Sina idadi kamili kwa siku zinauzwa ngapi, ila ni dawa zinazonunuliwa zaidi, inawezekana mfumo wa maisha unawafanya watu kupata maumivu au pia gharama yake ni nafuu. Mwingine unaweza kumuuliza kwanini usiende hospitali anakwambia panadol huwa zinamsaidia,” alisema Mkinga.

Watu wengi kukosa bima ya afya huenda ikawa sababu nyingine ya kushindwa kwenda kupata matibabu hospitali na kuishia kutumia dawa za kutuliza maumivu.


Nini athari

Kwa mujibu wa Dk Hamis Mkindi wa hospitali ya Bugando, panadol ni dawa zinazotakiwa kutumika kutuliza maumivu, lakini haina uwezo wa kutibu au kuondoa maumivu hayo moja kwa moja.

Dk Mkindi alieleza kuwa ni sawa kwa dawa hizo kupatikana kwa urahisi kwa kuwa zinatumika kumpa mtu nafuu ya muda mfupi, ila ni muhimu afuate ushauri wa kitaalamu kutoka kwa daktari.

“Kazi ya panadol ni kutuliza maumivu ya mwili yasiyo makali sana kama kichwa, viungo na misuli. Kutuliza homa, kupanda kwa joto la mwili kutokana na magonjwa mbalimbali. Ukitaka kutibu lazima uende hospitali uandikiwe dawa na daktari.

“Kila unapotumia hii dawa upo uwezekano wa kuzidisha sumu yake mwilini. Aidha kwa kunywa dozi kupita kiwango kinachotakiwa au kujikuta anakunywa dawa hii pamoja na dawa nyingine ambayo nayo ndani yake ina paracetamol, hivyo kujikuta katika kiwango kilichozidi,” alisema Dk Mkindi.


Panadol zinatakiwa kutumikaje?

Dk Mkindi alifafanua, “Kwa siku moja usitumie zaidi ya gramu 2.6 kwa mtoto chini ya miaka 12, na gramu nne kwa mtu mzima.

“Gramu nne ni sawa na vidonge nane kwa maana ya vidonge viwili kila baada ya saa sita na hayo ndio matumizi makubwa zaidi ya kutumia dawa hizi kwa mtu mzima. Ukiona homa au maumivu yanaendelea zaidi ya siku tatu baada ya kuzitumia ni vema kwenda hospitali.”

Mtaalamu huyo alieleza kuwa endapo dawa hiyo itatumika kwa muda mrefu na kwa kiwango zaidi ya kinachoshauriwa, upo uwezekano wa kutokea madhara kama tumbo kuuma, kichefuchefu, kizunguzungu na manjano kwenye macho.

Hatari zaidi ni kwamba dawa hizo zikitumika zaidi ya muda ulioshauriwa au kumeza nyingi kwa pamoja huleta madhara kwenye ini na huenda ikasababisha kiungo hicho muhimu kushindwa kufanya kazi.

Akizungumzia hilo, daktari mbobezi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Swalehe Pazi alisema asilimia 90 ya panadol anayotumia mtu inapita kwenye ini, ikiwa kiwango kitazidi kiungo hicho huelemewa na kushindwa kuitoa kwa utaratibu, hali inayosababisha mrundikano wa sumu ambao huaribu chembe hai na kusababisha mtu kupata manjano na hatimaye ini kushindwa kufanya kazi.

Mtaalamu huyo alikwenda mbele zaidi na kufafanua athari za dawa hizi kwenye ini huwakuta zaidi watumiaji wa pombe, wazee, watu wenye magonjwa ya ini yanayotokana na sababu nyingine na hata watoto wadogo.

“Pombe inapunguza uwezo wa ini kufanya kazi vizuri. Ikiwa utatumia panadol katika kiwango kisichoshauriwa, kuna uwezekano mkubwa kupata tatizo la ini, hivyo watumiaji wa pombe wanapaswa kufuata ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa hizo kinyume na hapo unaweza kuharibu ini lako.

“Watu wenye magonjwa ya ini tangu zamani kwa sababu zingine, ndiyo maana hawa dawa zao za maumivu huwa zinatolewa kwa uangalifu na haishairiwi watumie panadol kwani ni ngumu kujua ni kiwango gani kinaweza kuletea madhara kwao,” alisema Dk Pazi.

Pia aligusia watu wanaotumia dawa za kienyeji, akieleza kuwa baadhi ya mitishamba ina uwezo wa kuharibu ini na endapo paracetamol itaongezwa kuna uwezekano mkubwa wa kuleta athari kwenye ini.

Hata hivyo, mtaalamu huyo amewatoa wasiwasi watumiaji wa dawa hizo akisema, “Mtu ambaye amekuwa akitumia paracetamol kwa muda mrefu kwa kiwango kilichotakiwa hana sababu ya kuwa na wasiwasi, ila ikiwa umetumia kiwango kikubwa bila ya ushauri na una dalili ya manjano kwenye macho usidharau hali hiyo muone daktari kwa uchunguzi zaidi.”

Akizungumzia hilo, Meneja wa Uhusiano wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Gaudensia Simwanza alisema, “Panadol ipo kwenye kundi la dawa ambazo haihitaji cheti cha daktari, zimeruhusiwa kutumiwa na mtu pale anaposikia maumivu ila ni muhimu azingatie maelekezo.

“Ingawa panadol ipo kwenye kundi la dawa ambazo hazihitaji cheti cha dakari, haimaanishi mtu atumie bila ushauri wa daktari. ni muhimu kuzingatia maelekezo kabla ya matumizi,” alisema.

Kwa maoni na ushauri kuhusu habari hii, tuandikie kupitia 0658 376 444