MaDED 85 katika rada za Rais Samia

Thursday August 04 2022
New Content Item (2)

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa akitoa taarifa juu ya utekelezaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri 148 ya mwaka 2021 hadi 2022. Picha na Michael Matemanga

By Juma Issihaka

Dar es Salaam. Ni kama zimejiweka kwenye rada ya Rais Samia Suluhu Hassan. Hii ni baada ya halmashauri 85 nchini kushindwa kufikia asilimia 100 kwa makusanyo ya mapato, kiwango ambacho zilijiwekea kukusanya katika mwaka wa fedha 2021/22.

Halmashauri hizo zimejikuta katika hali hiyo, siku moja baada ya Rais Samia kuweka ukusanyaji wa mapato kuwa miongoni vipaumbele vya watendaji hao, alipowaapisha wakuu wa mikoa na watendaji wengine aliowateua hivi karibuni.

“Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ndiyo mtumiaji mkubwa wa fedha zinazokusanywa, lakini ukiangalia kinachotoka Tamisemi kuja huku ni kidogo mno. Waziri (Bashungwa) amesema mmevuka viwango vya ukusanyaji, aliponipa hiyo taarifa nikamwambia inabidi kupitia upya viwango mnavyojipangia,” alisema Rais Samia.

Akisisitiza hilo, alisema “nina hakika mnaweza kukusanya nyingi zaidi ya hizo, viwango mlivyojipangia ni vidogo mno, kwa kuangalia mazoea ya nyuma, lakini tukipanga viwango vingine kwa mujibu wa uwezo wa maeneo yetu, hiyo fedha inakusanyika,” alisema.

“Kwa hiyo nihimize sana ukusanyaji wa mapato, lakini pia kufanya mapitio ya viwango tunavyojiwekea vya ukusanyaji wa mapato,” alisema.

Akisisitiza hoja yake, Rais Samia alitolea mfano wilaya Malinyi iliyokuwa na mapato kidogo, lakini akasema alipelekwa mkuu wa mkoa mpya, mkuu wa wilaya mpya na viongozi wengine ili kuongeza mapato na ikafanikiwa.

Advertisement

“Halmashauri ile imekusanya mapato na kusaidia ujenzi wa hospitali ya wilaya, sasa kama Malinyi imeweza hakuna mwingine atakayeshindwa,” alisema Rais Samia.

Mbali na mapato, vigezo vingine vinavyotumika kupima utendaji wa halmashauri kwa mujibu wa Tamisemi ni matumizi ya mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo, utoaji mikopo ya asilimia 10, usimamizi wa urejeshaji wa mikopo hiyo na matumizi ya fedha za marejesho.


Hali ya mapato

Juzi, Waziri wa Tamisemi, Innocent Bashungwa alitoa taarifa ya makusanyo ya ndani kwa mwaka wa fedha 2021/22, akisema halmashauri 85 zimeshindwa kukusanya kadiri zilivyopanga.

Kati ya halmashauri hizo zisizofikia lengo la makusanyo, alisema 78 zimekusanya kwa asilimia 80 hadi 99, huku nyingine saba zikikusanya kati ya asilimia 58 hadi 79.

Hata hivyo, Bashungwa alisema halmashauri 100 ndizo zilizokusanya kwa asilimia 100 na zaidi, akifafanua kuwa zilizofikia mafanikio hayo zimeongezeka kutoka 57 za mwaka wa fedha 2020/21.

Katika hatua nyingine, licha ya baadhi ya halmashauri kutofikia malengo, Waziri huyo alisema makusanyo ya jumla ya halmashauri katika mwaka huo wa fedha, yamefikia asilimia 103, kiwango ambacho alisema hakikuwahi kufikiwa kwa miaka 10.

“Kwa mwaka wa fedha 2021/22, Sh888.7 bilioni zimekusanywa, sawa na asilimia 103 ya makisio yaliyokuwa Sh863.9 bilioni,” alisema.

Waziri huyo alitoa sababu kuu moja ya mapato hayo kupaa kuwa ni kuongezeka kwa vyanzo vya makusanyo kwa kila halmashauri.


Nani kapata nini

Halmashauri ya Kibaha, alisema imekuwa kinara kwa kigezo cha malengo ya makusanyo hayo, ikikusanya asilimia 247, ikifuatiwa na Mlele asilimia 185 na Morogoro iliyokusanya asilimia 158.

“Ongezeko la makusanyo katika wilaya ya Kibaha limetokana na mauzo ya eneo la uwekezaji ambalo halikuwa sehemu ya bajeti ya halmashauri hiyo, huku wilaya ya Mlele yalitokana na kushamiri kwa shughuli za kilimo na uwindaji baada ya kukamilika kwa barabara ya Tabora hadi Mpanda,” alisema.

Katika kundi hilo, Halmashari ya wilaya ya Bumbuli imeshika mkia kwa kukusanya asilimia 58, ikifuatiwa na Korogwe asilimia 67 na Bunda asilimia 70.

“Kwa kigezo cha wingi wa mapato Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongoza kwa kukusanya Sh75.3 bilioni, Kinondoni Sh47.3 bilioni na Dodoma Sh45.1 bilioni, huku zilizoshika mkia kwa upande huo ni Bumbuli Sh599.7 milioni, Kigoma Sh692.1 milioni, Madaba Sh792.3 milioni na Buhigwe Sh880.2 milioni,” alisema.


Pwani kidedea

Uchambuzi wa mapato hayo kimkoa, alifafanua kuwa Mkoa wa Pwani unaongoza ukikusanya asilimia 118, ukifuatiwa na Manyara asilimia 114, Katavi asilimia 112 na Songwe asilimia 111.

Kama ilivyokuwa mwaka jana, Mkoa wa Lindi umeshika mkia kwa mikoa ukusanya asilimia 87 ya makisio yake, ukifuatiwa na Mtwara na Geita ambayo kila mmoja umekusanya asilimia 93.

“Pamoja na kushika mkia, Lindi imeongeza makusanyo kutoka asilimia 78 mwaka 2020/21 hadi asilimia 87 mwaka 2021/22,” alisema.


Kuhusu matumizi

Katika kutekeleza miradi ya maendeleo, Bashungwa alisema halmashauri zimetumia Sh297.7 bilioni kwa kipindi hicho, sawa na asilimia 43 ya mapato yasiyolindwa ambayo ni Sh689.5 bilioni.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kwa kutumia asilimia 65, Chalinze asilimia 62, Arusha asilimia 62, huku Manispaa ya Moshi ikitumia kidogo zaidi (asilimia 34), Kinondoni asilimia 47 na Morogoro asilimia 49.

Kuhusu mikopo ya asilimia 10 ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, Bashungwa alisema halmashauri 48 zimechangia asilimia 10 au zaidi, 135 zimechangia asilimia tano hadi tisa na halmashauri moja imechangia chini ya asilimia tano.

Kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni kigezo kingine ambacho halmashauri zilipimwa nacho, ambapo Bashungwa alisema Wilaya ya Mtwara imeongoza kwa kutekeleza hoja 92 kati ya 102 zilizotolewa na mamlaka hiyo.

Iliyofuata ni Wilaya ya Siha iliyotekeleza hoja 65 kati ya 75, aidha Wilaya ya Bibaramulo, Serengeti na Nyang’hwale zimefanya vibaya kwa kutekeleza mapendekezo kwa asilimia 12.

Hata hivyo, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Wilaya ya Muleba, Kyerwa na Karagwe hazijatekeleza mapendekezo na kufunga hoja za CAG.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuwaapisha Wakuu wapya wa Mikoa, Ikulu jijini Dar es Salaam, alizitaka halmashauri kupitia upya viwango vya ukusanyaji mapato na kuziba mianya ya upotevu.

“Halmashauri zikapitie upya viwango vya ukusanyaji mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ili kujihudumia na kujikimu kwa mahitaji ya kiofisi,” alisema.

Advertisement