Madereva serikalini waonywa

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Tabora limewaonya baadhi ya madereva wa magari ya Serikali wasiofuata sheria kwa kisingizio cha kuwa na haraka.

  


Tabora.  Jeshi la Polisi mkoani Tabora limewaonya baadhi ya madereva wa magari ya Serikali wasiofuata sheria kwa kisingizio cha kuwa na haraka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Safia Jongo amezungumza leo Jumamosi Septemba 25, 2021 akisema madereva hao wanakimbiza magari wakiwa wamewasha taa na kupitia katika njia zisizoruhusiwa kwa madai ya kuwa na haraka.

Amesema watawakamata madereva hao na ikibidi kuwanyang'anya leseni zao.

"Sheria ni msumeno nawasihi madereva wa Serikali wawe wanafuata Sheria bila shuruti kwani wale watakaokiuka, tutawachukulia hatua na hata kuwanyang'anya leseni zao"Amesema

Bodaboda

Kamanda Jongo amesema zimekamatwa bodaboda 474 mwezi Septemba kwa makosa mbalimbali.

Amesema wameanza kampeni ya kuwakamata wanaopandisha abiria zaidi ya mmoja maarufu kama mishikaki na wale wanaokubali kupandishwa pamoja na wasiovaa kofia ngumu.

"Tutaanza kuwakamata abiria na dereva wasiovaa kofia ngumu na wale wanaopakizana mishikaki" amesema.


Imeandikwa na

Robert Kakwesi,mwananchi