Madiwani Handeni mji wagoma kupitisha rasimu ya bajeti

Madiwani Handeni mji wagoma kupisha rasimu ya bajeti

Muktasari:

  • kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa halmashauri ya mji Handeni mkoani Tanga mwaka 2015, madiwani wamegoma kuipitisha rasimu ya bajeti wakidai ina upungufu na kuagiza wataalamu  serikalini kuiboresha.

Handeni. Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa halmashauri ya mji Handeni mkoani Tanga mwaka 2015, madiwani wamegoma kuipitisha rasimu ya bajeti wakidai ina upungufu na kuagiza wataalamu  serikalini kuiboresha.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mussa Mkombati amesema katika rasimu hiyo ya bajeti kuna ongezeko la Sh46 milioni  ambayo madiwani hawakuipitisha na kushangazwa kuiona kwenye kabrasha kwa baadhi ya idara kuongezewa fedha.

Amesema rasimu hiyo haijaorodheshwa fedha kwa ajili ya kumalizia baadhi ya miradi ya maendeleo kama zahanati, vituo vya afya na madarasa.

"Kuna maelekezo tulitoa katika rasimu hiyo ya bajeti iwepo fedha kwa ajili ya kuweka duka maalum la dawa hospitali na kununua trekta kwa ajili kukusanya takataka zinazozagaa mjini lakini vyote hivyo havikuwepo,  pia kuna ongezeko la Sh46 milioni hatufahamu limetokea wapi,” amesema Mkombati.

Kutokana na upungufu ulioonekana kwenye rasimu hiyo ya bajeti, madiwani 16 kati ya 17 wa halmashauri ya mji Handeni wameikataa bajeti hiyo na kutaka ikarekebishwe.

Kaimu mkurugenzi halmashauri hiyo,  Fabian Massawe amesema wamepokea agizo hilo la madiwani na wanakwenda kufanya marekebisho ya rasimu hiyo ya bajeti.