Madiwani Tanganyika wacharuka, wataka DED asimwangushe Rais
Muktasari:
- Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika waitaka ofisi ya Mkurugenzi kutowachonganisha na wananchi kwa kushindwa kutekeleza miradi kwa wakati inayotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani.
Katavi. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, wameitaka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kutowachonganisha na wananchi kwa kushindwa kukamilisha miradi inayotekelezwa, kupitia mapato ya ndani.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani hao leo Septemba 13,2023 katika Mkutano Mkuu wa kufunga mwaka uliopita 2022/2023, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hamad Mapengo, amesema kutokamilika kwa miradi hiyo kunazua maswali kwa wananchi.
Amesema licha ya halmashauri hiyo kuvuka lengo la ukusanyaji mapato ya ndani zaidi ya asilimia 100, lakini fedha hizo haziwafikii wananchi kwa kuwa miradi mingi haijakamilika, na kwamba hali hiyo ni kumwangusha Rais.
“Majengo mengi yamejengwa yapo kwenye maeneo tofauti lakini hayajakamilika tatizo ni nini? Tunaomba mkamilishe wananchi wanahoji, tunakosa majibu, mnatujengea hali ngumu kwenye uchaguzi 2025,” amesema na kuongeza;
“Baada ya kupokea fedha za Uviko, tumejenga majengo mengi sana, lakini baadaye Rais Samia Suluhu Hassan, alileta fedha za kujenga nyumba za walimu wakuu na matundu ya vyoo, pia miradi hiyo haijakamilika.”
Akitolea mfano wa Shule ya Msingi Katongwe, mwenyekiti huo amesema: “Hiyo shule ipo kwenye kwenye kata yangu, matundu 11 ya vyoo hayajakamilika, nendeni Maghorofani, Igalukilo na maeneo mengine, acheni kumuangusha Rais.”
“Wakati zinakuja hizo fedha mlisema mmeshindwa kupeleka vifaa kwa sababu barabara hazipitiki wakati wa masika hakuna kilichofanyika badala yake tunaingia tena msima wa mvua,” amesema.
Mbunge wa Jimbo hilo Seleman Kakoso akaunga mkono hoja hiyo akisisitiza halmashauri kutekeleza miradi kwa wakati ili kutimiza azma serikali na chama.
“Nilifanya ziara kwenye kata, vijiji na vitongoji kuna maboma mengi hayajakamilika kwa maana ya kwamba fedha za mapato ya ndani hazijaenda kwa wananchi,”
“Mnatuchonganisha na wananchi, niombe Mwenyekiti hakikisha unamsimamia mkurugenzi ili apeleke fedha ili kukamilisha miradi,”amesema Kakoso
Suala lingine lililoibuka katika mkutano huo ni la ucheleweshwaji wa mikutano ya baraza inayodaiwa kutokwenda na ratiba na kusababisha Madiwani kushindwa kutekeleza majukumu yao.
“Leo tunafanya mkutano wa kufunga mwaka uliopita muda wake umekwisha muda mrefu, tunaingia na ratiba zilizopitwa na wakati tunaomba mwaka huu mbadilike,” amesema Diwani Kibigasi.
Eliza Joackim, Mkazi wa Wilaya ya Tanganyika, amesema kutokamilika kwa miradi kwa wakati inaathiri maendeleo ya eneo husika na ina sababisha wananchi wakose imani na serikali yao.
“Tunamshukru sana Rais Samia Suluhu Hassan amejenga shule nzuri sana, vituo vya kutolea huduma za afya, tunaomba wasimamizi wake wawe makini wasimuagushe watimize majukumu yao,” amesema Eliza.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Alex Mrema amekiri kuwepo hali hiyo akiahidi kufanyia kazi changamoto hizo.
“Nikiri zinaweza kuwepo changamoto zinazopelekea kucheleweshwa vikao, madiwani watapata taarifa na sababu husika,”
“Sisi kama halmashauri tutaendelea kusimamia miradi inayotekelezwa kupitia fedha za serikali kuu, nikuhakikishie asilimia 40 ya mapato ya ndani zitakwenda kwenye miradi,” amesema Mrema.