Madiwani wataka mkurugenzi kuwapangia 'trip'
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, wakijadili mambo mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.
Muktasari:
- Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro limemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kupanga safari ya madiwani kwenda kujifunza katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuona namna wanavyonufaika na msitu wa nusu maili baada ya wao kuingia ubia na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Rombo. Baraza la madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro limemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kupanga safari ya madiwani kwenda kujifunza katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuona namna wanavyonufaika na msitu wa nusu maili baada ya wao kuingia ubia na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Ombi hilo lilitolewa katika baraza la kawaida la madiwani la halmashauri hiyo wakati lilipoketi kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika halmashauri hiyo.
Akizungumzia kuhusu hifadhi ya msitu wa nusu maili unaomilikiwa na halmashauri hiyo, Diwani wa Kata ya Katangara Mrere, Venance Mallel amesema hawaoni faida inayotokana na msitu huo ambao kwa sasa unamilikiwa na halmashauri hiyo. Wanataka kuona msitu huo ukileta manufaa na tija kama ilivyo kwa halmashauri nyingine.
"Tunaomba baraza hili liridhie madiwani waende katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwenda kujifunza namna ambavyo wananufaika na msitu wa nusu maili ambao halmashauri wameingia mkataba na TFS. Kuna asilimia kadhaa zinaingia halmashauri na mapato yake ni makubwa kuliko msitu wetu wa nusu maili hapa Rombo," amesema
Amesema endapo hilo litafanyika, watakaporudi watakuwa wamejifunza mambo mengi ambapo wataweza kuishauri halmashauri namna bora ya kupata manufaa kutokana na msitu huo ikiwa ni pamoja na kuingia ubia na TFS.
"Endapo tutaingia ubia na TFS naamini halmashauri hii mapato yake yataongezeka, tutaepuka siku moja wale waliotuazima msitu ule kuuchukua kwa sababu tumeshindwa kuutunza hivyo naomba baraza hili liridhie hivyo," amesema.
Ameongeza "Kabla mwezi wa saba haujafika tunaomba madiwani pamoja na wataalamu wa halmashauri hii twende Ukerewe kujifunza namna ambavyo halmashauri hiyo inavyonufaika kutoka TFS na wataalam baada ya kutoka kule waangalie namna ya kuingia mkataba na msitu wetu wa nusu maili na TFS kama itakavyoshauriwa hapo baadaye," amesema.
Naye diwani wa kata ya Kitirima, Amedeus Cyprian amesema wanataka kuona msitu huo ukileta tija na manufaa makubwa katika halmashauri hiyo na kwamba endapo wataenda Ukerewe kujifunza watakaporudi watarudi na mawazo mapya ambayo wataweza kuishauri halmashauri namna ya kuendesha msitu huo kwa tija.
"Tunataka twende tukajifunza ili tukirudi tuweze kuishauri halmashauri vizuri namna ambavyo tutaweza kuuendesha ule msitu vizuri hivyo kwa mwaka mmoja tunaweza kupata Sh400 milioni na zaidi," amesema.
"Lazima tuingie gharama ndipo tuweze kuvuna, ziara huu ni muhimu sana tunaomba ifanyike ili tukirudi hapa tuone namna nzuri ya kusimamia msitu au kuingia mkataba na TFS tukapata mapato," amesema.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Godwin Chacha alisema hawazuii madiwani kwenda kujifunza na kwamba wachague kile ambacho kinaweza kufanyika ndani ya uwezo wa halmashauri hiyo.
"Ni lazima wakati tunafanya maazimio haya tuaangalie na gharama za kwenda kule Ukerewe, tuchague kile ambacho ni sahihi kufanyika ndani ya bajeti, hatuzuii watu kujifunza, tumelichukua tulichakate na kulileta katika vikao vyetu yafanyike maazimio kulingana na sheria, taratibu na uwezo wa halmashauri na majukumu yaliyopo mbele yetu," amesema