Maeneo matatu kinara utapeli wa ardhi yatajwa Kibaha

Mkazi wa Muheza, Vitusi Mkoromo akizungumzia uwepo wa mataperi wa ardhi kwenye maneo yao. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Wimbi la matapeli wa ardhi laendelea kuwatesa wananchi Kibaha walia wakosa amani wadai umasikini kuwasonga.

Kibaha. Wimbi la watu wanaojihusisha na utapeli wa ardhi limeendea kuwatesa wakazi wa Kata ya Tangini Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani hali ambayo inachangia kuwarudisha nyuma  kimaendeleo katika nyanja ya uchumi na kuzalisha migogoro isiyoisha.

Maeneo ambayo ni kinara kwa utapeli wa ardhi ni Mtaa wa Muheza, Machinjioni na Tangini.

Hayo yamebainishwa Jumatano Januari 25, 2023  wakati wa mkutano wa wanachi Mtaa wa Muheza  ambapo wameziomba mamlaka mbalimbali kuingilia kati ili kuwasaidia na kadhia hiyo.

"Mimi ni mmoja wa wajumbe wa Baraza la Ardhi na nyumba la usuluhishi Mtaa wa Muheza lakini kila kesi 10 za ardhi zinazokuja ofisini 8 zinatoka Mtaa wa Muheza hivyo Muheza imekithiri kwa utaperi wa ardhi hali ni mbaya," amesema Richard Mangi.

Amesema kuwa migogoro mingine ilisabaishwa na baadhi ya viongozi wa Serikali za Mtaa waliopita kwani walikuwa wanashirikiana na mataperi kuuza ardhi hivyo kwa sasa Muheza amani hakuna," amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Usuruhishi Kata ya Mailimoja, Mosi Musiba amesema kuwa matapeli hao wanatumia njia wanapouza ardhi ikiwemo kuchonga mihuri ya Serikali za Mitaa na kutengeneza nyaraka za kisheria hali ambayo inawaaminisha watu.

"Lipo wimbi kubwa hao watu ukikutana nao humo ndani yao kunakuwa na muuzaji pia shahidi mwingine mwanasheria na wana mihuri ya bandia hivyo kwa mwananchii mwenye uelewa mdogo lazima aingie chaka," alisema.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mtaa wa Muheza, Mwanawetu Saidi aliwataka wakazi wa mtaa huo kutotumia njia za mkato pindi wanapohitaji kununua maneo ya ardhi na badala yake watumie ofisi ya Serikali ambako watapewa utaratibu sahihi unaotakiwa.

"Hao watu matapeli wamekuwa wakisumbua wananchi na pia kuipaka matope Serikali hasa wanapotengeneza mihuri ya bandia inayosomeka Serikali jambo ambalo tumeendelea kupambana nalo ikiwemo baadhi kukaamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sharia," alisema.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mkoa wa Pwani, Joyce Mnkhoi alisema  kuwa ili wananchi hao kuepukana na migogoro hasa ya ardhi ni vizuri kufuata sheria za nchi pindi wanapohitaji kununua viwanja kwani masuala ya kesi yanarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kuchochea uvunjifu wa amani kwa jamii.