Mafuriko ya watalii Dar, Arusha

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na mafanikio ya ziara rasmi ya kiserikali iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan nchini Oman hivi karibuni. Mkutano huo ulifanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu

Muktasari:

Uwekezaji na utangazaji wa utalii unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatajwa ni miongoni mwa njia zitakazosaidia kukuza utalii na kuwavutia watalii wengi kuja hapa nchini.

Dodoma/Dar. Wakati Serikali ikitangaza matunda ya filamu ya Royal Tour, ikiwemo kuongezeka kwa watalii, Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha ametilia shaka takwimu zinazotolewa kuhusu sekta ya utalii, akisema zinatofautiana na uhalisia.

Akizungumza na waandishi wa habari aliowaita Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus ambaye aliambatana na mawaziri na makatibu wakuu alisema ziara iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan nchini Oman hivi karibuni imekuwa na mafanikio makubwa.

Katika mkutano huo, Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Profesa Godius Kahyarara alisema ongezeko la watalii hapa nchini ni moja ya matunda ya filamu ya Royal Tour.

Hata hivyo, Profesa Kahyarara katika mazungumzo yake hayo hakutaja idadi ya watalii walioongezeka zaidi ya kuainisha asilimia za ongezeko hilo.

Alisema filamu ya Royal Tour imeongeza asilimia 280 ya watalii jijini Dar es Salaam na asilimia 340 Arusha.

“Katika upande wa ndege inaonyesha miruko ya ndege hasa zinazoingia nchini imeongezeka ambapo kwa takwimu zilizochukuliwa Juni, 2021 hadi Juni 2022 inaonyesha baadhi ya mashirika makubwa ya ndege imeongezeka kutoka 93 hadi 124 kwa wiki,” alisema.

Filamu hiyo, Kahyarara alisema mauzo ya nje yameongezeka kutoka Dola za Marekani 7 bilioni hadi Dola 10 bilioni.

Alisema uwekezaji pia umeongezeka kufikia Dola za Marekani 9 bilioni kipindi cha Machi mwaka jana hadi Juni mwaka huu, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana ambapo ulikuwa ni Dola za Marekani 1 bilioni.

Kwa mujibu wa Kahyarara, kupitia filamu hiyo kuna mwekezaji amejitokeza anayetaka kuwekeza kwa kujenga hoteli za kitalii katika hifadhi mbalimbali, zikiwemo Serengeti, Arusha, Ngorongoro, Mwanza na Zanzibar.

Hata hivyo, alisema mikakati inafanyika kuzifungua hoteli zilizokuwa zimefungwa.


Hoja ya Nahodha

Kinyume na kauli hiyo ya Serikali, Nahodha alishuku ukusanywaji wa takwimu katika sekta ya utalii na kubainisha kuwa wingi wa vivutio Tanzania haulingani na mapato yanayokusanywa.

Alisema zipo nchi zenye idadi chache ya vivutio lakini inakusanya mapato mengi ya utalii, lakini kwa Tanzania ni kinyume chake.

“Mheshimiwa Spika, nchi yetu imebarikiwa sana kuwa na vivutio vya utalii, lakini kwa bahati mbaya idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu na kiwango cha mapato hakiendani na hali ilivyo, zipo nchi zinazotuzunguka zina vivutio vichache na mapato ni makubwa,” alisema.

Alisema kati ya ukusanywaji takwimu, ubora wa huduma au gharama za huduma za utalii, kuna eneo lina changamoto inayohitaji kupatiwa ufumbuzi.

Kwa mujibu wa Nahodha, Tanzania bara huingiza watalii 800,000 kwa mwaka wakati Zanzibar huingiza watalii 500,000 ilhali ina vivutio viwili ambavyo pia vinapatikana Tanzania bara.

“Namna inayotajwa kwa upande wa Bara ni ndogo sana ambayo haiendani na uhalisia, kwani Zanzibar ina magofu ya kihistoria na fukwe ambavyo pia vipo kwa Bara lakini pia upande wa pili kuna utalii wa mbuga za wanyama pia,” alisema.

Ili kukusanya mapato vema ya utalii, Nahodha alipendekeza Serikali kuutangaza zaidi utalii kupitia balozi zake zilizopo nje ya nchi.

Alipendekeza kuwepo mfumo wa ukusanyaji takwimu za utalii na kuunganisha na mifumo mingine serikalini, kadhalika kuimarisha chuo cha utalii kama ilivyo katika nchi jirani.


Maoni ya mdau

Alipoulizwa kuhusu ongezeko la idadi ya watalii nchini, Katibu Mtendaji wa chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Sirili Ako alisema kuna ongezeko la wageni lakini hana takwimu rasmi kuhusu ongezeko hilo.

“Ni kweli wageni wanaongezeka lakini sina takwimu hapa ni kwa kiwango gani lakini wanachama wetu wanathibitisha kuna ongezeko la inquiries (maulizo) ya wageni wanaotaka kuja Tanzania. Kwa hiyo ongezeko lipo,”alisema Ako.

Imeandikwa na Juma Issihaka, Mariam Mmbwana (Dar) na Abel Chidawali (Dodoma)