Mafuriko yabomoa nyumba 117 Mtwara

Thursday January 14 2021
mafurikopic

Nyumba zikiwa zimizingirwa na maji katika eneo la Chuno kufuatia mvua iliyonyesha mkoani Mtwara na kusababisha mafuriko. Picha na Florence Sanawa

By Florence Sanawa

Mtwara. Nyumba 117 zimebomoka katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na watu kadhaa kukosa makazi huku nyumba 315 zimezingirwa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema jana kuwa watu hao ambao hawana makazi wamehifadhiwa kwa jamaa zao.

Hata hivyo, alieleza hakuna, ambaye alikuwa ameripoti kwenye kambi zilizoandaliwa na Serikali katika shule na vyuo mbalimbali.

Byakanwa alisema nyumba zilizokuwa zimeharibika zilikuwa za maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, ambayo sehemu yake kubwa ilikuwa imeathirika na mafuriko hayo.

Alisema hali si nzuri na kushauri wananchi wafike maeneo yaliyopangwa ili kusaidiwa kwa urahisi zaidi hasa huduma za kibinadamu.

“Unajua katika maeneo ya Matopeni, Likonde, Mangamba na Chipuputa sehemu kubwa ya nyumba zimezungukwa na maji na taarifa tuliyonayo ya mamlaka ya hali ya hewa ni kwamba mvua zitaendelea kunyesha.

Advertisement

“Wananchi wanapaswa kuendelea kutoka katika maeneo yaliyojaa maji na wafike katika maeneo yaliyotengwa kwa usalama wao ili kujua kama kuna mahitaji ya msingi ya kibinadamu tuweze kuwasaidia,”aliongeza Byakanwa.

Naye Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Mtwara, Christina Sunga alisema hadi sasa kwa kata ya Naliendele pekee zaidi ya nyumba 55 zimezingirwa maji, huku nyumba tatu zimebomoka.

Sunga alisema tatizo hilo halijatokea Manispaa ya Mtwara pekee, aliongeza halmashauri ya wilaya ya Mtwara zaidi ya nyumba 70 zimebomoka huku vyoo 50 vikititia ambapo kanisa moja limetajwa kubomoka. Sunga alisema kuwa mbali na maji kujaa katika nyumba za watu, pia hali si nzuri katika barabara za ndani ya halmashauri hiyo.

Pia watu walioathirika na mafuriko wamesimulia namna walivyoathirika na mafuriko hayo, ambapo Mwajuma Juma, anayeishi Kiangu alisema kuwa mvua hizo zilisabababisha ajiokoe mwenyewe hivyo kupoteza mavazi, vyakula na mahitaji mengine muhimu.

“Hapa nilipo sina kitu chochote yaani nilikuwa na kila kitu ndani lakini leo hii hata nguo ya kuvaa kubadilisha sina, hata chakula sina sijui hali ikoje kwenye nyumba yangu na siwezi kwenda kwa kuwa maji bado ni mengi ,” aliongeza.

“Unajua hii taarifa ya kwamba kuna tahadhari ya mvua kunyesha sikuiona wala sikuisikia, sio wote tunaingia kwenye mitandao ama tuna televisheni, Mamlaka ya Hali ya Hewa waangalie namna bora ya kutoa taarifa zao kwa wananchi,” alieleza Mwajuma kwa masikitiko.

Naye Rahimu Mohamed, mkazi wa mtaa wa Kiyangu alisema hali si nzuri na hajui hali ya vitu vyake ndani ikoje. “Yaani jana hali bado haiko poa, tulikimbia tukiwa na nguo moja hadi sasa hatuwezi kubadilisha kwa kuwa mabegi yote yamelowa hata uokoaji ulikuwa mgumu. Sina hakika na madaftari na vitu vingine hata chakula malazi bado ni shida kwetu tumejihifadhi kwa marafiki.

“Juzi saa 4.00 usiku maji yalianza kuingia ndani, hatukupata usingizi mpaka asubuhi, hali haikuwa nzuri tuliamua kuviweka vitu juu ya dari ili kuvinusuru hasa vyakula na madaftari lakini vingine tulishindwa kwa kuwa maji yalikuwa yakijaa kwa kasi,” alisema Rahma.

Advertisement