Magari 24,521 yanaswa kwa malimbikizo ya faini barabarani Tanzania

Magari 24,521 yanaswa kwa malimbikizo ya faini barabarani Tanzania

Muktasari:

  • Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini Tanzania, Wilbroad Mutafungwa amesema katika kipindi cha siku tano zilizopita, idadi ya magari 24,521 yamekamatwa kupitia oparesheni ya ukamataji wa magari yenye malimbikizo ya faini zinazotokana na makosa ya barabarani

Dar es Salaam. Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini Tanzania, Wilbroad Mutafungwa amesema katika kipindi cha siku tano zilizopita, idadi ya magari 24,521 yamekamatwa kupitia oparesheni ya ukamataji wa magari yenye malimbikizo ya faini zinazotokana na makosa ya barabarani. 
Akizungumza na wanahabari leo Januari 25, 2021 Jijini Dar es Salaam, Kamanda Mutafungwa amesema oparesheni hiyo iliyoanza Januari 20, 2021 itaendelea katka mikoa yote hadi Februari 20, mwaka huu chini ya utekelezaji wa Kanuni za faini ya makosa barabarani za mwaka 2011. 
“Makosa yanayosababisha zaidi uvunjifu huo wa sheria za barabarani ni pamoja na madereva kutumia mwendokasi maeneo ya makazi, kutosimama katika mistari ya zebra na ku-overtake(kulipita gari kwa mbele wakati wa mwendokasi), “alisema Mutafungwa.
Katika oparesheni hiyo, maofisa wa jeshi hilo wakiongozana na baadhi ya maofisa wa Mawasiliano Mamlaka ya Mapato Tanzania wameendelea na ukaguzi wa magari mitaani, maeneo ya kupaki magari, maeneo ya kutengeneza magari(gereji) au maeneo mahali penye mzunguko wa magari.
“Sasa kutokana mazingira hayo tumeamua kuanzisha msako mkali ili kuhakikisha madeni yaliyotokana na tozo za usalama barabarani yanalipika kwa maana ya kuwapata wahusika na magari husika ili walipe madeni, kwa kufanya hivyo adhabu ndio itakuwa imekamilika tuliyoitoa,”amesema. 
Mutafungwa amesema miongoni mwa sababu za malimbikizo ya madeni hayo ni pamoja na wamiliki wa magari kukosa utamaduni wa kukagua magari baada ya kuyaazimisha kwa madereva wenzao na wamiliki kutofanya ukaguzi wa magari baada ya kuwaachisha kazi madereva. 
Kwa mujibu wa Mutafungwa, tayari kiasi cha Sh1.4bilioni kati ya Sh11bilioni zimeshakusanywa ndani ya siku hizo tano ikiwa ni siku 25 zimebakia kabla ya kufunga  oparesheni hiyo inayoendana na usimamizi wa sheria pamoja na utoaji wa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri nchini.