Magufuli azindua chuo cha Veta Mkoa wa Kagera

Muktasari:

Rais Magufuli aliyeanza ziara mkoani Kagera amezindua ujenzi wa chuo cha ufundi stadi (Veta) mkoani humo na kuzindua shule ya sekondari ya Ihungo iliyobomolewa na tetemeko.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha Veta mkoa wa Kagera pamoja na kuzindua shule ya sekondari ya Ihungo iliyopo mkoani humo ambayo ilibomolewa na tetemeko la ardhi la mwaka 2016.

Rais Magufuli amefanya hayo leo Januari 18 akiwa kwenye ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Kagera ikiwa ndiyo ziara yake rasmi ya kwanza tangu alipochaguliwa kwa kipindi chake cha pili katika uchaguzi wa mwaka jana.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa shule ya Ihungo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema ujeszi wa shule hiyo umegharimu Sh10.9 bilioni na kuifanya kuwa shule bora hapa nchini.

Amesema wameanza kuyaona matokeo ya uwekezaji wa serikali katika sekta ya elimu kwani sasa viwango vya utoro vimepungua kwa asilimia asilimia tatu lakini wanafunzi wameongezeka kati ya asilimia 10 hadi 30.

“Ufaulu nao umeongezeka, sasa mkoa wa Kagera ufaulu ni asilimia 88.8 kwa shule za msingi na ufaulu wa sekondari umefikia asilimia 90,” amesema Gaguti wakati akitoa salamu za mkoa kwa Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo amemhakikishia Rais Magufuli kwamba wateule wake wataendelea kuchapa kazi ili kuhakikisha azma yake kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu inafanikiwa.

“Sisi uliotupa dhamana hii tutafanya kazi usiku na mchana katika kukusaidia ili kufikia azma yako ya kila Mtanzania anapata elimu,” amesema Jafo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa shule ya Ihungo.