Magufuli: Baada ya uchaguzi Serikali imejipanga kununua vichwa vya treni

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

Serikali imepanga kununua vichwa vipya vya treni 39 kwa ajili ya njia kuu na vingine 18 vya treni sogeza sogeza, mebehewa 800 ya kusafirishia mizigo na 37 abiria

 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema baada ya uchaguzi kukamilika Serikali imejipanga kununua vichwa vya treni 39 kwa njia kuu na vingine 18 vya treni sogeza sogeza.

Mbali na hilo pia imejipanga kununua mebehewa 800 ya kusafirishia mizigo na 37 abiria

Amesema hayo katika uzinduzi rasmi wa treni ya abiria inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Arusha kupitia Moshi na Tanga iliyokuwa imeacha kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 30.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwa mfano Afrika kwa mashirika yanayofanya biashara na kufanya kazi kwa kuhudumia wananchi wake ikiwemo wanyonge.

“Wito wangu kwenu (TRC) hakikisheni mnaendelea kuimarisha na kuboresha huduma zenu na gharama zenu zinakuwa chini na kupiga rushwa ili watanzania waweze kunufaika na usafiri huu,”

“Watanzania pia hususani wakazi wa mikoa ya kaskazini kutumia reli hii vizuri ili kuweza kunufaika nayo, serikali tayari imetekeleza wajibu wake sasa ni wajibu wa Watanzania wote kuweza kuilinda,”amesema.

Amesema kuna wakati aliwahi kusikia njama za watu wakitaka kuharibu reli hivyo aliwataka Watanzania kulinda miundombinu ya treni inatunzwa ili kuweza kuwasaidia.

“Ujio wa treni hii hapa Arusha, uchumi wake utapanda, watu watafanya biashara, hata mama lishe watapeleka vyakula vyao kwa viongozi wa treni na abiria wanaoteremka, wenye nyumba za kulala wageni watapata wateja kwa mpigo hivyo ujio wa treni hii ni suluhisho kwa ajili ya kujenga uchumi wa maeneo haya,” amesema Magufuli.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa Serikali kutokubali kubinafsisha vitu vya msingi katika nchi huku akitolea mfano wa ndege zilizobinafsishwa.

“Tulibinafsisha ndege zote zikaisha tumekuja kuanza upya, tukabinafsisha treni tumekuja kuanza upya, tulikuwa na meli zilizoachwa tangu enzi za baba wa Taifa hazipo, sasa hili liwe ni fundisho, mimi sitakuwa Rais wa Maisha ila natoa ujumbe wangu kwa wale watakaokuja baadaye kuwa hili liwe fundisho,’’

“Hata nchi zilizoendelea mashirika yao ya reli hawajabinafsisha ibaki kuwa ndani ya serikali ili huduma kwa wananchi wanyonge ndiyo itawafikia Wananchi kupitia hiyo treni na vinginevyo,” amesema Magufuli.