Magufuli kuzindua shamba la miti Chato

Magufuli kuzindua shamba la miti Chato

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania,  John Magufuli anatarajiwa kuzindua shamba la miti wilayani Chato mkoani Geita  kesho Jumatano  Januari 27, 2021.

Chato. Rais wa Tanzania,  John Magufuli anatarajiwa kuzindua shamba la miti wilayani Chato mkoani Geita  kesho Jumatano  Januari 27, 2021.

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika kesho saa 2 asubuhi  katika eneo la Butengo wilayani Chato mkoani Geita.

Shamba la miti Chato ni miongoni mwa mashamba 23 ya Serikali yanayosimamiwa na kuendelezwa na wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) na limeanzishwa sehemu ya eneo la msitu mkubwa wa hifadhi ya Biharamulo - Kahama.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya ujio huo mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 69,000 ni la Pili kwa ukubwa baada ya shamba la miti Saohill lenye ukubwa wa hekta 135,900.

Amesema uanzishwaji na uendelezwaji wa shamba hilo unaenda sambamba na malengo ya Serikali ya kuhifadhi mazingira na kuinua uchumi wa nchi na wananchi wake.

Gabriel amesema mradi huo wa upandaji miti ambao serikali imewekeza unatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira na kuchangia uhifadhi wa misitu katika Kanda ya ziwa na nchi kwa ujumla.

Amesema mradi huo utasaidia kuzalisha malighafi ya viwanda vya mazao ya misitu kama vile mbao karatasi, nishati pamoja na kutoa ajira za muda mrefu na mfupi kwa watanzania wote.