Mahabusu sasa kupimwa Covid-19

Mahabusu sasa kupimwa Covid-19

Muktasari:

  • Serikali imesema ili kuzuia maambukizi ya Covid-19 kuingia magerezani, imeanza kuthibiti vituo vya polisi, magereza na mahakama kwa kuhakikisha tahadhari zinachukuliwa maeneo hayo pamoja na kufanya kipimo cha haraka cha Covid -19 kwa mahabusu wote wanaofikishwa gerezani kwa mara ya kwanza.

Dar es Salaam. Serikali imesema ili kuzuia maambukizi ya Covid-19 kuingia magerezani, imeanza kuthibiti vituo vya polisi, magereza na mahakama kwa kuhakikisha tahadhari zinachukuliwa maeneo hayo pamoja na kufanya kipimo cha haraka cha Covid -19 kwa mahabusu wote wanaofikishwa gerezani kwa mara ya kwanza.

Pia imekusudia kutoa kipaumbele cha dhamana kwa mahabusu wenye makosa yanayodhaminika kisheria ili kupunguza msongamano.

Hayo yamesemwa leo Jumapili, Julai 25, 2021 na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi wakati akisoma mwongozo wa udhibiti wa ugonjwa wa corona (uviko-19) kupitia afua ya kuthibiti misongamano katika jamii bila kuathiri shughuli za kiuchumi toleo la kwanza.

“Tumeshaagiza vituo vya Polisi vitatakiwa vinaweka maeneo ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, watumishi na watu wote wanaoingia katika vituo vya polisi wavae barakoa muda wote.

“Wanatakiwa kutoa kipaumbele cha dhamana kwa mahabusu wenye makosa yanayodhaminika kisheria ili kupunguza msongamano na kufanya kipimo cha haraka cha Covid -19 kwa mahabusu wote wanaofikishwa gerezani kwa mara ya kwanza,” amesema Profesa Makubi.

Amesema lazima wahakikishe wanawapima joto la mwili watu wote kabla ya kuingia kituoni na chumba cha mahabusu.

Mahabusu sasa kupimwa Covid-19

“Hii ni pamoja na kuruhusu ndugu mmoja tu kumtembelea mfungwa, kumuona mahabusu katika siku iliyotengwa na kuhakikisha wafungwa na ndugu wote wanavaa barakoa na wanakuwa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.

“Tunaagiza wasikilizaji wa kesi mahakamani wazingatie kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu,” amesema Profesa Makubi.