Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama ilivyoamua kesi kupinga Tume ya Jaji Lila

Muktasari:

  • Uamuzi huo umetolewa jana jioni  Jumatatu, Juni 8, 2026 na Jaji Augustine Rwizile aliyesikiliza shauri hilo baada ya kuridhika kuwa, kuna hoja ya kujadiliwa inayopaswa kuamuliwa na Mahakama



Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma imeruhusu kupingwa mahakamani uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Uamuzi huo umetolewa jana jioni Jumatatu, Juni 8, 2026 na Jaji Augustine Rwizile aliyesikiliza shauri hilo baada ya kuridhika kuwa, kuna hoja ya kujadiliwa inayopaswa kuamuliwa na Mahakama.

Uamuzi uliotokana na shauri la maombi ya ruhusa kufungua shauri la mapitio ya kimahakama (judicial review) kwa lecccngo la kupinga uamuzi wa Rais Samia kufanya uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa tume hiyo.

Shauri hilo lilifunguliwa na mwanaharakati Buberwa Ephraim Buberwa na mwenzake Joseph Daud Mabugo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, makamisha wake watatu.

Makamishna hao ambao ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ni Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.

Tangazo la Rais Samia kuunda tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila kuteua makamishna hao lilitolewa Mei, 18, 2026.

Aliunda tume kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Katika shauri hilo waombaji waliomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama, kuiomba itengue uamuzi huo wa Rais Samia kuwateua makamishna wa tume hiyo, na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo, wakidai kuwa,  hana mamlaka kisheria kufanya hivyo.

Shauri hilo lililosikilizwa jana,  mawakili wa waombaji, Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, waliieleza Mahakama kuwa wateja wao wamekidhi vigezo vyote vitatu vya kupewa ruhusa hiyo kama vilivyokwisha kuwekwa na Mahakama.

Vigezo hivyo ni mwombaji kuonesha kuwa kuna hoja inayohitaji kujadiliwa na Mahakama, kuonesha kuwa ana masilahi katika jambo au uamuzi unaolalamikiwa na mwisho maombi kufunguliwa ndani ya muda yaani miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi au kufanyika kwa jambo linalolalamikiwa.

Hata hivyo, hoja kama waombaji walithitibitisha kuwepo kwa hoja inayotakiwa kujadiliwa, ndio hoja hiyo pekee iliyobishaniwa, hivyo kuibua mvutano mkali wa hoja za kisheria baina ya pande zote, kabla ya Mahakama kumaliza ubishi huo kwa uamuzi huo.

Wakati jopo la mawakili sita wa Serikali lililowawakilisha wajibu maombi wote likipinga vikali kuwa waombaji hawakuweza kuthibitisha kuwepo hoja inayohitaji kujadiliwa katika uamuzi huo wa Rais, jopo la mawakili wawili wa waombaji lilisisitiza kuwepo hoja hiyo.


Uamuzi wa Mahakama

Jaji Rwizile baada ya kusikiliza na kuchambua hoja za pande zote katika uamuzi wake alioutoa jana jioni, alikubaliana na hoja za mawakili wa waombaji, kuwa wamekidhi matakwa ya kisheria kustahili kuruhusiwa kufungua shauri la kupinga uamuzi wa Rais.

Jaji Rwizile kwanza alielezea kwa ufupi namna waombaji walivyokidhi vigezo viwili kati ya vitatu ambavyo havikubishaniwa, kwamba walifungua shauri hilo ndani ya muda na kwamba wana haki kisheria kufungua shauri hilo kwa kuwa, wana masilahi ya kutosha.

Alifafanua uamuzi unaolalamikiwa (uteuzi wa makamishna wa tume hiyo) ulifanyika Mei 18, 2026 na wao walifungua shauri hilo kuomba ruhusa kuupinga uamuzi huo, Mei 24, yaani ndani ya siku saba tu tangu kufanyika uamuzi huo. ‎

‎Kuhusu haki ya kufungua shauri hilo isiishie kwa waombaji walieleza kuwa, Watanzania pia waliathirika na matukio ya vurugu za wakati wa uchaguzi, hivyo wana masilahi na suala wanalolilalamikia.

‎Kuhusu hoja iliyoibua mvutano, yaani kama waombaji walithibitisha kuwepo hoja inayohitaji kujadiliwa, Jaji Rwizile alikubaliana na mawakili wa Serikali kuwa kifungu cha 20 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, kimesema kuwa ili tume ianze kufanya kazi lazima kwanza itangazwe katika Gazeti la Serikali (GN).

Pia, alikubaliana na hoja ya mawakili wa Serikali (wajibu maombi) kwamba, katika tangazo lililoambatanishwa na waombaji katika hati ya maombi yao hakuna mahali ambako limesema kuwa tume hiyo imetangazwa.

Hata hivyo, alisema kuwa wajibu maombi wote walikubali kuundwa kwa tume hiyo na uteuzi wa makamishna, lakini walipinga tu kuwa tume hiyo haiwezi kuzuiwa kutekeleza majukumu yake kwa kuwa, haijatangazwa GN na hivyo haina mamlaka kutekeleza kazi zake na kwamba bado hazijajulikana.

Kwa upande mwingine Jaji Rwizile alikubaliana na mawakili wa waombaji akisema kuwa kwa kuangalia kiapo cha waombaji kilichounga mkono maombi, waombaji wanapinga uteuzi wa makamishna wa tume hiyo.

Pia, alisema kuwa kwa mujibu wa kiambatanisho cha tatu cha waombaji kilichopewa jina la Matwiga 3 (Taarifa ya Serikali/Ikulu kwa umma kuhusu uundwaji na uteuzi wa makamishna hao), tume hiyo imeundwa chini ya Sura ya 32 (Sheria ya Tume za Uchunguzi).

Aliongeza kuwa, kiambatanisho hicho hicho kimeeleza wazi kuwa uundwaji wa tume hiyo ya Jaji Lila umetokana na mapendekezo ya tume iliyotangulia (Tume ya Jaji Chande).

‎Hivyo, Jaji Rwizile alisema kuwa kwa kusoma tu kiapo cha waombaji na viapo kinzani vya wajibu maombi kuna hoja ya msingi inayobishaniwa, kama Rais ana mamlaka kuunda tume za aina hiyo.

‎Alisisitiza kuwa, kwa sababu hiyo hiyo ndipo hoja ya msingi inayohitaji mjadala inapoibika, ambayo inahitaji kujadiliwa na kutolewa tafsiri na Mahakama.

‎"Hivyo,  nimeridhika kuwa maombi haya yametimiza vigezo vyote na hoja ya kujadili imetimizwa pia," alisema Jaji Rwizile na kuhitimisha uamuzi wake.

"Kwa hiyo Mahakama inakubaliana na maombi haya na inaruhusu waombaji wafungue maombi kusudiwa (maombi rasmi ya mapitio ya kimahakama kupinga uamuzi wa Rais) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya leo (jana) kwa mujibu wa sheria."

Jopo la mawakili wa Serikali waliowawakilisha wajibu maombi wote liliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo akisaidiwa na Wakili wa Serikali Wakuu, Vivian Method aliyewasilisha hoja za kupinga shauri hilo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola.

Wawakili wengine katika jopo hilo walikuwa Wakili wa Serikali Mkuu, George Kalenda, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edwin Webiro na Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha.